Waziri Mchengerwa akemea fitina na majungu yanayowanyima fursa wengine

Na James K. Mwanamyoto-Maswa

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa amewataka baadhi ya watendaji katika taasisi za umma kutoendekeza fitina na majungu zinazowanyima fursa za uteuzi watumishi waadilifu na wachapakazi.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akizungumza na Watendaji na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa alipowasili wilayani humo kwa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Mhe. Mchengerwa ametoa wito huo Oktoba 9, 2021 wilayani Maswa alipokuwa akizungumza na Watendaji na Viongozi wa Wilaya hiyo, wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Mhe. Mchengerwa amesema, ili kumuenzi Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere tukiwa tunaelekea miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu, Watendaji na Viongozi hawana budi kusimamia misingi ya haki ambayo Mwalimu Nyerere alituachia ili kujenga taifa letu.

Mhe. Mchengerwa amesema, kuna Watumishi wengi ambao ni waadilifu, wachapakazi wazuri na wanastahili kupewa nafasi za uteuzi lakini kwa kuwa baadhi ya Watendaji wanasikiliza majungu na fitina wanawaacha na kupewapendekeza wengine ambao hawana sifa stahiki.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa akisisitiza jambo kwa Watendaji na Viongozi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa alipokuwa akizungumza nao wakati wa ziara yake ya kikazi ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

“Tutumie vizuri nafasi za uongozi tulizopewa kwa kutenda haki badala ya kuendekeza fitina na majungu na kuwakosesha haki watumishi wanaostahili na hatimaye kuwakatisha tamaa ya kutekeleza kikamilifu majukumu yao,” Mhe. Mchengerwa amesisitiza.

Ili kupata watumishi wenye sifa, amewataka Watendaji hao kujiridhisha na vigezo vya utendaji kazi wa watumishi ambao majina yao wanayawasilisha Ofisi ya Rais-UTUMISHI kwa ajili ya taratibu za uteuzi.

“Tutende haki, tusiwasilishe majina ya nafasi za uteuzi kwa kigezo cha kufahamiana bali tujiridhishe na utendaji kazi wa watumishi ambao majina yao yanawasilishwa kwani kuna watumishi wengine hawana watu wanaowafahamu wa kuwasaidia na ni wachapakazi wazuri sana, hivyo tusiwakatishe tamaa,” Mhe. Mchengerwa amefafanua.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi Prisca Kayombo akitoa neno la shukrani kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa mara baada ya Mhe. Mchengerwa kuzungumza nao wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma Wilayani Maswa na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Kwa upande wake, Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Bibi Prisca Kayombo amekiri kupokea maelekezo ya Mhe. Waziri na kuahidi kusimamia vema utekelezaji wa maelekezo hayo.

“Mhe. Waziri, tumeyapokea maelekezo yako, mimi nikiwa ndiye Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, nimeguswa sana na maelekezo yako, hivyo nitahakikisha naweka usimamizi mzuri kwa Watumishi wa Umma wa Mkoa huu ikiwa ni pamoja na kutenda haki kwa Watumishi wote,” Bibi. Kayombo amesisitiza.
Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Aswege Kaminyoge akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Wilaya yake kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mhe. Mohamed Mchengerwa wakati wa ziara ya kikazi ya Mhe. Mchengerwa ya kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma Wilayani Maswa na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Mhe. Mchengerwa amehitimisha ziara yake ya kikazi ya siku mbili Mkoani Simiyu iliyolenga kuhimiza uwajibikaji kwa Watumishi wa Umma na kukagua utekelezaji wa miradi ya TASAF.

Post a Comment

0 Comments