NECTA yatangaza Shule 10 Bora matokeo ya Darasa la Saba 2021

NA MWANDISHI MAALUM

Baraza la Mitihani la Tanzania (NECTA) limetangaza matokeo ya Mtihani wa Kumaliza Elimu ya Msingi 2021 (Matokeo ya Darasa la Saba mwaka 2021.
Wakati matokeo ya darasa la saba yaliyotangazwa leo yakipokelewa kwa hisia tofauti, Shule ya Msingi Graiyaki ya mkoani Mara ndiyo imeongoza kitaifa katika matokeo hayo huku Mkoa wa Kagera ukiongoza kuingiza shule nyingi katika orodha ya shule 10 bora kitaifa.

Matokeo hayo ya mtihani huo uliofanyika Septemba mwaka huu yametangazwa leo Oktoba 30, 2021 na Baraza la Mtihani Tanzania (Necta) ambapo ufaulu wa ujumla umeongezeka kwa asilimia 6.6 ndani ya mwaka mmoja.

Watahiniwa 907,820 kati ya 1,107,460 waliofanya mtihani huo wamefaulu sawa na asilimia 81.97 ikiwa ni ongezeko la wanafunzi 74,130 ikilinganishwa na mwaka jana.

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde akitangaza matokeo hayo ameitaja Graiyaki ambayo ilikuwa na watahiniwa 50 kushika nafasi ya kwanza kitaifa ikifuatiwa na St Peter Claver ya mkoani Kagera katika nafasi ya pili.

Nafasi ya tatu imeenda kwa Shule ya Msingi Rocken Hill ya mkoani Sinyanga, Kemebos ya Kagera imeshika nafsi ya nne huku Bishop Caeser ya Kagera pia ikishika nafasi ya tano.

Shule ya Msingi Kwema Modern iliyokuwa na watahiniwa 44 ya Shinyanga iko nafasi ya sita, St Magret (Arusha) nafasi ya saba, Waja Springs (Geita) iko katika nafasi ya nane na Kadama ya Geita imeshika nafasi ya tisa.

10 bora hiyo imefungwa na Shule ya Msingi Chalinze Modern Islamic ya mkoani Pwani.
Kwa matokeo hayo, mkoa wa Kagera ndiyo umeingiza shule nyingi (3) ukifuatiwa na Shinyanga na Geita ambayo imeingiza shule mbili kila moja huku mikoa iliyobaki ikiingiza shule moja moja. Pia orodha hiyo imetawaliwa na shule kutoka Kanda ya Ziwa ambapo nane za kanda hiyo zimeingia.

Licha ya ushindani kuwa mkali kuwania orodha hiyo ya dhahabu, Graiyaki imefanikiwa kuvunja rekodi yake ya mwaka 2019 baada ya kuishusha Shule ya Msingi God’s Bridge ya mkoani Mbeya ambayo mwaka jana ilishika nafasi ya kwanza kitaifa.

Shule hiyo ya God’s Bridge haipo kabisa katika 10 bora ya mwaka huu wala Mbeya haijafanikiwa kuingiza shule hata moja katika orodha hiyo.

Shule hiyo imeshika nafasi ya 756 kati ya 11909 katika kundi lake la shule zisizozidi wanafunzi 50.

Katika hatua nyingine, Shule ya Msingi Twiboki ya mkoani Mara ambayo mwaka huu imefanikiwa kutoa wanafunzi watano bora kitaifa, imetupwa nje katika orodha ya 10 bora ambayo katika matokeo ya mwaka jana ilishika nafasi ya tatu.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news