Simba SC: Yanga SC tupisheni kileleni, tunakuja

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Simba SC ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, wamewataka watani wao wajiandae kuwapa nafasi kileleni.

Ni baada ya mtanange wa leo ambao wamefikisha alama 11 na kuchukua nafasi ya pili huku watani wao Yanga SC wakiwa na alama 15, hivyo kuongoza katika kilele cha msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Wamefikia hatua hiyo baada ya kuwalaza Namungo FC 1-0 usiku huu katika mchezo wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara Uwanja wa Benjamin Mkapa uliopo Halmashauri ya Manispaa ya Temeke mkoani Dar es Salaam.

Kagere aliyeingia dakika ya 72 kuchukua nafasi ya Nahodha, John Raphael Bocco, alifunga bao hilo akimalizia pasi ya beki wa kushoto, Mohammed Hussein‘Tshabalala’.

Namungo FC ilimaliza pungufu baada ya kiungo wake Mzanzibari, Abdul Aziz Makame kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 42 kwa kumchezea rafu.

Simba inafikisha pointi 11 na kupanda nafasi ya pili ikiwa inazidiwa pointi nne na vinara, Yanga SC baada ya wote kucheza mechi tano.Aidha,Namungo FC inabaki na alama zake tano za mechi tano pia.

Awali Coastal Union imelazimishwa sare ya 0-0 na Tanzania Prisons Uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga kama ilivyokuwa kwa Biashara United na Mbeya City Uwanja wa Karume, Musoma mkoani Mara.

Biashara sasa ina alama sita, Coastal alama nne, Mbeya City alama saba na Prisons pointi mbili baada ya wote kucheza mechi tano pia.

Post a Comment

0 Comments