Serikali kupitia TANROADS yaja na tiba mbadala kuzuia ajali barabarani

NA MWANDISHI MAALUM

WIZARA ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wakala wa Barabara nchini (TANROADS) wameanza mradi wa majaribio wa kufunga kamera za barabarani katika maeneo ya mkoa wa Pwani na Morogoro pamoja na kusanifu barabara mpya kwa michoro ya kisasa ili kuzuia ajali za mara kwa mara.
Mwenyekiti wa Baraza la Usalama Barabarani ambaye pia ni Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo (Mb) akiweka shada la maua na kuwasha mshumaa katika eneo la kumbukumbu ya ajali iliyoua wanafunzi wa Shule ya Msingi Luck Vincent katika mteremko wa Mlima Rhotia mjini Karatu, Arusha.

Kaimu Mkurugenzi wa Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi (Ujenzi), Mhandisi Kashinde Mussa ameyasema hayo Novemba 27, 2021 katika mahojiano wakati wa kufunga Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani iliyofanyika eneo la mlima Rhotia ilipotokea ajali ya wanafunzi wa Lucky Vincent mwaka 2017.
Kaimu Mkurugenzi Usalama na Mazingira kutoka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, Mhandisi Kashinde Mussa wa kwanza aliyevaa kofia ya bluu pamoja na Meneja Usalama na Mazingira wa TANROADS, Zafarani Madayi aliyevaa kofia nyeusi wakizungumza na wandishi wa habari.

Kashinde ambaye pia alikuwa akizungumzia hoja za Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo (Mb) ambaye katika hotuba yake alisema chanzo cha ajali iliyoua wanafunzi wa Lucky Vincent katika mlima huo ni ukosefu wa alama za barabarani, alisema TANROADS kama wakala wa serikali anayetunza barabara zote kuu nchini imejipanga kupunguza ajali za namna hiyo.

Kwa upande wake, Meneja Usalama na Mazingira wa Wakala wa Barabara nchini (TANROADS), Zafarani Madayi amesema baada ya kuona mafanikio kwenye mradi wa kamera za barabarani kuzuia mwendo kasi kwa mikoa ya Pwani na Morogoro hivi sasa wako kwenye mpango wa kuweka kamera katika barabara zote nchini, lakini pia kuhakiki na kuboresha alama zote za barabarani ili kuepusha ajali.
Zafarani amesema katika maonyesho ya wiki nzima yaliyokuwa yakifanyika katika uwanja wa Shekh Amri Abeid jijini Arusha wadau mbalimbali wameweza kupata elimu ya shughuli za TANROADS katika banda la Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi na kujifunza kazi ambazo zinafanywa na wizara hiyo.

Amesema, wamepokea agizo la Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Khamis Hamza Chilo (Mb) la kushirikiana kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi sahihi ya alama za barabarani na kupunguza ajali na kwamba TANROADS imekuwa ikitekeleza jukumu hilo kila wakati.
Awali akifunga maonyesho hayo katika eneo la Rhotia ambalo ajali iliyoua wanafunzi wa shule ya msingi Lucky Vincent mwaka 2017, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi,Khamis Hamza Chilo (Mb) amewataka wadau mbalimbali wa barabara kushiriki kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara ili kupunguza ajali.

"Ndugu zangu vifo vinapangwa na Mungu lakini ajali hazipangwi na Mungu, Nawaombeni kila mmoja atumie nafasi yake kutoa elimu ya matumizi sahihi ya barabara, Mheshimiwa Rais Samia ameshatoa maagizo na mimi naendelea kusisitiza kila mmoja afanye matumizi sahihi ya barabara,"amesema.

Amewataka mabalozi wa usalama barabarani kushirikiana na kikosi cha usalama barabarani kutoa elimu kwa madereva bodaboda ili kuepusha ajali zinazosababishwa na uendeshaji mbovu usiozingatia matumizi ya alama za barabarani.
Kwa upande wake Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani, SSP Wilbroad Mtafungwa amewataka wadau wa barabara kutafakari vifo vya wanafunzi 30 na walimu wawili wa Shule ya Msingi Lucky Vincent na kuchukua hatua za kudhibiti ajali za barabarani.

"Leo hii wanafunzi hawa hatunao, wamepoteza ndoto walizokuwa nazo na za wazazi wao kwa sababu tu ya dereva mmoja asiyependa kufuata sheria na kanuni za usalama barabarani, Nawaombeni sana tutafakari hili," amesema.
Mei 6, 2017 ndoto za wanafunzi 30 na walimu wawli pamoja na dereva mmoja wa Shule ya Msingi ya Lucky Vincent ya jijini Arusha zilikatizwa ghafla katika ajali ya gari walilokuwa wakisafiria kwenda hifadhini, ambapo walipofika katika eneo la Rhotia kwenye mteremko mkali gari lilipata ajali kutokana na mwendo kasi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news