Mwanamfalme William afunguka mazito kuhusu uhifadhi wa wanyamapori, awapa tuzo za kifahari Waafrika watatu

NA GODFREY NNKO

TUZO za kifahari za Tusk Conservation Awards zimerejea usiku wa kuhamkia leo Novemba 24, 2021 jijini London nchini Ungereza kama tukio la ana kwa ana baada ya onesho la mwaka jana kutofanyika kwa njia hiyo kutokana na sababu ya mlipuko wa Virusi Vya Corona (UVIKO-19).
Mwanamfalme William (katikati) akiwa na washindi wa tuzo za kifahari za Tusk Conservation Awards kutoka nchini Namibia, Nigeria na Madagascar baada ya kuwakabidhi usiku wa kuhamkia leo Novemba 24, 2021. (Picha na Reuters).

Mwanamfalme William aliwasili katika Ukumbi mashuhuri wa BFI Southbank mjini London akiwa na tabasamu la kipekee, tayari kwa ajili ya kutangaza washindi wa tuzo hizo maarufu kama Tusk Conservation Awards.

Duke huyo wa Cambridge mwenye umri wa miaka 39 aliwasili ukumbini hapo akiwa na furaha si tu kwa sababu anatoa tuzo, bali kutokana na mchango wa watu hao ambao wamekuwa walinzi wema wa wanyamapori barani Afrika.

Mwanamfalme William alizindua sherehe hizo za kila mwaka ambazo zilianza mwaka 2013 ili kuangazia na kusherehekea mafanikio ya mashujaa wa Afrika ambao wameonesha ari na moyo safi katika juhudi za kuhifadhi na kuwalinda wanyamapori ili wasipotezwe na majangili.

Katika hafla hiyo, Mwanamfalme huyo alianza kwa kukabidhi kila mshindi tuzo kabla ya kutoa hotuba na kisha kuhudhuria tafrija maalum na wanachama wakuu na Wakfu wa Tusk (Tusk Trust).

Pia Mwanamfalme huyo alizungumza na washindi wa tuzo hizo ili kusikia zaidi juu ya kazi zao wakati wakiwa mstari wa mbele katika juhudi za uhifadhi barani Afrika.

Katika hotuba yake, Mwanamfalme William ametoa pongezi kwa wote ambao wanahatarisha maisha yao ili kulinda wanyamapori ambapo wapo katika hatari ya kutoweka barani Afrika.

"Baada ya mkutano wa COP26, ni wazi kwamba lazima tuone mazingira, uhifadhi na mabadiliko ya hali ya hewa yanapewa uzito. Kila mmoja wetu anatambua wazi kuwa, bioanuwai yenye utajiri wa ajabu barani Afrika ina uwezo mkubwa sana. Lakini haya yanawezekana tu ikiwa mazingira haya yatabaki kuwa sawa na yanalindwa kama mifumo ya ikolojia inayofanya kazi,"amesema.

“Uhifadhi wa wanyamapori wetu una muhimu mkubwa sana katika kuendeleza mazingira ya asili na kurejesha ustawi bora wa mazingira kwa ajili ya kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi. Ikiwa hatutakuwa na nguvu moja katika kusimamia na kuhifadhi wanyamapori na mazingira yetu, tusitegemee kuwa na uendelevu wa uoto wa asili.Tutaendelea kuzidisha mabadiliko ya tabia nchi ambayo yamekuwa na matokeo mabaya katika hali ya hewa duniani, tuendelee kuhifadhi na kulinda mazingira yetu,"amesema.

Pia aliangazia athari mbaya za Ugonjwa wa Virusi vya Korona (UVIKO-19) kwenye miradi ya uhifadhi barani Afrika ambayo amesema, janga hilo limesababisha mapato ya utalii kushuka kwa kasi katika miezi 18 iliyopita.

"Afrika imeathiriwa sana, kwani uchumi, kazi na maisha vimeharibiwa na maagizo ya kukaa ndani na vizuizi vya kusafiri. Miradi mingi ya Tusk ambayo nimepata bahati ya kutembelea imeathiriwa sana, hasa pale ambapo kuna utegemezi wa utalii ili kudumisha kazi yao ya uhifadhi,"amesema.

Mwanamfalme William, ambaye ana mamlaka ya Kifalme katika Wakfu Tusk (Tusk Trust) ameshiriki katika tuzo hizo za kila mwaka mara kadhaa na mwaka jana alirekodi ujumbe wa video akiwapongeza washindi.

WASHINDI

Mtendaji Mkuu wa Save the Rhino Trust nchini Namibia, Simson Uri-Khob ndiye mshindi wa kwanza katika Tuzo ya Mwanamfalme William ya Uhifadhi Afrika, akiheshimu kazi yake kwa zaidi ya miaka 30 katika kuokoa idadi ya faru weusi nchini Namibia.

Aidha, Suleiman Saidu ambaye ni mlinzi mkuu wa wanyamapori katika Pori la Akiba la Yankari nchini Nigeria ameshinda Tuzo ya Mhifadhi wa Wanyamapori ya Tusk kwa ushujaa wake na juhudi za kupunguza ujangili wa tembo ambao hapo awali ulikuwa umeenea hadi kufikia kisa kimoja tu tangu mwaka 2015.

Saidu ametoa tuzo yake kwa walinzi 100 wa mbuga za Kiafrika ambao kwa wastani hupoteza maisha yao katika maeneo ya kazi kila mwaka, wengi wakiuawa na wawindaji haramu wanaowinda wanyama walio hatarini kutoweka.

Naye Julie Razafimanahaka ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Madagasikara Voakajy ambalo ni Shirika la Uhifadhi nchini Madagaska ameshinda Tuzo ya Tusk kwa Uhifadhi barani Afrika kwa kazi yake ya kuhifadhi msitu wa mvua wa Mangabe na viumbe mbalimbali wanaoishi humo kwa mafanikio makubwa.

Mwanamfale William amekuwa pia mlezi wa Shirika la Royal African Society linalolenga kukuza uhusiano kati ya Afrika na Uingereza na hushiriki sana juhudi za kukabiliana na ujangili na kuendeleza uhifadhi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news