Serikali yasisitiza mchakato wa kupata vazi la Taifa unaendelea

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

WIZARA ya Utamaduni,Sanaa na Michezo imetaja mafanikio ambayo imeyapata katika kipindi cha miaka 60 huku ikidai haijaachana na mchakato wa kupata vazi la Taifa ambapo imewataka watanzania kuendelea kubuni vazi hilo liweje.
Pia,imetenga kiasi cha Shilingi Bilioni 10.5 kwa ajili ya ujenzi wa Vituo vya Michezo katika mikoa ya Dar es Salaam, Geita na Dodoma. (Sports Recreational and Leisure Centers).
Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Paulin Gekul ameyasema hayo Novemba 13, 2021 wakati akiyataja mafanikio ya wizara.

Amesema, Serikali inatambua umuhimu wa vazi la Taifa na ipo katika mchakato wa kuhakikisha linapatikana vazi ambalo limepitia mchakato wa kupigiwa kura na watanzania wote.

“Sisi kama Wizara tunafahamu umuhimu wa vazi la Taifa na mnafahamu mchakato umeanza muda mrefu kidogo na hivi karibuni tulifikia hatua fulani.Kwa sasa watanzania wamepewa nafasi ya kuonesha mavazi yao halafu tutapigia kura ‘then’ tutakuja na vazi letu la Taifa.

“Hatujaliacha bado lipo katika mikono yetu na pia tumekuwa tukielekezwa mara kwa mara na Waziri Mkuu ni maelekezo kwetu tunaenda nayo hatua kwa hatua iko siku tutafikia hitimisho na vazi la Taifa litakuwa limepatikana na watanzania wengi watakuwa wanalifahamu,”amesema.

UTAMADUNI

Amesema tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika kwa sasa Tanzania Bara, kumeshuhudia mafanikio mbalimbali katika Sekta ya Utamaduni nchini ikiwemo kukua kwa fani mbalimbali za Utamaduni zikiwemo Sanaa, Malikale, Makumbusho na Nyaraka.

“Kukua kwa matumizi ya Lugha ya Kiswahili ndani na nje ya nchi. Mwaka 2006 Kiswahili kilipitishwa rasmi kuwa lugha rasmi ya Umoja wa Afrika; mwaka 2019 Kiswahili pia imekuwa lugha rasmi katika Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC),”amesema.

SANAA

Naibu Waziri huyo amesema tangu kupatikana kwa Uhuru wa Tanganyika kwa sasa Tanzania Bara, kumeshuhudia mafanikio mbalimbali katika Sekta ya Sanaa nchini ambayo ni pamoja na kuanzishwa kwa Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) ambapo mwaka 1984 Serikali ilitunga Sheria ya Baraza la Sanaa la Taifa namba 23 ambayo ilianzisha Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA).

“Pamoja na majukumu mengine husajili wasanii, kutoa vibali vya shughuli za sanaa, kuwatetea wasajiliwa wake, kuwatafutia masoko ya kazi zao na kusimamia uanzishwaji wa mashirikisho ya sanaa nchini. Kuwepo kwa Baraza kumeifanya sekta ya sanaa kushamiri hadi kufikia sekta hiyo kuongoza katika ukuaji wa pato la taifa kwa mwaka 2018/2019 kwa asilimia 13.7,”amesema.

Pia katika kipindi hiki, kumeanzishwa Taasisi ya Bodi ya Filamu Tanzania (TFB) ambapo mwaka 1976 Serikali ilianzisha na kuitambua kama Bodi ya Filamu na Michezo ya Kuigiza Tanzania. TFB ilianzishwa kwa Sheria Namba 4 ambayo husimamia masuala yote ya filamu na michezo ya kuigiza.

Vilevile,Wizara inajivunia kuanzishwa kwa mifumo ya kielektroniki ya kusajili wasanii, kutoa vibali na leseni, pamoja na kufuatilia kazi za wasanii kwenye vyombo vya habari na mitandaoni ambapo Baraza la Sanaa la Taifa – BASATA, Bodi ya Filamu Tanzania – BFT na Taasisi ya Hakimiliki Tanzania – COSOTA wamekamilisha mifumo ya kielektroniki. Mifumo hii itatoa huduma zifuatazo kutokea popote duniani.
“Kurasimisha maeneo ya kuoneshea kazi za sanaa nchini; ambapo kwa sasa takribani maeneo 4000 yamerasimishwa;Kuimarisha usajili wa kazi za ubunifu zikiwemo za maandishi, filamu na muziki. Zaidi ya Wasanii 1,668 na kazi 2,132 zilisajiliwa kufikia Desemba 2020,”amesema.

MEDALI 16

Kwa upande wa Sekta ya michezo,Naibu Waziri huyo amesema Tanzania imefanikiwa kupata jumla ya Medali 16 katika michezo mikubwa duniani.

Amesema ni katika michezo ya Olympic (2); Jumuiya ya Madola (7); na Michezo ya Bara la Afrika (7); na kwamba timu zetu zimeshiriki katika michezo mikubwa bila kukosa tangu Nchi ipate uhuru.

WACHEZAJI 28 WA KULIPWA

Mheshimiwa Gekul amesema, Tanzania imefanikiwa kuwa na wachezaji wa kulipwa 54 katika nchi mbalimbali duniani tangu Uhuru.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news