Maamuzi ya Serikali kuhusu ukusanyaji ushuru wa maegesho

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) imeridhia kurudisha Mfumo wa Ukusanyaji Ushuru wa Maegesho kwa Njia ya Kielektroniki (TeRMIS) uanze kutumika tena kuanzia Desemba Mosi, 2021 katika maeneo yote ambapo mfumo huo umefika.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (0R-TAMISEMI), Mhe. Ummy Mwalimu ameyasema hayo Novemba 5, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.

Mheshimiwa Waziri amesema kuwa , hadi sasa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais-TAMISEMI tayari wamezifanyia kazi changamoto zilizojitokeza katika matumizi ya mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji ushuru wa maegesho ambapo ilikuwa changamoto kwa watumiaji.

“Ukusanyaji wa ushuru wa maegesho ya magari kwa kutumia mfumo wa TerMIS utapunguza mianya ya upotevu wa mapato ya Serikali na kuwezesha fedha hizo kuingia moja kwa moja serikalini. Kutokana na umuhimu wake ninarejesja matumizi ya mfumo huu kuanzia tarehe 1 Desemba 2021,”amesema.

Pia amesema , miongoni mwa changamoto ambazo wamezifanyia kazi ni pamoja na wateja kutopatiwa taarifa za kudaiwa ushuru wa maegesho kwa wakati, kiwango kikubwa cha gharama za maegesho, muda wa kulipa ambapo hapo awali mtumiaji wa maegesho alitakiwa kulipa ushuru ndani ya siku saba tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo alipaswa kulipa mara mbili ya ushuru aliokuwa anadaiwa.

Aidha, na endapo atazidisha siku 14 pia alitakiwa ushuru wa maegesho pamoja na faini ya shilingi 30,000.

“Mtumiaji wa maegesho sasa atatakiwa kulipa ushuru ndani ya siku 14 badala ya siku saba tangu alipotumia maegesho na endapo atashindwa kulipa ndani ya muda huo atatakiwa kulipa ushuru wa maegesho pamoja na faini ya shilingi 10,000 badala ya shilingi 30,000 zilizokuwa zikitozwa awali. Hivyo adhabu ya shilingi 30,000 nimeifuta,”amesema Waziri Ummy.

Wakati huo huo, Waziri ameitaka TARURA kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi hasa kwa mikoa ilioanza kutumia mfumo huo ikiwemo Dar es Salaam, Mwanza, Singida, Iringa na Dodoma ili kuwepo na uelewa wa kutosha kabla ya kuanza tena kwa matumizi ya mfumo huo muda uliopangwa.

Post a Comment

0 Comments