TFS wakabidhi msaada wa madawati 120 Shule ya Msingi Kipera wilayani Mvomero

NA MWANDISHI MAALUM

KATIKA kuunga mkono juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika kuboresha sekta ya elimu nchini, Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania ( TFS) umekabidhi msaada wa madawati 120 yenye thamani ya Shilingi Milioni 12.6 kwa Shule ya Msingi Kipera iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.
Kamishna wa Uhifdhi TFS, Profesa Dos Santos Silayo akizungumza wajibu wao katika kulinda,kutunza na kuhifadhi misitu na rasilimali zake alipokuwa akikabidhi madawati 120 kwa shule ya Msingi Kipera .

Mbali na madawati hayo TFS imeahidi kutoa tena msaada wa madawati mengine 70 katika shule hiyo yenye wanafunzi 1110 ili kumalizia kabisa idadi ya madawati yanayohitajika,hivyo kumaliza kabisa changamoto ya uhaba uliokuwepo kwa muda mrefu.

Akizungumza leo Oktoba 18,2021 wakati wa kukabidhi madawati hayo mbele ya viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero, walimu, wazazi, wananchi pamoja na wanafunzi Kamishna wa Uhifadhi TFS Profesa Dos Santos Silayo amesema Wakala huo unaowajibu wa kushiriki kikamilifu kuunga mkono juhudi za Rais Samia Suluhu Hassan katika kutatua changamoto ndani ya jamii.

“Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) pamoja na shughuli zetu za usimamizi wa misitu na rasilimali zitokanazo na misitu ,tumekuwa tukishiriki katika kusaidia jamii katika nyanja mbalimbali, hiki ambacho tumekifanya kwa Shule ya Msingi Kipera tumekuwa tukikifanya na katika maeneo mengine.

“Leo tumekabidhi madawati 120 lakini katika taarifa ya Mwalimu Mkuu wa Shule amesema wakipata madawati mengine 70 watakuwa wamemaliza changamoto ya uhaba wa madawati.Hivyo niwaahidi tutaleta madawati hayo ili wanafunzi wetu wasome katika mazingira mazuri.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro Maajabu Nkanyemka ambaye pia ni Ofisa Elimu Msingi wa wilaya hiyo akisisitiza jambo kuhusu umuhimu wa madawati hayo kutunzwa.

“Pia tutamalizia ujenzi wa madarasa mawili ambao ujenzi wake tumeambiwa haujakamilika, tunafanya haya kwa ajili ya kumuunga mkono Rais Samia ambaye amedhamiria kuboresha sekta ya elimu nchini ,”amesema Profesa Silayo huku akiwapongeza walimu, wazazi na wanafunzi kutokana na mafanikio ambayo shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 1976 imeyapata ikiwemo ufauli mzuri wa wanafunzi ambao wamekuwa wakiupata mwaka hadi mwaka.

Akifafanua zaidi mbele ya wananchi wa Kijiji hicho kwamba Wakala huo ni wa Serikali na umepewa jukumu la kusimamia rasilimali za misitu na nyuki,hivyo ni wajibu wao kuhakikisha nyuki wanakuwepo.”Tunasimamia pia misitu, na hata mkiona miti ni kazi yetu, tunasimamia misitu nchi mzima.

“Tunapata mvua kwasababu ya uwepo wa misitu, wanyama wanaishi msituni. Ukiwa na miti unapata mazao ya aina mbalimbali na yote hayo yanatokana na kutunza na kuhifadhi misitu.Matunda mazuri yayofanywa na TFS tumeona wanafunzi wa kipera nao wanayafaidi.”
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Msingi Kipera mkoani Morogoro wakiwa wamekaa katika madawati mapya ambayo yametolewa na TFS kwa ajili ya shule hiyo Sehemu ya madawati yaliyokabidhiwa na TFS kwa Shule ya Msingi Kipera iliyoko Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro.Madawati hayo yamekabidhiwa na Kamishna wa Uhifadhi TFS Profesa Dos Santos Silayo ( hayuko pichani).

Profesa Silayo amesisitiza Rais Samia anafanya kazi kubwa na nzuri ya kuwatumikia Watanzania, hivyo wao wameamua kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kukabidhi madawati hayo na kumalizia yaliyobakia pamoja kuboresha miundombinu ya madarasa mawili.

“Tutashirikiana kuboresha mazingira mazuri ya shule ya msingi Kipela, Waziri wa Maliasili na Utalii pamoja na Naibu Waziri walipanga kuwepo lakini katika tukio hili lakini kutokana na kuwa na majukumu mengine nimewawakilisha,hata hivyo wamenituma nije niwaambie tuendelee kutunza rasilimali za misitu ,miti ,ikolojia na nyuki,”amesisitiza na kuongeza Rais Samia amesema kazi iendelee hivyo TFS wataendelea kuwatumikia wananchi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro ambaye ndio Ofisa Elimu Msingi katika wilaya hiyo Maajabu Nkanyemka ameshukuru kupatikana kwa madawati hayo ,amewaomba walimu,wanafunzi na wazazi kushirikiana kuyatunza.

“Tunahidi madawati haya tutayatunza, tutayatumia vizuri kama ilivyokusudiwa, tunaka kuona yanatumika kwa wanafunzi waliopo na wanaokuja.Kwa kuwa TFS lwameahidi madawati mengine 70 basi suala la matengenezo ya madawati watakayoharibika tutafanya halmashauri ya Mvomero.

“Yanayofanywa na Rais Samia katika elimu ,ni wajibu wetu sisi halmashauri kuunga mkono juhudi zake kwa vitendo, na hiki ambacho kimefanywa na TFS ni sehemu ya kuonesha kuunga mkono kazi inayofanywa na Rais,”amesisitiza.

Awali akizungumza kwa niaba ya walimu,Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Kipera William Rufili amesema wanashukuru changamoto ya uhaba wa madawati kupata ufumbuzi wake pamoja na majengo mawili ya madarasa, lakini pia ametoa ombi kwa wadau wengine kujitokeza kusaidia kwani wanayo changamoto ya uhaba wa matundu ya vyoo.

“Jumuiya ya Kipera na kata ya Mlali wamefurahia ugeni wa TFS kutokana na lengo ambalo limetukutanisha , shule yetu imepitia hatua mbalimbali za maendeleo , na kwa sasa inajumla ya wanafunzi 1,110 na walimu 24 .Taarifa ya miundombinu, jumla ya vyumba vya madarasa vinavyohitajika ni 25 lakini kwa sasa vipo 11 na viwili havijapakamilika

“Jitihada za wananchi wamefikia hapo hivyo bado tunahitaji msaada wa wananchi na Serikali katika madawati , tunao upungufu wa madawati 190 baada ya kukabidhiwa leo madawati 120 yamebakia madawati 70,hivyo tunawaomva TFS mtusaidie,”amesema.

Mwanafunzi Moshi Salum anayesoma darasa la sita katika shule hiyo ametoa pongezi kwa TFS kwa msaada huo wa madawati lakini akatoa ombi iwapo itawezekana kwa TFS iwasaidie katika kuwajengea ofisi za walimu,viti pamoja na meza.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news