Rais Samia ateta na Katibu Mtendaji wa African Leaders Malaria Alliance (ALMA)

NA MWANDISHI MAALUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo Novemba 8, 2021 amekutana na kuzungumza na Katibu Mtendaji wa African Leaders Malaria Alliance (ALMA), Bi. Joy Phumaphi, Ikulu Chamwino mkoani Dodoma.  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Katibu Mtendaji wa African Leaders Malaria Alliance (ALMA) Bibi. Joy Phumaphi, mara baada ya kuwasili Ikulu Chamwino Mkoani Dodoma leo Novemba 8, 2021.(PICHA NA IKULU).

Katika mazungumzo hayo, Mhe. Rais Samia amemshukuru Bi. Phumaphi na kumhakikishia ushirikiano wa Serikali katika kukabiliana na malaria nchini pamoja na kupunguza vifo vya mama na mtoto.

Mhe. Rais Samia amesema jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa na Serikali, ikiwa ni pamoja na uundwaji wa Mabaraza ya Malaria ngazi zote pamoja na kupitia Umoja wa Wabunge wa Tanzania walio katika mapambano dhidi ya Malaria (TAPAMA) ambao wanafanya kazi kubwa ya kusaidia mapambano dhidi ya ugonjwa wa Malaria katika majimbo yao.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemuomba Bi. Phumaphi kuisaidia Tanzania kupata teknolojia ya kisasa ili kuboresha vyandarua vinavyozalishwa nchini pamoja na kuwezesha viuadudu vya kibaiolojia kuweza kutambulika kimataifa ikiwa ni moja ya jitihada za kuwezesha Serikali kufikia lengo la kutokomeza ugonjwa wa Malaria kufikia sifuri ifikapo mwaka 2030.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa ALMA Bi. Phumaphi amemshukuru Mhe. Rais Samia kwa ushirikiano wake na ALMA na kumpongeza kwa jitihada mbalimbali anazochukua kukabiliana na ugonjwa wa Malaria nchini Tanzania.

Bi. Phumaphi amesema Tanzania ni mojawapo ya nchi za kuigwa Afrika kutokana na mafanikio iliyoyapata katika mapambano dhidi ya ugonjwa huo, hivyo ALMA itaendelea kufanya kazi na Serikali ya Tanzania katika kukabiliana na changamoto mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news