Maagizo ya Waziri Mchengerwa kwa TAKUKURU yagusa kila eneo

NA DOREEN ALOYCE

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa amewataka viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU) kuongeza jitihada katika kutoa elimu kwa wananchi ili waweze kujua haki zao na waweze kuepukana na vitendo vya kutoa na kupokea rushwa.
Baadhi ya viongozi kutoka mikoa 28 ya TAKUKURU wakifuatilia hotuba ya Waziri Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) leo Novemba 25, 2021 jijini Dodoma. (Picha na Doreen Aloyce/DIRAMAKINI BLOG).

Aidha, amewaagiza viongozi hao kufuatilia vyema utekelezaji wa miradi yote ya kimaendeleo inayoendelea hapa nchini na wahakikishe kuwa kusiwepo na mianya ya rushwa.

Ameyasema hayo leo Novemba 25, 2021 jijini Dodoma wakati akifungua mkutano mkuu wa mwaka wa viongozi 60 kutoka katika mikoa 28 ya taasisi hiyo, wenye lengo la kujadili utendaji kazi pamoja na changamoto katika kazi zao.

“Utekelezaji wa miradi ya kiimaendeleo umeghubikwa na udanganyifu, ninyi kama TAKUKURU kiongozi wa kila wilaya apimwe namna anavyoweza kusimamia matumizi ya fedha katika kila wilaya na niseme tu kwamba hili ni jukumu letu sote katika kusimamia kusimamia.

“Mheshimiwa Rais wetu Samia Suluhu Hassan alivyofungua hizi fursa za uchumi hakumaanisha watu watumie fedha hizo vibaya na kutumia nyaraka za uongo kuhusu gharama zinazotumika katika miradi hiyo, tumieni mkutano huu kujadili malengo na muhakikishe kusiwepo na mianya ya uchepushaji wa fedha hizo kwa ajili ya matumizi binafsi katika kila mradi,”amesema Mchengerwa.

Aidha, amesema taasisi hiyo isionekane na kasoro ya rushwa na badala yake iwe mstari wa mbele kufanya kazi usiku na mchana ili kuokoa rasilimali za taifa.

HISTORIA

“Jukumu langu kubwa kwa siku ya leo ni kufungua mkutano huu. Lakini, ninaomba mniruhusu kabla ya kutekeleza jukumu hilo nirejee kwa kifupi historia ya mapambano dhidi ya rushwa nchini na kuanzishwa kwa taasisi hii muhimu ili kwa pamoja tujue kwa nini taasisi hii ina sura iliyonayo leo.

"Kipekee kabisa ninawaomba pia ndugu zangu wa habari mtusaidie katika jambo hili; jengeni kiu ya kuifahamu vizuri TAKUKURU ili kupitia ufahamu huo muwe mabalozi wazuri wa kuitangaza pamoja na kuchapisha habari zinazojitosheleza kuhusu historia ya mapambano dhidi ya rushwa hapa nchini.

"Ndugu viongozi na wageni waalikwa, suala la Rushwa ni suala la kihistoria na mapambano dhidi ya Rushwa hapa nchini yalianza hata kabla ya Uhuru ambapo mwaka 1930 utawala wa Kiingereza ulitumia Kanuni ya Adhabu ya India “The Indian Penal Code” kuwaadhibu watumishi wa Serikali ya kikoloni waliopatikana na hatia ya kupokea hongo.

"Mnamo mwaka 1945 Sheria ya kwanza ya “The First Penal Code of Tanganyika” Sura ya 16 ilianza kutumika kudhibiti vitendo vya hongo na matumizi ya nyaraka zenye taarifa za uongo kwa lengo la kumdanganya mwajiri.

"Mwaka 1958 Sheria ya Kuzuia Rushwa “The Prevention of Corruption Ordinance Cap.400” ilianzishwa. Wakati Tanganyika (Tanzania Bara) ikipata Uhuru mwaka 1961, ilirithi utumishi wa umma ambao ulikuwa umeghubikwa na watendaji wasio waaminifu, adilifu na wenye vitendo vya rushwa waliokuwa wakihudumu katika Serikali ya kikoloni.

"Katika kipindi hicho, nchi yetu ilikuwa inakabiliwa na upungufu wa watumishi wazawa wenye sifa na taaluma mbalimbali za kuwawezesha kutekeleza majukumu ya taasisi mpya zilizoanzishwa.

"Pia hawakuwepo watumishi wazawa wa kujaza nafasi zilizoachwa wazi na maafisa wa kikoloni ambao walilazimika kuacha kazi baada ya uhuru. Changomoto nyingine ni kuwepo kwa mifumo ya utawala na mitizamo ya watumishi ya kikoloni isiyozingatia miiko na maadili ya utumishi wa umma iliyohujumu huduma za kijamii kama vile afya, makazi bora, barabara na elimu.

"Vitendo hivyo vilisababisha kuwepo kwa changamoto kubwa tatu ambazo ni ujinga, umaskini na maradhi miongoni mwa wananchi, tangu nchi yetu ipate uhuru, historia inabainisha uwepo wa vipindi mbalimbali ambavyo vimekuwa na uhitaji tofauti wa namna ya kukabiliana na tatizo la rushwa, sambamba na utatuzi wa changamoto za usimamizi wa Utumishi wa umma ikiwa ni pamoja na: kutekeleza Sera ya Wazawa mwaka 1961, kuandaa mipango ya rasilimaliwatu mwaka 1963, kuanzisha Jeshi la Kujenga Taifa mwaka 1963.

"Muungano wa Tanganyika na Zanzibar mwaka 1964, kuanzisha mfumo wa chama kimoja cha siasa mwaka 1965 yote hiyo ililenga kuimarisha na kujenga utumishi wa umma ambao utaondokana na mitazamo ya mifumo ya kikoloni iliyokuwa imeghubikwa na vitendo vya rushwa na uhujumu uchumi wa nchi na kuleta tija katika uendeshaji wa Serikali, kuimarisha usimamizi wa watumishi Serikalini, na kuimarisha utoaji huduma za kijamii na kiuchumi licha ya kuwa mafanikio yaliyopatikana hayakukidhi matarajio kwa wakati wote.

"Katika kuliona hilo, Rais wa Awamu ya Kwanza, Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alipokuwa analihutubia Bunge jipya Oktoba 12, 1965, alisema, “Rushwa ni Adui mkubwa wa Haki. Tusipoidhibiti, itaangamiza Taifa letu”.

"Mnamo mwaka 1970 Sheria ya Kuzuia Rushwa (Cap.400) ilirekebishwa na kuongeza kifungu kinachotamka kuwa ni kosa kwa mtumishi wa umma kumiliki mali idhaniwayo imepatikana kwa njia ya rushwa.

"Mwaka 1971 Sheria hiyo ilifanyiwa marekebisho na kubadilishwa kuwa Sheria ya Kuzuia Rushwa Na.16 ya mwaka 1971 ambayo ilikuwa na makosa ya Rushwa manne (4) ili kukabili tatizo la rushwa nchini.
Baadhi ya viongozi kutoka mikoa 28 ya TAKUKURU wakifuatilia hotuba ya Waziri Mohamed Mchengerwa (hayupo pichani) leo Novemba 25, 2021 jijini Dodoma. (Picha na Doreen Aloyce/DIRAMAKINI BLOG).

"Miaka mitatu baada ya kutungwa kwa sheria hii mwezi Januari, 1975 Serikali ilianzisha Kikosi cha Kuzuia Rushwa kwa lengo la kuongeza mapambano dhidi ya rushwa nchini.

"Kikosi kilikuwa chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani, kilikuwa na kazi kuu tatu ambazo ni kuzuia rushwa, kupeleleza na kuendesha mashtaka dhidi ya watuhumiwa wa makosa ya rushwa nchini. Mkurugenzi Mkuu wa kwanza wa Kikosi hiki alikuwa ndugu Geofrey Sawaya. Mabadiliko ya viongozi wakuu wa kikosi hiki yaliendelea kwa miaka kadhaa ambapo viongozi watatu wa kwanza walikuwa wanatoka katika Jeshi la Polisi,"alifafanua Waziri Mchengerwa na kuongeza kuwa;

"Waziri Mkuu Hayati Edward Moringe Sokoine alianzisha msako wa wahujumu uchumi mjini Dodoma, Machi 25, 1983 ambao ulipelekea kuanziashwa kwa Sheria ya Uhujumu Uchumi Na. 13 ya mwaka 1984 ambayo ilishughulikia makosa ya uhujumi Uchumi,"amesema.

MABORESHO SHERIA

Waziri Mohamed Mchengerwa ameendelea kufafanua kuwa, mwaka 1991, Sheria ya Kuzuia Rushwa Na.16/1971 iliboreshwa ili iendane na wakati na katika maboresho hayo Kikosi kilibadilishwa jina na kuwa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (TAKURU) wengi waliizoea kama PCB, yaani ‘Prevention of Corruption Bureau’ na hapo taasisi ilihamishwa kutoka katika Jeshi la Polisi na kuwekwa chini ya Ofisi ya Rais.

Amesema, ilipofika mwaka 2007 jina lilibadilika na kuwa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) au ‘Prevention and Combating of Corruption Bureau’ (PCCB).

Pia Waziri amesema, ilitungwa Sheria ya Kuzuia na Kupambnana na Rushwa Na. 11 ya Mwaka 2007 ambayo iliongezewa makosa na kufikia 24.


"Misingi ya waasisi, maono na fikra zao yaligusa mioyo ya wananchi wa kawaida katika kupigania vita dhidi ya maadui wa haki, maadui wa haki ambao wamegawanyika katika sehemu kuu tatu, Ujinga, Maradhi na Umasikini, isingeliwezekana kama Taifa hili kushinda vita dhidi ya Amani, kushinda vita dhidi ya Ukombozi, kushinda vita dhidi ya maendeleo bila ya mapambano dhidi ya rushwa kuwa halisi katika nyakati zao.

"Tegemeo la wananchi ni viongozi waliowachagua na viongozi walioteuliwa, viongozi wa karne ya leo hatutegemei kufikiri katika maisha yao na wengi wao wametekwa na hofu ya rushwa na ubadhirifu mioyoni mwao.

"Wengi wao wamekuwa wazembe wakifikiria maisha bila watanzania waliochagua, kati yao viongozi wengi wa majiji makubwa wametekwa mifukoni mwa matajiri wadhulumaji na watoa rushwa, waonevu, wanyonyaji wasiolitakia mema Taifa lao.

"Wameingia kwenye Payrow ya matajiri wala rushwa wanyonyaji wa haki za wanyonge kwa fedha zao. Kamwe msikubali kuruhusu kudidimia kwa matumaini ya mioyo ya Watanzania kwa Taifa lao. Uzembe na ubadhirifu utaliangamiza Taifa letu, tutumie maneno ya waasisi na viongozi waliotangulia wa Taifa hili kama nyenzo ya kutuwezesha katika mapambano dhidi ya uzembe, dhuluma na ubadhirifu wa mali za umma.

"Ingelikuwa ni nyakati za mwalimu, nyakati za Joto ya Vita dhidi ya Amini, nyakati za kulitambulisha Taifa la Ujamaa na Kujitegemea, Nyakati ya Azimio la Arusha na Madaraka Mikoani. Ningeliwakumbusha maono ya Hayatti Edward Moringe Sokoine aliyewahi kuwa Waziri Mkuu wa Nchi hii aliyeamini na kuonya kuwa “Ole wake kiongozi mzembe na asiye na nidhamu nitakayemkuta, hana Usalama wa kazi. Kiongozi mzembe na mbadhirifu (mla rushwa) wahesabu siku zao labda tusiwajue, hawa hatutawalinda kwa vitendo vyao viovu, Alisema hayo tarehe 26-31983,"amebainisha Waziri Mchengerwa.

KWA NINI WAZIRI AMEREJEA HISTORIA?

"Ndugu viongozi na wageni waalikwa, kwa nini nimerejea kwa kifupi historia hii? Mosi ni kuonesha ni kwa namna gani Serikali ilivyodhamiria kwa vitendo kusimamia mapambano dhidi ya Rushwa, kuanzia Serikali ya Awamu ya Kwanza, Pili, Tatu, Nne, Tano na sasa ya Sita.

"Pili ni kuonesha kuwa siyo jambo geni kwa taasisi hii kuongozwa na Mkuu ambaye anatokea Jeshi la Polisi. Mtakubaliana nami ndugu viongozi na washiriki kuwa hata katika Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007 iliyoifuta Sheria ya Kuzuia Rushwa Na.16/1971, baadhi ya mamlaka ya Afisa Uchunguzi wa TAKUKURU yanatokana na Sheria zinazotumiwa na Jeshi la Polisi na ndiyo maana anayomamlaka ya kumkamata mtuhumiwa na hata kumuweka mahabusu.

"Hivyo, ninaomba nitumie fursa hii kukupongeza Kamishna wa Polisi Salum Rashid Hamduni, na Bibi Neema Mwakalyelye kwa kuteuliwa na kuapishwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kuiongoza TAKUKURU.

"Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaimani kubwa sana na utendaji wenu uliotukuka, tokea ukiwa Jeshi la Polisi. Na ni imani yake pasipo shaka kuwa utaisaidia nchi yetu katika mapambano dhidi ya rushwa.

"Hivyo, ni rai yangu kuwa kwa sasa unapaswa kuhakikisha unaudhihirishia ulimwengu na watanzania wote kuwa ulistahili majukumu haya kwa kufanya kazi kwa weledi na uaminifu mkubwa pasipo kumuonea wala kumpendelea mtu yeyote, kuboresha taswira na kuimarisha mifumo ya utendaji kazi za taasisi huku ukilinda maslahi ya Taifa letu,"amebainisha Waziri Mchengerwa.

IMANI YA RAIS

Waziri Mchengerwa amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan anaamini kuwa kwa umoja wao na kwa ushirikiano na viongozi pamoja na watumishi wengine wa TAKUKURU utaisaidia Serikali anayoiongoza kuijenga Tanzania ambayo wananchi wake watanufaika na rasilimali za umma na kupata huduma bora pasipo kuombwa au kutoa rushwa.

“Ndugu viongozi na wageni waalikwa, kuundwa kwa taasisi hii ni tukio la Azma ya kujenga nguzo kuu za serikali za kuinua na kukweza ufanisi wa uwajibikaji uwe na watumishi wa umma wenye miiko ya maadili kwa ustawi na maendeleo ya jamii na Taifa. Kitaifa taasisi hii ni nanga ya Taifa letu kwa usalama wa tija ya kutoa wajibu wa uwazi na ukweli wa kuchangia utawala bora; hususani katika kuchuja na kuondoa kasoro zioteshazo maovu yanayoambatana na yaliyofichika katika kurasa za mikataba hasi.

“Sasa ninaomba nirejee katika muktadha wa mkutano huu. Ndugu Mkurugenzi Mkuu, nimesikia maelezo yako kuhusu utendaji kazi wa Taasisi katika mwaka wa fedha wa Julai 2020 hadi Juni 2021. Pasipo kurudia kile ulichokisema, ninaomba kuchukua fursa hii kuwapongeza sana kwa mafanikio makubwa ya kiutendaji mliyoyapata katika kipindi hicho. Hongereni sana.

“Mtakubaliana nami kuwa TAKUKURU inapofanya vizuri, Serikali na nchi zinakuwa zimefanya vizuri katika mapambano dhidi ya rushwa. Ndiyo maana tunasema nyinyi mmepewa dhamana ya kuongoza mapambano haya; mkizembea tunaanguka wote na mkiwa imara na kutimiza wajibu wenu ipasavyo, tunainuka wote.

“Kwa umuhimu wa pekee watumishi wote tambueni kwamba, Taasisi yenu ni kioo cha jamii na nyinyi ni walinzi safi wa haki za jamii na haki za Taifa. Kwa kuwa watumishi wote wa nafasi zote nyinyi ni wakingaji waaminifu wa haki kwa jamii na haki kwa Taifa, kwa hiyo sasa mnapaswa kuwa na matendo yenye usafi wa moyo na muwe na nafasi zenye taratibu za kuitwa ni za watu wenye sifa ya watenda haki. Kumbukeni, watu na haki zao maana yake ni pete na kidole visivyoachana,”amefafanua Waziri Mchengerwa.

Pia Waziri Mchengerwa amebainisha kuwa, kutokana na uimara wao, Tanzania kwa takribani miaka mitatu mfululizo imefanya vizuri, kwa vipimo vya kimataifa, katika mapambano dhidi ya rushwa.

Hivyo, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais, Samia Suluhu Hassan itaendelea kuijengea TAKUKURU uwezo wa kifedha, kisheria na kwa kuipatia rasilimali watu na vitendea kazi vya kutosha ili mtekeleze majukumu yenu kwa ufanisi zaidi kwa kadri bajeti itakavyoruhusu.

“Kwani tatizo la rushwa miongozi mwa watumishi wa serikali haliwezi kuondolewa bila ya kuwa na miongozo imara inayosimamia utendaji wa kazi ipasavyo. Wasimamizi wawe wenye uwezo; waadilifu, wabunifu na wenye mienendo na tabia nzuri.

“Ndugu Viongozi na wageni waalikwa, moja kati ya jambo muhimu sana katika mapambano dhidi ya rushwa ni kuwa na sheria imara. Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, tangu iingie madarakani Machi mwaka huu 2021, imechukua hatua za makusudi kuiboresha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Na.11/2007.

“Mhe. Rais Samia aliagiza mchakato wa maboresho hayo uanze mara moja, na kama alivyogusia Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, na ni faraja kwetu kuwa Taasisi zote zinazohusika zimeshiriki kuandaa mapendekezo hayo. Serikali itaufikisha muswada wa maboresho ya Sheria hiyo Bungeni,”amesema Waziri.

TAKUKURU HAILINGANISHWI

Mheshimiwa Waziri Mchengerwa amefafanua kuwa, taasisi hiyo isijilinganishe na taasisi yoyote ile kwani kila taasisi ina changamoto zake.

“Taasisi hii kujilinganisha na taasisi nyingine ni kutafuta matope ya taasisi nyingine muyapake kwenye taasisi yenu. Serikali imeiwezesha TAKUKURU kutekeleza Muundo Mpya wa Utendaji wa Taasisi hatua inayotarajiwa iongeze ufanisi wa chombo hiki muhimu.

“Pia, katika mwaka huu wa fedha wa Julai 2021 hadi Juni 2022, Serikali imetoa kibali cha ajira mpya 350 za watumishi wa TAKUKURU. Hatua hii ya Serikali imelenga kuijengea uwezo zaidi Taasisi hii ili imudu kutekeleza majukumu yake ya kisheria kwa ufanisi zaidi,”ameongeza.

Waziri amesema kuwa, taasisi hii mafanikio yake yatokane na kuheshimika uwajibikaji adilifu wa kila mtumishi. Ikumbukwe kwamba samaki mmoja akioza katika wilaya, Mikoa na Taifa wote wameoza

“Pamoja na mchango wa Serikali, ni dhahiri mafanikio yaliyopatikana mwaka jana yamechagizwa pia na wadau wengine wa ndani na nje ya Tanzania.

“Taasisi hii kuweni na mfumo karimu na jamii na ndiyo itapata mchango mkubwa wa viarifu vya kuchujia kwa yale yanahitaji mashirikiano ya Umma. Ushirikiano wa wadau katika kuzuia na kupambana na rushwa ni wa muhimu sana.

"Hatuwezi kufanikisha mapambano haya peke yetu; Lazima tushirikiane na wadau wengine, kwa mawazo, utaalamu hata misaada ya kifedha, ili tuweze kudhibiti vitendo vya Rushwa.

HESHIMA KWA WADAU

“Nitumie fursa hii, kwa niaba ya Serikali, kuwashukuru sana wadau wote walioshirikiana na wanaoendelea kushirikiana na TAKUKURU pamoja na Serikali kwa ujumla katika mapambano dhidi ya rushwa,”amesema.

Wadau hao, Waziri amesema ni pamoja na Jumuiya ya Madola kupitia programu ya kujenga mapambano endelevu dhidi ya rushwa nchini Tanzania (Building Sustainable Anti – Corruption Action in Tanzania, kwa kifupi BSAAT).

Wengine ni Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Taasisi isiyokuwa ya Serikali ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS) ya Ujerumani, Women Fund Tanzania Trust (WFT-T), Chama cha Skauti Tanzania (CST), Action Aid na Sikika.

“Ninawasihi ushirikiano na wadau hawa uendelee kuimarishwa kila mwaka kila kuitwapo leo ili kwa pamoja tuitokomeze rushwa hapa nchini,”amesisitiza Waziri Mchengerwa.

MWONGOZO

Waziri Mchengerwa amesema, hivi karibuni, ulizinduliwa Mwongozo wa Mafunzo kwa Wawezeshaji Kufundisha Vijana wa Skauti kuhusu mapambano dhidi ya Rushwa.

Mwongozo huo amesema, umeandaliwa kwa ushirikiano kati ya TAKUKURU na Chama cha Skauti Tanzania (CST) kwa ufadhili wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Konrad Adenauer Stiftung (KAS).

“Kipekee kabisa niwapongeze sana kwa maamuzi yenu ya kuwashirikisha vijana wa Skauti katika mapambano dhidi ya rushwa.

“Ninaomba nichukue fursa hii kuwataarifu kuwa Serikali inamatarajio makubwa sana katika mpango huu.

"Ni jambo lisilopingika kuwa kwa kuwashirikisha Skauti, Taifa litaongeza idadi ya wapambanaji dhidi ya adui rushwa kwa sababu vijana hawa ni wengi na watafahamu vizuri kuhusu madhara ya rushwa, manufaa ya kutokuwa na rushwa, nafasi na wajibu wa kuzuia na kupambana na rushwa na watashiriki ipasavyo kukabiliana na vitendo vya rushwa. Niwaombe, kupitia mkutano huu japokuwa ndiyo mnaanza utekelezaji muwe na tabia ya kufanya tathmini mara kwa mara ya namna mpango huu mnavyoutekeleza ili muweze kuboresha pale patakapobainika kuwa na mapungufu au changamoto.

KUHUSU TRILIONI 1.3

“Ndugu viongozi na wageni waalikwa, kama mnavyofahamu, Oktoba 10, 2021 Mheshimiwa Rais alizindua ‘Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19, hapa jijini Dodoma. Kampeni hii itakayogharimu Shilingi trilioni 1.3 itawezesha kutekeleza miradi ya maendeleo itakayoboresha huduma za jamii katika sekta ya afya, elimu, utalii na sekta ya maji. Halmashauri zote 185 za Tanzania Bara zitanufaika na fedha hizi ambazo kupitia miradi ya maendeleo itakayojengwa, wananchi watapata huduma bora za afya katika mazingira bora zaidi hatua itakayotuwezesha kukabiliana na magonjwa mbalimbali ikiwemo janga la UVIKO-19.

“Watoto wetu pia watasoma katika mazingira bora yatakayowaepusha na janga hili la UVIKO-19 na kuwawezesha kupata elimu bora kwa maendeleo yao na ya Taifa kwa ujumla.

“Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan, kufungua uchumi siyo fursa ya kuneemesha maslahi ya watu binafsi kupitia uundwaji wa mikataba katili ya kudhuru pato la Taifa lisiwe na Tija kwa maslahi ya Taifa.

Hii siyo kampeni ndogo, ni kampeni kubwa na inayohitaji ushiriki wa kila Mtanzania katika utekelezaji wake ili miradi itakayojengwa iakisi fedha zitakazotumika na iwe endelevu.

“Sote tunafahamu kuwa mara kadhaa utekelezaji wa miradi ya maendeleo umegubikwa na vitendo vya rushwa vikiwemo ubadhirifu, uchepuzi, matumizi mabaya ya madaraka au matumizi ya nyaraka za uongo kuhusu gharama zilizotumika katika manunuzi au ujenzi. Nawasihi rejeeni kauli ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan aliyoitoa Bungeni tarehe 22 Aprili, 2021 “Hatutawaonea aibu viongozi na watumishi wezi wa mali za umma, tutaendeleza juhudi za kupambana na rushwa katika utumishi wa umma…” pamoja na maelekezo yake ya tarehe 10 Oktoba, 2021 wakati alipokuwa akizindua mpango huu.

“Hivyo kwa muktadha ule ule nami Ninawaagiza TAKUKURU mfuatilie kwa karibu utekelezaji wa miradi yote kupitia kampeni hii ili tupate matarajio yaliyokusudiwa. Tumieni mkutano huu kujipanga kimkakati kufuatilia utekelezaji wa miradi kupitia fedha hizi ili thamani halisi ya fedha ikaonekane katika miradi husika,”amefafanua na kuagiza Waziri Mchengerwa.

Pia ameitaka taasisi hiyo kuongeza ujuzi, maarifa na weledi wa kutengua vitendawili vya chui waliovaa ngozi za kondoo, ambao wana dhuluma za kudhuru kupitia mifumo katili ya matendo ya udokozi wa dhana za mbinu za kuuma na kupulizia za panya.

“Pamoja na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo pamoja na kampeni hii, nguvu pia zielekezwe katika Kuzia Vitendo vya Rushwa Kubwa ambazo zinaathari kubwa sana katika uchumi wa Taifa letu, tufanye uchunguzi wa vitendo vya rushwa kubwa na wahusika wafikishe Mahakamani hususani katika Mahakama Maalum ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi.

“Lakini kuwafikisha mahakamani ni hatua moja, hatua ya pili ni kuhakikisha kuwa Jamhuri inaongeza uwezo wa kushinda kesi zinazofikishwa mahakamani.

“Ninafahamu kuwa siyo jukumu la TAKUKURU kutoa uamuzi wa kesi iliyoko mahakamini, bali ni jukumu la Mahakama ila ni wajibu wa TAKUKURU kuchunguza na kuwasilisha mahakamani ushahidi unaojitosheleza na usiokuwa na shaka wa kutendeka kwa makosa ya rushwa ili Mahakama iweze kuwatia hatiani watuhumiwa wa vitendo vya rushwa, hili ni jukumu lenu la msingi na mnapaswa kulitekeleza kwa kushirikiana na Ofisi ya taifa ya mashtaka kwa maslahi mapana ya Taifa letu ili haki ionekane inatendeka,”amesema Waziri Mchengerwa.


JITIHADA ZA TAKUKURU

Mheshimiwa Waziri amebainisha kuwa, TAKUKURU imefanya kazi kubwa kuelimisha umma kuhusu mapambano dhidi ya rushwa na kuzuia mianya ya rushwa.

“Nikirejea taarifa ya Mkurugenzi Mkuu katika majukumu haya, utendaji wenu uliongezeka. Pamoja na ongezeko hilo, wapo wananchi ambao hawajafikiwa.

“Endeleeni na jitihada za kuwafikia wananchi na hasa waliopo vijijini. Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele zaidi katika kuzuia vitendo vya rushwa ikiwemo kuwaelimisha wananchi ili wafahamu haki zao katika upatikanaji wa huduma, madhara ya rushwa na jinsi ya kutoa taarifa za rushwa.

“Taasisi hii itoe wajibu sahihi usiopoka haki za wasio na kasoro za kupata haki za Uhuru wa dhamana. Hakimu haki ndiye atajenga sifa nzuri za kuthaminika nyinyi ni taasisi ya utalawa Bora kwa Serikali ya awamu ya sita.

“Ni imani yetu kuwa wananchi wakiwa na ufahamu wa kutosha kuhusu Rushwa na madhara yake basi itawarahisishia kukabliana nayo kwakuwa hawatatoa wala hawata sita kutoa taarifa za vitendo vya rushwa.
“Aidha, elimu hiyo itawafunua zaidi macho wananchi, kutambua vitendo vya rushwa vinavyoweza kutokea katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kutoa taarifa kwenu na kwa mamlaka nyingine zinazohusika.

“Hivyo, nitumie fursa hii kuwaomba wadau wengine washirikiane zaidi na TAKUKURU katika kufikisha elimu ya mapambano dhidi ya rushwa kwa umma.

“Wahenga walisema ‘elimu ni ufunguo wa maisha’, na kwa mapambano dhidi ya rushwa elimu hiyo ni ufunguo wa ufahamu mpana wa jinsi ya kuikabili rushwa kwa mafanikio ya Taifa letu.

“Lakini nguvu zaidi ielekezwe katika kudhibiti mianya ya rushwa. Tukifanya hivo kwa wakati, tutaokoa fedha nyingi za umma hasa katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo. “Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19” inahusisha manunuzi na ujenzi wa miradi mingi ya maendeleo.

“Msibaki nyuma, fuatilieni kwa karibu matumizi yote ya fedha hizo zitakazotolewa kutekeleza kampeni hii ili zitumike kadiri ilivyokusudiwa na kwa mujibu wa sheria husika.

“Hatua hiyo itafanikisha kujengwa kwa miradi bora itakayotoa huduma bora kwa wananchi lakini itatujengea heshima kama nchi kuwa tunatumia vizuri fedha za mikopo ya maendeleo hivyo kuaminika zaidi na kupata mikopo mingine,”amefafanua Waziri Mchengerwa.

MIAKA 60 YA UHURU

Wakati huo huo, Waziri Mchengerwa amesema kuwa, mwaka huu, tarehe 9 Desemba tutaadhimisha miaka 60 ya Uhuru.

“Mambo mengi mazuri yamefanyika kuijenga Tanzania ikiwemo kutunza amani, upendo, umoja, mshikamano na kuendeleza mapambano dhidi ya umaskini, ujinga na maradhi.

“Haya yamefanyika kwa kujenga miundombinu bora ya kutoa huduma za afya, elimu na ile ya kukuza vipato vya wananchi na Taifa kwa ujumla. Juhudi zaidi zimefanyika kukabili tatizo la rushwa nchini.

“Tutafakari, Tanzania mikataba na mikopo yote je, ndani kwa ndani hakuna mifereji ya kutorokea maslahi ya taifa?, Mikopo yote na mikataba yote je, ina uadilifu wa yale hutangazwa ya kuondoa umaskini ama kuondoa uduni na udumavu kwa mambo mtambuka ya maslahi ya Taifa?.

“Nashukuru ndugu Mkurugenzi Mkuu kwa kunidokezea kuwa mtachapisha makala maalum gazetini kueleza hatua zilizochukuliwa na Serikali na wadau wengine katika miaka 60 ya kuzuia na kupambana na rushwa.

“Hiyo ni hatua nzuri ya kutuonesha sote tulikotoka, tulipo na tunapoelekea. Ninawaomba Watanzania wote na wadau wetu wa maendeleo tuendelee kushikamana kulinda na kudumisha yale tuliyofanikisha katika miaka 60 na kuongeza juhudi katika kufanya makubwa zaidi ya kimaendeleo ikiwemo kukabili tatizo la rushwa,”amesema.

ANGALIZO LA WAZIRI

“Taasisi yenu kuamini shutuma isiwe haraka haraka kwa kupokea taarifa za kutoka upande mmoja wa shilingi.

“Hii ni kufanya kazi kwa ubabaishaji wa kudhalilisha weledi na ni kupaka matope taasisi na Serikali yake.

“Viongozi wa taasisi msikimbie changamoto za mitego ya kuletewa mambo ya ukweli bandia hivyo mkiyabaini siyo aibu kufuta shutuma.

“Epukeni dhambi za kutafuta uongo mtamu wa kuthaminisha mambo ya kutengenezwa na ukweli bandia wa kuumiza Utu na Ubinadamu wa watu wanaobambikizwa kasoro za makosa potofu.

“Taasisi hii kuweni ni mamlaka ya awali ya siku rafiki ya kusikiliza utetezi wa kila mtu anayesutwa kuwa katenda uhalifu wa matakwa binafsi kumbe alilazimishwa na viongozi wake wakuu ambao hutumia hovyo yao madaraka.

“Taasisi hii iache woga wa hofu ya kufuta tuhuma za kuundwa na hasama za waumbaji fitina za kukomoa, ambazo hatma yake ni kufuta mvuto wa kuitwa hii ni Taasisi ya Haki za Jamii na haki za Taifa.

“Taasisi hii na Watumishi wake wote shindeni vishawishi vya kutengenezwa na hali za ugumu wa maisha.

“Taasisi msiigeuse kuwa mtaji wa dhamana za kujenga mazalia ya fumbuzi kwa maisha binafsi. Vyeo vyenu visiwe ni chombo cha kuvulia dhuluma za vishawishi katili kwa utu wa binadamu wanaotuhumika.

“Taasisi hii na viongozi ondoeni muhali wa hofu za woga za watumishi wa daraja la wadogo ambao hukaa kimya wameduwaa kwa yale wanayajua na viongozi hamyajui.

“Haya ni yale ya mawazo ya upekee wa kuchangia fikra kwa kutendeka maamuzi ya sifa sahihi na sifa makini za kuinua heshima ya taasisi. Wito wangu kwa watumishi wote, Taasisi hii iokoene na kasoro,”ameagiza Waziri Mchengerwa.


RUSHWA NI UGONJWA

Aidha, Waziri Mchengerwa alitumia nafasi hiyo kueleza kuwa, rushwa ni ugonjwa kama kansa, haitakiwi tuache iendelee kusambaa.

“Ninatambua kuwa mapambano dhidi ya rushwa ni vita, inahitaji kujipanga na kujitoa sadaka ikiwezekana uhai. Prof.Patric Lumbumba (PLO) alipokuwa akihutubia at the 3rd Anti-Corruption Convention alisema “Corruption is the war, we need to sacrifices for our lives, the question is are we ready to sacrifices”. Aliendelea kusema “we have good laws but what we need is confersersion of moral and change of the heart”.

“Mimi kiongozi wenu nimejitoa na nipo mstari wa mbele katika vita hii, hivyo napenda niwatie moyo nanyi ili tuweze kusimama pamoja katika mapambano haya kwa kuwa dhamana tuliyopewa ya kulitumikia taifa hili ni kubwa sana.

“Fanyeni kazi usiku na mchana, kufa na kupona ili kuokoa rasilimali za taifa hili. Naomba nimalizie kwa maneno machache ya Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Mhe. Benjamin Mkapa alipokuwa analihutubia Bunge mwaka 1995 aliwahi kusema “Maneno matupu, japo yawe matamu kiasi gani hayawezi kumaliza rushwa. Kushirikiana na kila mmoja kutimiza wajibu wake katika vita hivi, ndio mwanzo wa mafanikio”.

DC KONDOA

Naye Mkuu wa Wilaya ya Kondoa, Hamis Mkanachi akiongea kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amewataka viongozi hao kutumia mkutano huo kujadili tathimini ya mwaka mzima na zaidi wajikite katika kutatua uzembe pamoja na kutowajibika kwa baadhi ya viongozi wa taasisi hiyo.

“Wito wangu kwenu ni kwamba tathmini yetu iwe ya kina na tutazame namna tutakavyoweza kujipambanua katika kila wilaya namna bora ya utendaji,”amesema Mkanachi.

MKURUGENZI TAKUKURU

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu kutoka katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), Salumu Hamduni amesema wametekeleza majukumu na kwa kipindi cha mwaka 2020 hadi 2021 jumla ya shilingi bilioni 29.3 ziliokolewa ambapo bilioni 11 .2 ziliokolewa kwa mfumo wa fedha taslimu na utaifishaji mali na kiasi cha bilioni 18 zilidhibitiwa kabla hazijatumika.
Amesema, miradi ya kimaendeleo 1,188 zenye thamani ya bilioni 714.17 katika sekta ya afya, maji, elimu ziliweza kufatiliwa na kuona makosa ambayo wameyachukulia hatua.

“Tumeelimisha katika ngazi ya makao makuu pamoja na wakuu wa TAKUKURU kuzuia vitendo vya rushwa kuelimisha, kushirikisha jamii pamoja na kuwafikisha watumiwa mahakamani kwa kushirikiana na Ofisi ya Taifa ya Mashtaka majalada 1,053 yalichunguzwa na kukamilishwa na majadala 339 yaliwasilishwa kwa Mkurugenzi wa Mashitaka kuomba kibali cha kuwafikisha mahakamani ambapo kesi mpya zilipatikana 542, na kesi 541 zilitolewa uamuzi ambapo Jamhuri iliweza kushinda kesi 345,”amesema Hamduni

Aidha, akizungumzia changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, Hamduni amesema ni pamoja na ufinyu wa bajeti ambao umeathiri uchunguzi, mafunzo kwa wafanyakazi, ununuzi wa vifaa na mahitaji mbalimbali pamoja na uhaba wa wafanyakazi.
 
Aidha, akizungumzia changamoto zinazoikabili taasisi hiyo, Hamduni amesema ni pamoja na ufinyu wa bajeti ambao umeathiri uchunguzi, mafunzo kwa wafanyakazi, ununuzi wa vifaa na mahitaji mbalimbali pamoja na uhaba wa wafanyakazi.Mkutano huu Mkuu wa Mwaka wa Viongozi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Ruswa nchini (TAKUKURU) umefunguliwa leo Novemba 25, 2021 na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mheshimiwa Mohamed Mchengerwa katika Hoteli ya Morena jijini Dodoma ambapo utaendelea hadi Novemba 27,2021.

Pia mkutano huu unahudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU,CP. Salum Rashid Hamduni, Naibu Mkurugenzi Mkuu,Bi. Neema Mwakalyelye, wakuu wa vitengo na wakurugenzi wasaidizi pamoja na wakuu wa TAKUKURU mikoa yote nchini. 
 
Hata hivyo, mkutano huo wa siku tatu wa viongozi wa TAKUKURU umebebwa na kauli mbiu isemayo ”Kupambana na Rushwa ni Jukumu lako”.

Post a Comment

0 Comments