Makachero wadaka wahamiaji 18 mjini Makete

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MAKACHERO wa Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na vikosi vya Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Njombe wamefanya msako katika Kitongoji cha Isaganilo kilichopo wilayani Makete mkoani Njombe na kufanikiwa kuwakamata wahamiaji haramu 18 na Mtanzania mmoja aliyekuwa akijaribu kuwavusha ili kuingia nchini Malawi.
Akitoa onyo kwa wahusika wa biashara hiyo ya giza, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Njombe, John Yindi amesema kumekuwa na mikasa mingi ya kukamatwa kwa wahamiaji haramu wakitoka nchi jirani, lakini hadi sasa wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kuutia nguvuni mtandao wa biashara hiyo inayopingwa vikali duniani.

Kamanda Yindi amesema, mafanikio makubwa waliyoyapata hivi karibuni yametokana na ushirikiano mkubwa kutoka kwa wananchi wa maeneo mbalimbali ya mkoa wa Njombe ambao wamekuwa wakivujisha taarifa na kwamba tabia ya kuwafichua wahusika inapaswa kuendelea kwa usalama wa wananchi na taifa kwa ujumla.

“Tumefanikiwa kuwakama wahamiaji katika maeneo mbalimbali ya mkoa wa Njombe, hatua ambayo ni matokeo ya wananchi wazalendo ambao wamekuwa wakitoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama juu ya uwepo wa watu wasiowatambua katika makazi yao,"amesema Kamanda wa Jeshi la Uhamiaji Mkoa wa Njombe.

Katika operesheni hiyo, Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah amesema mamia ya wahamiaji haramu wanaokamatwa mkoani humo wanashirikiana na Watazania, hivyo jeshi halitamuacha salama atakayebainika kutumia chombo chake kuwavusha watu hao.

“Tumewakamata wahamiaji 18 akiwemo mtanzania mmoja ambaye alikuwa akisafirisha watu hao jambo ambalo ni kinyume cha taratibu na jeshi limejizatiti kudhibiti watu hao hadi watakapo koma,"amesema Kamanda Issah.

Wiki tatu zilizopita Jeshi la Uhamiaji liliwakamata wahamiaji haramu 52 wilayani Wanging’ombe mkoani Njombe wakitokea nchi za Ethiopia na Malawi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news