Serikali yaipongeza One Acre Fund kwa kuwakopesha wakulima pembejeo

NA ELIASA ALLY

WAZIRI wa wa Kilimo Prof. Adolf Mkenda amelipongeza shirika lisilokuwa la kiserikali la One Acre Fund kwa kuwakopesha wakulima pembejeo na kuwapa utaratibu wa kulipa taratibu katika msimu wa kilimo.
Hivi karibuni akiwa katika Halmashauri ya Iringa Vijiji wakati akikabidhi wananchi wa Ugwachanya wapatao 229 ambao wamepata mbolea ya mkopo kutoka One Acre Fund, Waziri Mkenda aliwataka wawekezaji wengine kuiga mfano wa shirika hilo ambalo linawasaidia wananchi.

Aidha, Waziri huyo wa kilimo aliyataka makampuni mengine kuleta mbolea lakini yahakikishe kuwa mbolea hizo wanazozileta zinakuwa na viwango na ubora kwa mkulima.

"Serikali ina mpango wa kuagiza mbolea kutoka nchi za Burundi na Morocco kwa lengo la kupunguza makali ya bei ya mbolea kwa wakulima ambao wataanza msimu wa kilimo tofauti na bei ya sasa ambayo siyo rafiki kwa mkulima,"amesema Waziri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika hilo,Jennifer Lindgren amesema, shirika limewekeza zaidi ya bilioni 18 kwa ajili ya kuwasaidia wakulima kukopa pembejeo na wana mpango wa kutoa elimu ya kulima kilimo cha zao la alizeti.

"One Acre Fund pamoja na kuwekeza katika kuwakopesha wakulima mbolea inajikita katika zao la kilimo cha alizeti katika Mkoa wa Iringa kwa kuwapa elimu wakulima kulima zao la kilimo cha alizeti na mahindi ambapo wataalamu wa shirika wapo maeneo yote,"amesema.

Kwa upande wa wakulima, Robert Lunyiliko amesema mbolea aliyoipata itamsaidia kulima zao la nyanya na mahindi ambapo anategemea kupata gunia 20 kwa ajili ya chakula.

Pia ameiomba Serikali kuwasaidia kupata soko la mahindi,kwani kwa sasa wana mahindi mengi wameyafungia majumbani kutokana na kukosekana kwa soko la maana la kuuzia mazao yao.

Post a Comment

0 Comments