DC Twange, DED Mbogo waingia mstari wa mbele kufanya usafi wa mazingira

NA MARY MARGEWE

MKUU wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Lazaro Twange ameamua kuingia mstari wa mbele kuwaongoza watumishi wenzake na wananchi katika zoezi maalumu la kuyafanyia mazingira usafi pamoja na kupanda miti.
Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Lazaro Twange (aliyevaa shati jeupe) akishirikiana na watumishi pamoja na wananchi wa Kijiji cha Dareda Kati, Kata ya Ayalagaya wilayani humo kufanya usafi wa mazingira.

DC Twange akiwa bega kwa bega na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Anna Mbogo wameanzisha utaratibu huo ambao umepongezwa na watu wengi, ukiwa na lengo la kuifanya halmashauri ya wilaya hiyo kuwa na mandhari nzuri ambayo pia ni tiba kubwa kwa afya ya binadamu katika maisha ya kila siku.
Mkuu wa Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Lazaro Twange akinyeshea maji mti alioupanda katika Kijiji cha Dareda Kati, Kata ya Ayalagaya wilayani humo mara baada kumaliza kufanya usafi wa mazingira.

Kwa nyakati tofati wanakijiji cha Dareda wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, utaratibu huo unafaa kuigwa na viongozi wengine kwani, hatua ya kufanya usafi na kupanda miti kwa wingi italiwezesha Taifa letu kukabiliana na athari zinazotokana na mabadiliko ya tabia nchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati mkoani Manyara, Anna Mbogo akipanda mti mara baada ya kumaliza zoezi la kufanya usafi wa mazingira katika Kijiji cha Dareda Kati, Kata ya Ayalagaya huku akiwa pamoja na watumishi wa halmashauri hiyo na wananchi wa eneo husika ikiwa ni katika maandalizi ya kuelekea kwenye maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Tanzania Bara.

Kwa nini usafi?  

Shirika la Afya Duniani ( WHO) linasema kuwa,mazingira machafu ni moja wapo ya sababu kuu ya kuenea kwa maradhi hapa nchini na duniani kote.

Kwa msingi huo, hatua ya kila mmoja kujitokeza kufanya usafi na kuweka juhudi mbalimbali za kuyaboresha zitaleta matokeo makubwa kwa ustawi bora wa afya zetu, uchumi na mazingira bora kwa ajili ya maendeleo endelevu.
Baadhi ya tafiti zinazohusiana na mazingira zilizoonwa na DIRAMAKINI BLOG zinasisitiza kuwa, kuingia mstari wa mbele kuyaboresha mazingira kuna manufaa makubwa katika nyanja mbalimbali.

Ndiyo maana katika mahojiano na blogu hii mmoja wa wananchi mjini hapa aliyejitambulisha kwa jina la Petro anasema kuwa, kufanya usafi iwe tabia endelevu kwa kila mwana kaya, kwani faida zake ni kubwa kuliko hasara.

"Hakuna hasara yoyote katika kufanya usafi, ni faida tupu, angalia kwa sasa watu wanateseka kutokana na ukame, hali hii imechangiwa na tabia zetu wenyewe binadamu, tungefanikiwa kuyapa kipaumbele mazingira yetu kwa kufanya usafi ambao unajumuisha upandaji miti, leo hii tungekuwa tunakimbilia makoti, hatutamani hata kuona mvua zikiendelea, lakini ni kinyume chake, sasa tunatamani hata kutembea bila kuvaa nguo barabarani, joto ni kali, jua linagonga utosi kweli kweli .
"Hivyo niseme wazi kuwa, huu si wakati wa kuchekeleana kuhusu uchafuzi wa mazingira, kwani usafi wa mazingira ni muhimu sana ili kuhakikisha kuwa afya inazingatiwa na kuzuia uwezekano wa binadamu kukabiliana na athari za taka,"anaongeza Petro.
Kwa mujibu wa tafiti, miongoni mwa taka zinazoweza kusababisha matatizo ya afya ni kinyesi cha binadamu na wanyama, taka ngumu, majitaka na nyingine nyingi ambazo zinapatikana katika mazingira yetu ya kila siku. 

Ndiyo maana, athari zake zimekuwa nyingi ambapo baadhi ya magonjwa ambayo yamekuwa yakiikumba nchi yetu na kusababisha vifo ni kipindupindu.

Kipindupindu ni ugonjwa ambao huibuka mara kwa mara na chanzo chake kikubwa ni kutozingatia usafi wa mazingira.
Hivyo, tabia ya kutozingatia usafi wa mazingira imekuwa ikisababisha baadhi ya watu kutiririsha maji ya vyooni mitaani hata kuibua harufu kali ambayo ni hatari kwa afya za watu.

Katika nchi yetu kwenye baadhi ya miji watu hutiririsha maji hasa wakati wa mvua, ili kukwepa kukodi magari ya kunyonya maji hayo, jambo ambalo ni hatari zaidi ya gharama ambazo mtu mmoja anakwepa kuwajibika kuzilipa.

Aidha, baadhi ya watu wamekuwa wakijenga vyoo kandokando ya mfereji kisha hutiririsha majitaka wakati wa mvua, tabia ambayo nayo ni hatari zaidi.

DIRAMAKINI BLOG inaamini kuwa, usafi wa mazingira yetu unaanzia katika kaya zetu hadi huko juu, ukishindwa kutimiza wajibu wako katika kuyapa mazingira yako kipaumbele katika usafi, tarajia kuvuna matokeo mabaya kiafya na kuyumba kiuchumi. Fedha au mali unazotafuta kwa bidii pasipo kuzingatia usafi, utakuja kuzitumia kwa muda mfupi utakapokumbana na changamoto za kiafya zinazochangiwa na uchafu wa mazingira.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news