Tanzania yatangaza utalii nchini Ujerumani

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Balozi wa Tanzania nchini Ujerumani, Mhe. Dk. Abdallah Salehe Possi amefungua rasmi Onesho la Utalii la My Tanzania Roadshow 2021 lililoanza leo katika mji wa Frankfurt nchini Ujerumani.
Onesho hilo litafanyika katika nchi tatu zikiwemo Ujerumani, Austria na Switzerland kwa muda wa siku sita kuanzia leo Oktoba 25 hadi Oktoba 30,2021.

Katika onesho hilo Ujumbe wa Tanzania wenye jumla ya kampuni za utalii 28 pamoja na taasisi za TANAPA na Ngorongoro utakutana na Wafanyabiashara ya Utalii (Travel Agents) wapatao 150.

Mhe. Balozi Possi ameahidi kutoa ushirikiano wa kuendelea kutangaza utalii kupitia njia mbalimbali ikiwemo mikutano ya kimtandao.

Sambamba na vyombo vya habari ili kuhakikisha idadi kubwa ya watalii kutoka nchi zinazozungumza lungha ya Kijerumani wanatembelea Tanzania.

Haya yanajiri ikiwa awali pia DIRAMAKINI BLOG imeripoti kuwa, Wizara ya Maliasili na Utalii imesema inatarajia kufanya mkutano mkubwa wa Kimataifa wa Utalii na Masoko (Tourism Marketing) katika Jiji la Arusha, wiki ya pili ya mwezi Novemba mwaka huu.
Waziri wa Maliaslili na Utalii, Dkt. Damas Ndumbaro akizungumza kuhusiana na kufanyika kwa mkutano wa kimataifa wa utalii na masoko wakati akifanya mahojiano maalum ya jinsi Wizara ya Maliasili na Utalii ilivyojipanga kutangaza vivutio vya utalii ilivyonavyo kimataifa kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini kutoka watalii milioni 1.5 hadi kufikia watalii milioni 5 kama ilani ya CCM inavyoelekeza ifikapo mwaka 2025

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt.Damas Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo Jijini Dar es Salaam wakati akifanya mahojiano maalum ya jinsi Wizara hiyo ilivyojipanga kutangaza vivutio vya utalii ilivyonavyo kimataifa kwa lengo la kuongeza idadi ya watalii nchini kutoka watalii milioni 1.5 hadi kufikia watalii milioni 5 kama ilani ya CCM inavyoelekeza ifikapo mwaka 2025.

Waziri Ndumbaro amesema lengo la mkutano huo utakaofanyika kwa muda siku mbili utajadili namna ya kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini kwa kuwakutanisha wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi wakiwemo wamiliki wa makampuni ya Kimataifa ya kutangaza utalii duniani pamoja na Wataalam kutoka Shirika la Umoja wa Kimataifa linaloshughulikia masuala ya utalii Duniani ( UNWTO).

Akizungumzia Washiriki hao, Dkt.Ndumbaro amesema mkutano huo wa kimataifa utatoa fursa kwa Washiriki duniani kote hata kwa wale watakaoshindwa kufika nchini wataweza kushiriki kwa njia ya mtandao pia.
Akizungumzia sababu iliyopelekea Wizara hiyo kuamua kufanya mkutano huo, Dkt.Ndumbaro amesema kama nchi imejaliwa kuwa na vivutio vingi vya utalii na vya kipekee ambavyo havipatikani mahali popote duniani isipokuwa Tanzania lakini vivutio hivyo vimekuwa havijulikani Kimataifa.

”Nilipofika Wizarani baada ya kufanya kazi kwa muda wa mwezi mmoja tu nikawambia wenzangu kwamba kama ningekuwa natoa ‘marks’ kwenye maeneo mawili kwenye uhifadhi na utalii, kwenye uhifadhi ningetoa marks mia kwa mia lakini kwenye utalii ningetoa moja ya mia kwani kwa vivutio vya utalii tulivyonavyo Tanzania tumeshindwa kuvitangaza, tungevitangaza vizuri mapato yetu yangekuwa sio ya hapa,”amesisitiza Dkt.Ndumbaro.

Dkt.Ndumbaro amesema nchi ya Tanzania katika suala la vivutio vya utalii ipo vizuri ila kwenye suala la ”marketing” ya vivutio vya utalii haipo vizuri.

“Tunaona kwenye suala la kujitangaza ndio kuna ugonjwa ndio maana Mimi na Wenzangu tunajitahidi kupigania kuleta mikutano mikubwa ifanyike nchini pamoja na kuanzisha mazao mengine ya utalii kama njia kutangaza vivutio vya utalii tulivyonavyo,” amesisitiza Dkt.Ndumbaro.

Dkt.Ndumbaro amesema uamuzi wa kufanya mkutano huo wa masoko na utalii ni moja ya mikakati maalum ambayo kama Wizara ni kuhakikisha jitihada alizozianzisha Rais Samia Suluhu Hassani za kuitangaza utaliii nchini kupitia kipindi chake maarufu cha “Royal Tour” hazipoi na kusisitiza kuwa kampeni hiyo inazidi kuwa ya moto kila kukicha.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news