Rais Samia: Tuendelee kumuenzi Hayati Maalim Seif Sharif Hamad

NA MWANDISHI MAALUM

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka Wazanzibari kumuenzi Hayati Maalim Seif Sharif Hamad kwa kuendeleza mshikamano na umoja wa Kitaifa ili Zanzibar izidi kupata maendeleo makubwa.
Mhe. Rais Samia amesema hayo Novemba 5, 2021 wakati akihutubia katika Kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamadi, katika hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip, Mjini Unguja.

Akimzungumzia Hayati Maalim Seif, Mhe Rais. Samia amesema alikuwa daraja la amani na mtu aliyeongozwa na maono ya maslahi mapana ya taifa hivyo hatuwezi kuizungumzia amani ya Zanzibar na Tanzania bila kumtaja Maalim Seif.

Pia Mhe Rais. Samia amebainisha kuwa hata pale wafuasi wake walipokuwa na msimamo tofauti, daima alikuwa na ushupavu katika uongozi na uwezo wa kushawishi kukubalika kwa jambo analoliamini hali iliyopelekea kupunguza jazba ya wafuasi wake.
Mhe Rais. Samia amemuelezea Hayati Maalim Seif kuwa alikuwa kiongozi jasiri aliyekuwa na uwezo wa kwenda kinyume na mawazo ya wafuasi wake hali inayotoa funzo kwa wanasiasa wengine kusimamia wanachokiamini lakini kuweka mbele maslahi ya taifa.

Aidha, Mhe Rais. Samia amesema Hayati Maalim Seif ataenziwa hata na Chama cha Mapinduzi (CCM), kwa kuacha alama nzuri katika uongozi wake hasa wakati alipokuwa kijana na kiongozi mkubwa ndani ya Chama na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa mfumo wa chama kimoja.
Aidha, Mhe. Rais Samia amesema baadhi ya wanasiasa wanapotofautiana huanzisha vurugu zisizoisha tofauti na alivyokuwa Hayati Maalim Seif ambaye aliamini kumaliza tofauti zinazojitokeza kwa majadiliano na maridhiano, jambo ambalo Maalim Seif alisimamia wakati wote wa uhai wake.

Mhe. Rais Samia amesema jambo jengine ambalo Maalim Seif atabaki kukumbukwa ni tabia yake ya kupingana kwa kutumia hoja na sio lugha zisizo na staha kama ilivyo kwa baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa nchini.

Akizungumzia juu ya suala la mabadiliko ya tabia nchi, Mhe. Rais Samia amesema tayari zipo taarifa za wanasayansi kuwa visiwa vya Zanzibar haviko salama kutokana na kuathirika na mabadiliko ya tabianchi na ni vyema wananchi na Serikali kuliangalia suala hilo ili athari zake zisiwe kubwa zaidi.

Kongamano hilo la kwanza la kumbukizi ya maisha ya Maalim Seif limefanyika chini ya kauli mbiu isemayo “Maalim Seif, Umoja na Maridhiano katika Ujenzi wa Zanzibar na Tanzania Mpya” .
Kongamano hilo limehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar Mhe. Othman Masoud Othman, Rais Mstaafu wa Zanzibar Mhe. Amani Abeid Karume, Waziri Mkuu Mstaafu Jaji Joseph Sinde Warioba, Mjane wa Maalim Seif Bi. Awena Sinani Masoud, viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa, viongozi wa dini pamoja na mabalozi mbalimbali.

Mhe. Rais Samia amerejea Jijini Dodoma akitokea Zanzibar na kupokelewa na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Anthony Mtaka pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia kwenye ufunguzi wa Kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad lililofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza jambo na Bi Awena Sinani Masoud aliyekua mke wa Hayati Maalim Seif Sharif Hamad baada ya kufungua Kongamano la Kumbukizi ya Maisha ya Maalim Seif Sharif Hamad lililofanyika katika ukumbi wa Golden Tulip, Zanzibar. (ZOTE NA IKULU).

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news