Rais Dkt.Mwinyi atoa maagizo ya kuneemesha vijana kwa viongozi wa wilaya, mikoa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameutaka uongozi wa mikoa na wilaya zote nchini kuhakikisha vijana wa Kizanzibari wanapewa kipaumbele katika upatikanaji wa nafasi za ajira katika miradi yote ya uwekezaji inayotekelezwa katika maeneo yao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi,Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi akiondoa kipazia kuashiria kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa Hoteli ya Kitalii ya L’oasis Beach Resort Kizimkazini Mkoa wa Kusini Unguja, kushoto ni Mkurugenzi wa mradi huo, Bw.Ahmed Saber akiondoa kipazia, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha mwaka mmoja wa uongozi wake, hafla hiyo imefanyika katika eneo la ujenzi wa hoteli hiyo Kizimkazini.


Dkt. Mwinyi ametoa wito huo leo katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi wa Hoteli ya Kitalii ya L’oasis Beach Resort iliyopo Kizimkazi Dimbani Mkoa wa Kusini Unguja, ikiwa ni maadhimisho ya kutimiza mwaka mmoja tangu kiongozi huyo aingie madarakani.

Amesema, viongozi wa mikoa na wilaya pamoja na wawekezaji wana wajibu wa kuhakikisha vijana wa Kizanzibar, hususan wale walioko katika maeneo ya miradi wanapewa kipaumbele katika suala la uaptikanaji wa nafasi za ajira ili waweza kunufaika na uwepo wa uwekezaji huo. 

Mheshimiwa Rais Dkt. Mwinyi amesema, viongozi hao pia wana jukumu la kusimamia na kuhakikisha hoteli hizo zinanunua bidhaa zote zinazopatikana au kuzalishwa katika maeneo hayo, ikiwemo bidhaa zitokanazo na uvuvi, kilimo, pamoja na ufugaji, ikiwa ni hatua ya wananchi hao kupata soko la bidhaa zao.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakipiga makofi baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Hoteli ya Kitalii ya L’oasis Beach Resort Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja na kushoto ni Mkurugenzi wa mradi huo, Bw.Ahmed Saber, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji, Mhe. Mudrik Soranga, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Rashid Hadidi Rashid na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamkaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar.(ZIPA) Bw.Sharif Ali Sharif, wakipoga makofi baada ya kuwekwa kwa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Mradi huo, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha Mwaka Mmmoja wa Uongozi wake Dkt. Mwinyi.

Rais Dkt. Mwinyi akwia amefuatana na Mama Mariam Mwinyi katika hafla hiyo, aliwataka viongozi hao kuhakikisha wawekezaji wanasaidia upatikanaji wa huduma za jamii katika maeneo wanayowekeza, ikiwemo suala la maji, elimu, huduma za afya pamoja na miundombinu ya barabara. “Wajibu wa wawekezaji katika kuisaidia jamii ufanyike vyema,”amesisistiza.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alieleza kuwa wawekezaji wako tayari kuwekeza baada ya kujenga imani kubwa na Serikali kutokana na kuwepo kwa amani, umoja na mshikamano nchini, hivyo akabainisha umuhimu wa uwekezaji huo kuleta tija kwao na kwa Taifa.

Amewashukuru wawekezaji hao kwa imani hiyo na kuwekeza miradi mikubwa hapa nchini, hivyo akatumia fursa hiyo kuwataka wananchi kuendelea kuitunza amani iliyopo ili utalii uweze kuleta tija na manufaa kwa Taifa na wananchi kwa ujumla.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akimsikiliza Mhandisi wa Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya L’oasis Beach Resort Kizimkazini, Mwinyi Sarboko akitoa maelezo ya ujenzi huo baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha Mwaka Mmoja wa Uongozi wake, hafla hiyo imefanyika katika viwanja vya ujenzi huo Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja.
Wananchi wa Kizimkazi wakimsiliza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi (hayupo pichani) akizungumza na wananchi hao baada ya kuweka Jiwe la Msingi la Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Kitalii, ikiwa ni shamrashamra ua kuadhimisha Mwaka Mmoja wa Uongozi wake.

Amesema, Sekta ya Utalii itaendelea kuwa sekta kuu ya uchumi wa Zanzibar, mbali na uchumi huo kushuka kutokana na janga la ugonjwa wa UVIKO 19 ulioikumba dunia.

Hata hivyo, alieleza kuwa hali imeendelea kutengemaa baada ya ugonjwa huo kuonyesha dalili za kupungua, hivyo akawataka wanachi kuendelea kumuomba Mwenyezi Mungu ili ugonjwa huo umalizike kabisa.

Mapema, Mkuu wa Mkoa Kusini Unguja, Hadidi Rashid Hadidi alisema uongozi wa Mkoa huo kwa kutambua kuwa Mkoa uko katika ukanda wa Utalii, umelazimika kuweka kipambele katika suala la usafi katika maeneo yote ya Mkoa huo. Alisema hatua ya kufanyika maridhianao ya kisiasa hapa nchini kumeshajiisha uwepo wa amani na hivyo kuhamasisha shughuli za uwekezaji.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Wananchi wa Kijiji cha Kizimkazi Mkoa wa Kusini Unguja (hawapo pichani) wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Hoteli ya Kitalii ya L’oasisi Beach Resort, ikiwa ni shamrashamra za kuadhimisha Mwaka Mmoja wa Uongozi wake.(Picha na Ikulu)

Mkuu wa Mkoa huyo alieleza kuwa Mwekezaji wa Hoteli ya L’ oasis Beach Resort ameweza kutekeleza mradi huo kutokana na imani kubwa aliyonayo kutokana na uhamasishaji unaofanywa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi.

Nae Mkurugenzi wa Mradi huo wa Hoteli ya L’oasis Beach Resort, Ahmeid Saber alimshukuru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kuunga mkono utekelezaji wa mradi huo, pamoja na kuahidi kutekeleza kikamilifu sheria na miongozo yote ya Uwekezaji.

Ujenzi wa Hoteli ya L’oasis Beach Resort umegharimu Dola za Kimarekani Milioni 15, inahusisha vyumba 142, ikiwemo vyumba maalum vyenje hadhi ya juu 14 pamoja na Mabwawa ya kuogelea 23, ikiwa na jumla ya wafanyakazi 150 kati yao 103 kutoka Shehiya za Kizimkazi na pale ujenzi wake utakapokamilika itakamilisha ajira za vijana 300.

Post a Comment

0 Comments