Rais Dkt.Mwinyi azidi kufungua anga Zanzibar, Serikali yake yalenga makubwa

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Mwinyi amesema uamuzi wa Serikali wa kushirikiana na kampuni za National Air Travel Agency (DNATA) pamoja na EGIS katika uendeshaji wa Huduma za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Terminal 111, unalenga kuimarisha uchumi kwa mtazamo mpana ili kuvutia mashirika ya ndege zaidi kufanya safari zake hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji saini mkataba wa mashirikiano ya uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na DNATA kulia ni Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Amour Hamil Bakari na Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya EGIS, Cristian Laugier, hafla hiyo imefanyika Novemba 24, 2021 Ikulu jiini Zanzibar. (Picha zote na Ikulu).

Dkt. Mwinyi amesema hayo katika shughuli ya utiaji saini wa mkataba wa Mashirikiano ya Uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (Terminal 111), baina ya Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi na Dubai National Air Travel Agency (DNATA), pamoja na Kampuni ya EGIS hafla iliofanyika Ikulu jijini Zanzibar.

Alieleza kuwa, ongezeko la ndege utaongeza idadi ya watalii wanaokuja kuitembelea Zanzibar, wageni, mizigo na ukuaji wa biashara pamoja na soko la ajira.

Alisema, ujio wa watalii utaambatana na ukuaji wa sekta mbalimbali muhimu katika ukuaji wa uchumi, akibainisha uamuzi huo wa Serikali umelenga kuleta manufaa mapana ya kiuchumi katika sekta zote.

Rais Dkt.Mwinyi alizitaka taasisi zote zinazofanya kazi katika uwanja huo wa ndege ikiwemo za Serikali na binafsi kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi.

Alizitaja taasisi hizo ikiwemo Idara ya Uhamiaji, ZRB, Watendaji wa Wizara Afya pamoja na vyombo vya Ulinzi na Usalama kushirikiana na kampuni hizo na kuboresha utendaji wao na kutoa huduma bora kwa wageni, vinginevyo mafanikio yanayotarajiwa kamwe hayawezi kufikiwa.

Aidha, aliishukuru wajumbe wa Kamati ya majadiliano ya Serikali kwa kazi nzuri waliyofanya mpaka kufikia makubaliano hayo yenye maslahi na Taifa, huku akibainisha kuwa zoezi hilo lilikuwa zito , gumu na lililochukua muda mrefu kukamilika.

“Nimeridhika sana kwamba mikataba hii tuliotiliana saini imezingatia maslahi mapana ya nchi yetu,”alisema.

Rais Dkt. Mwinyi alisema, Serikali imeamua kutafuta kampuni zenye sifa Duniani ili kuja kusaidiana katika uendeshaji wa Huduma za Kiwanja hicho cha Ndege kwa lengo la kuwa huduma zenye kiwango cha kimataifa.
Baadhi ya viongozi na wageni mbalimbali walioalikwa katika hafla ya utiaji saini Mkataba wa mashirikiano ya uendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume baina ya Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi na Dubai National Air Travel Agency iliyofanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Alisema, Serikali imewekeza fedha nyingi zipatazo Dola za Kimarekani Milioni 128 kwa ajili ya ujenzi wa Terminal 111, pamoja na kuimarisha miundombnu ya barabara nje ya kiwanja, ujenzi wa uzio pamoja na maegesho ya magari, hivyo imelazimika kutafuta kampuni zenye uwezo wa kimataifa ili kuwa na huduma zinazofanana na hadhi ya Terminal 111.

Alisema, kamapuni hizo zilizopatikana katika mchakato wa kuendesha huduma katika uwanja huo zina uwezo mkubwa na kutambulika kimataifa.

Aliongeza kuwa, kampuni hizo zimekuwa zikiendesha shughuli katika nchi mbalimbali Duniani, ambazo zinafanana na zile zilizokabidhiwa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, na kubainisha matumaini yake ya kupata huduma zinazohitajiwa.

Dkt. Mwinyi alisema Kampuni ya DNATA inatambulika kwa uwezo wake mkubwa katika uendeshaji wa Viwanja vya Ndege vipatavyo 126 Duniani kote,ikiwa imeanzishwa tangu mwaka 1959.

Aidha, alisema kampuni hiyo ina uwezo mkubwa katika ushughulikiaji wa huduma za abiria, ushughulikia mizigo, kuweka taratibu nzuri na mwenendo wa ndege, pamoja na masuala mbalimbali ya usalama wa abiria na mizigo katika viwanja vya ndege.
 

Mapema, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Rahma Kassim Ali aliipongeza Kampuni ya DNATA kwa kuteuliwa kuendesha huduma za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume Terminal 111, hivyo akaiomba kufanya shughuli zake kwa ufanisi, sambamba na kuwarithisha uzoefu wafanyakazi wazalendo ili kuwa bora na endelevu.

Alisema, utiaji saini wa mikataba minne juu ya uendeshaji wa huduma katika uwanja huo ni miongoni mwa juhudi za serikali katika uimarishaji wa miundombinu ya anga pamoja na kurahisisha shughuli za usafiri na usafirishaji.

Alisema, Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi iliona ipo haja ya kushirkiana na Kampuni za DNATA na EGIS kwa kuzingatia uzoefu na kutambulika kwao Kimataifa.

Nae, Makamu Mwenyekiti wa Kampuni ya DNATA ambae pia ni Mwenyekiti wa Kampuni ya Emirates Leisure, Steve Allen alisema kupitia ushirikiano uliotiwa saini na kampuni hiyo itaweza kuzalisha ajira zisizo rasmi zipatazo 400 kwa wazawa, sambamba na kuimarisha huduma katika uwanja huo wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume (terminal 111).

Aidha, Mkurugenzi wa Biashara wa Kampuni ya EGIS Christian Laugier alisema kampuni hiyo inatoa huduma katika viwanja vya ndege 17 Barani Afrika, Zanzibar ikiwa cha tano miongoni mwao.

Jengo la Terminal 111 ambalo limefikia asilimia 90 ya ujenzi wake na linalotarajiwa kukabidhiwa Serikalini hivi karibuni, limejengwa na Kampuni ya Beijing Contract Engineering Group (BCEG) kutoka nchini China, likiwa na urefu wa mita za mraba 25,000 na uwezo wa kuhudumia abiria 1,6000,000 kwa mwaka.

Katika hafla hiyo jumla ya mikataba minne imetiwa saini, ikiwemo Mkataba wa Huduma za Abiria na mizigo, mkataba wa huduma za Uendeshaji, mkataba wa kumbi za wageni pamoja na mkataba wa uendeshaji wa huduma za Maduka na Migahawa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news