RMO Tanga: Chanjo ya UVIKO-19 aina ya Sinopharm dozi 46,000 imesambazwa vituoni

NA YUSUPH MUSSA

MGANGA Mkuu wa Mkoa wa Tanga Dkt. Jonathan Budenu amesema chanjo ya UVIKO 19 Awamu ya Pili aina ya Sinopharm kutoka nchini China, ambapo chanjo ya dozi ya awali kwa Mkoa wa Tanga wamepokea 46,000, tayari imesambazwa kwenye vituo vyote vya chanjo kwenye mkoa huo ikiwemo hospitali, vituo vya afya na zahanati.
Akizungumza na mwandishi wa habari hizi Leo Oktoba 26, 2021 ofisini kwake jijini Tanga, Dkt. Budenu alisema baada ya kumaliza dozi ya awali, watapokea dozi ya pili pia 46,000 ili kukamilisha dozi kwa wananchi 46,000 wanaotarajiwa kuchanjwa. Hadi Oktoba 24, 2021, tayari dozi 46,000 za awali zimeshasambazwa kwenye vituo vya chanjo katika halmashauri zote 11 za mkoa huo.

"Mkoa wa Tanga tumepokea chanjo ya UVIKO 19 aina ya Sinopharm dozi 46,000. Dozi hiyo ni ya awali, ambapo tutakapomaliza, tutaletewa nyingine dozi 46,000 kwa ajili ya kukamilisha dozi. Dozi ya chanjo ya Sinopharm ni tofauti na Jensen ya J&J kutoka Marekani, kwani chanjo ile ulikuwa ukichanja mara moja unakuwa umemaliza, lakini hii ya Sinopharm unatakiwa kurudia mara ya pili ili kukamilisha dozi.

"Na kuchoma chanjo ya kwanza hadi kurudia chanjo ya pili tumeweka kuanzia siku ya 21 hadi siku ya 28 tangu kuchoma ya awali. Tumeweka hiyo wiki moja ili mtu aweze kuchagua ni siku gani atakwenda kupata chanjo ya pili. Na tayari chanjo hiyo tumesambaza kwenye vituo vyote vya chanjo kwenye halmashauri zote 11 za mkoa wa Tanga," amesema Dkt. Budenu.

Dkt. Budenu alisema kama walivyofanikiwa kwenye Chanjo ya UVIKO 19 Awamu ya Kwanza ya Jensen iliyotengenezwa na J&J ya Marekani, ambapo Mkoa wa Tanga ulipokea chanjo 35,000, na waliweza kukamilisha ndani ya muda uliopangwa, na zoezi hilo kufanikiwa kwa asilimia 90, ametaka ule ushirikiano uliooneshwa na viongozi wa kisiasa, viongozi wa dini, watendaji, wataalamu wa afya na wananchi, ukaonekane tena kwenye chanjo hiyo ya Awamu ya Pili ya Sinopharm.

"Kama tulivyofanikiwa kwenye Chanjo ya UVIKO 19 Awamu ya Kwanza ya Jensen iliyotengenezwa na J&J ya Marekani, ambapo Mkoa wa Tanga tulipokea chanjo 35,000, na tuliweza kukamilisha ndani ya muda uliopangwa, kwani tulianza zoezi hilo la chanjo Agosti 3, 2021 na kukamilisha Oktoba 9, 2021, hivyo kukamilisha kabla ya muda wa mwisho wa Oktoba 14, 2021, na zoezi hilo kufanikiwa kwa asilimia 90.

"Ni kweli zoezi hilo lilisuasua miezi miwili ya awali, na hapo ndipo tulipopoteza ile asilimia 10 sababu watu walikuwa hawajapata elimu ya UVIKO 19. Lakini katika siku 14 za uelimishaji kuanzia Septemba 26, 2021, kwa Wakuu wa Idara na Vitengo, wahudumu wa afya, viongozi wa siasa, dini, watumishi, watendaji kwenye kata na vijiji pamoja na wananchi, zoezi hilo lilifanikiwa na watu kuweza kuchanja, hivyo naamini hata kwenye chanjo ya Awamu ya Pili ushirikiano huo utaendelezwa," amesema Dkt. Budenu.

Dkt. Budenu alisema jambo la kutia moyo, tangu wameanza zoezi hilo Agosti 3, 2021 hadi Oktoba 9, 2021 hakuna mwananchi ambaye amepata madhara kutokana na chanjo hiyo. Hivyo wananchi wanatakiwa kuendelea kuunga mkono chanjo ya UVIKO 19 sababu haina madhara yeyote kwa binadamu.

Dkt. Budenu alisema chanjo ya Sinopharm kwa Mkoa wa Tanga imepangwa hadi Desemba 31, 2021 iwe imekamilka kwa dozi ya awali na dozi ya pili, na ndoto yake ni kuona Mkoa wa Tanga, wananchi wake wanachanja kwa asilimia 70 ili kuwa na kinga imara, kwani kama asilimia 70 ndani ya mkoa watachanja, watawalinda wengine ikiwemo wao wenyewe.

"Tumepanga chanjo ya Awamu ya Pili ambayo sasa tumeletewa Sinopharm, iwe imekamilka Desemba 31, 2021 kwa dozi ya kwanza na dozi ya pili. Napenda wananchi waendelee kupokea chanjo hizi. Serikali ya Awamu ya Sita ya Rais Samia Suluhu Hassan inafanya kila juhudi kupata chanjo na kuchanja wananchi wake wenye umri kuanzia miaka 18 na kuendelea. Naamini siku tutakapochanja asilimia 70 ya wananchi wetu wa Mkoa wa Tanga, tutakuwa tumeondoa hatari ya ugonjwa huu wa UVIKO 19 kwenye jamii,"amesema Dkt. Budenu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news