Benin yazima matumaini ya Taifa Stars kufuzu Kombe la Dunia 2022

NA GODFREY NNKO

NYOTA wa timu ya Taifa ya Benin, Jodel Dossou na Steve Mounie wamezima matumaini ya Tanzania kupitia Taifa Stars kufuzu Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar.

Dossou wa Benin ndani ya kipindi cha kwanza kwa maana ya dakika ya 44 ndiye aliyeanza kuzima ndoto hiyo baada ya kupachika bao safi katika nyavu za Madagascar.

Naye Mounie alimaliza mahesabu kwa kuachia bao lingine ndani ya dakika ya 79, hivyo kuifanya Benin kujikusanyia alama zote tatu huku Madagascar wakirudi nyumbani na matokeo sawa na yale waliyopata Taifa Stars ingawa wao DR Congo wamewachapa mabao matatu kwa sufuri katika mtanange huo wa Novemba 11, 2021.

Katika mtanange huo uliopigwa katika dimba la Stade de I'Amitie nchini Benin umeiwezesha Benin kuongoza Kundi J kwa alama 10 huku nafasi ya pili ikichukuliwa na DR Congo kwa alama 8, nafasi ya tatu Tanzania kwa alama 7 na Madagascar wanaburuza mkia kwa alama 3.


Pengine Taifa Stars iliyokuwa inaongoza msimamo wa Kundi J kabla ya mchezo huo,inaweza kujilaumu baada ya kuutumia uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke vibaya, kutokana na kuruhusu mabao matatu katika dakika ya 6, 66 na 85 huku wao wakiongoza umiliki wa kandanda safi.

Mabao ya DR Congo yaliwekwa nyavuni na Gael Kakuta, Nathan Idumba Fasika na Ben Malango.

Kwa matokeo hayo, Taifa Stars itacheza mchezo wa mwisho dhidi ya Madagascar mjini Antananarivo, Novemba 14,2021 huku DR Congo ikicheza nyumbani dhidi ya Benin siku hiyo hiyo, hivyo Taifa Stars imeshindwa kufuzu baada ya matokeo hayo, kwani kwa sasa ni timu moja ndiyo itasonga mbele.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news