Mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Dkt.Mwinyi ulivyoleta mwanga na matumaini makubwa Zanzibar

NA RAJAB MKASABA

"Kama nilivyozungumza wakati napokea matokeo ya uchaguzi pale Maruhubi na leo naomba nirejee tena lengo letu ni kuijenga Zanzibar na Zanzibar mpya itajengwa na sisi sote bila kujali tofauti zetu za kiitikadi, nina waahidi nipo tayari kuyaridhia maridhiano yalio katika katiba yetu ya Zanzibar na kushirikiana na nyinyi kuijenga Zanzibar mpya na Zanzibar ni muhimu kuliko tofauti zetu;

Hayo ni maelezo ya Rais Dkt. Mwinyi katika sehemu ya hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, sherehe iliyofanyika katika uwanja wa Amaan jijini Zanzibar mnamo Novemba 2, 2020 ambapo tayari umeshatimia mwaka mmoja hivi sasa tokea aingie madarakani na mwanga mkubwa wa matumaini umeanza kuangaza katika kuieletea Zanzibar maendeleo endelevu.
Aliyekuwa Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu akimuapisha Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi (kulia) kuongoza Zanzibar kwa Awamu ya 8 kuanzia 2020-2025 katika sherehe za kiapo zilizofanyika katika uwanja wa Amaan jijini Zanzibar.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Dkt. Mwinyi aliahidi kwamba Serikali atakayoiunda itaongoza katika misingi ya haki,uwajibikaji,uwazi,usawa kwa wananchi wote bila ya kumbagua mtu yeyote kutokana na itikadi ya jinsia,siasa,dini ama eneo analotoka.

Alisema, Wazanzibari wote ni wamoja na wana haki ya kunufaika na rasilimali zilizopo kwa misingi ya usawa" Ninachowaahidi ni kuunda serikali makini," alisisistiza.

Rais Dkt. Mwinyi alieleza kwmaba katika serikali atakayoiunda atazingatia nidhamu, maadili ya viongozi,watumishi wa umma, utendaji kazi wenye viwango bora, kasi ya kimaendeleo ya kiuchumi pamoja na kuimarisha huduma za kijamii kwa kuzitumia vyema rasilimali zilizopo kwa manufaa ya Wanzanzibar.

Aliahidi kuwa katika kipindi cha uongozi wake atahakikisha anashirikiana na viongozi atakaowateua pamoja na wananchi katika kufanikisha utekelezaji wa mipango mikuu ya maendeleo ikiwemo muongozo uliomo katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2020/2025, Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2020-2050,malengo ya maendeleo endelevu ya kimataifa pamoja na ahadi alizozitoa kwa wananchi wakati wa kampeni.

"Nawashukuru wote mliojitokeza katika sherehe hii muhimu ya kihistoria wakiwemo viongozi wa staafu na mabalozi wa mataifa mbalimbali,"alisema Rais Dkt.Mwinyi.

Aliwashukuru wananchi kwa kujitokeza kwa wingi kupiga kura Oktoba 28 hii ni kielelezo cha kuonyesha namna mlivyokomaa kisiasa,kidemokrasia na kutambua kuwa uchaguzi ndio njia sahihi kuwapata viongozi wa Zanzibar kwa misingi ya sheria.

"Sote tunathamini sana heshima mliotupa ambayo ni kielelezo cha upendo wenu kwa CCM na sisi tutahakikisha tunatekeleza wajibu wetu ipasavyo kwa kuwatumikieni katika kuziinua hali za wananchi ili ziwe bora zaidi,"alisisitiza Rais Dkt. Mwinyi.

Katika hotuba yake hiyo aliyoitoa mara baada ya kuapishwa na Jaji mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, kuwa Rais wa Awamu ya Nane ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,Rais Dkt. Mwinyi aliwaeleza wananchi kwamba atatekeleza ufanisi ahadi zote alizotoa wakati wa kampeni za uchaguzi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt.Hussein Ali Mwinyi akipongezwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati huo ambapo Rais Samia alikuwa Makamu wa Rais Mteule wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, baada ya Dkt. Mwinyi kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo kwa awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Alisisitiza kwamba Serikali atakayoiunda itashirikiana na vyama vya upinzani vilivyokubali na kuridhishwa na matokeo ya urais yaliyotokana na uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 28, mwaka jana.

Rais Dkt. Mwinyi alitumia fursa aliyoipata siku hiyo kwa kuwapongeza wagombea wa vyama vya upinzani kwa kuheshimu maamuzi ya wananchi na kutoa ahadi ya kushirikiana nao katika serikali atakayoiunda.

"Ndugu zangu ninawapongeza wagombea wenzangu kwa nafasi ya urais kwa kuheshimu maamuzi ya wananchi na ninatoa ahadi ya kuwa nitashirikiana nanyi katika serikali nitakayoiunda katika kuwatumikia wananchi katika kuijenga Zanzibar,"alisema.

Katika hotuba hiyo Dkt. Mwinyi alisema kuwa amepata imani kubwa kutokana na maelezo yaliyotolewa na mgombea urais wa chama cha ADA-TADEA,Juma Ali Khatib, mara baada ya kutangazwa matokeo ya Urais, huko katika ukumbi wa Chuo cha Utalii Maruhubi, Mkoa wa Mjini Magharibi mnamo Oktoba 29,2020 wakati akitoa neno la shukurani kwa niaba ya vyama mbalimbali vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi mkuu.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akipongezwa na Rais mstaafu wa Zanzibar Mzee Ali Hassan Mwinyi Mwinyi baada ya kuapishwa rasmi kushika wadhifa huo awamu ya nane ya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hafla ilifanyika katika Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar.

Rais Dkt.Mwinyi alisema kuwa ahadi na kauli za viongozi hao wa upinzania zilimpa matumanini makubwa ya kushirikiana katika kuendelea kuijenga Zanzibar mpya yenye neema tele kama alivyowahidi wananchi kwa upande wa Unguja na Pemba wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu.

Mapema Oktoba 29, mwaka 2020 Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ilimtangaza Dkt. Hussein Ali Mwinyi kupitia tiketi ya CCM kuwa mshindi wa kiti cha Urais wa Zanzibar baada ya kupata kura 380,402 sawa na asilimia 76.27 ya kura zote.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi akikaribishwa Ikulu Zanzibar na Rais Mstaafu wa Awamu ya Saba wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein, mara baada ya kuapishwa huko katika uwanja wa Amaan jijini Zanzibar katikati ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mstaafu Balozi Seif Ali Idd.

Akitangaza matokeo hayo Mwenyekiti wa ZEC Jaji mstaafu Hamid Mahmoud alisema wagombea uraisi walikuwa 17 waliopigiwa kura 498,786 sawa na asilimia 88.07 ya wapiga kura 566,352 waliojiandikisha, amesema kura zilizoharibika ni 10,944 sawa na asilimia 2.19.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 96 (2 na 3) cha sheria namba 4 ya 2018 namtangaza rasmi Dkt.Hussein Ali Mwinyi wa CCM kuwa amechaguwaliwa na wananchi wa Zanzibar kuwa mshindi wa kiti cha Urais wa Zanzibar katika uchaguzi uliofanyika Oktoba 28, 2020,” alisema Jaji Mstaafu Hamid Mahmoud wakati akitangaza matokeo hayo.

Post a Comment

0 Comments