TMA:Kutakuwepo ongezeko la joto kali nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imesema kuna ongezeko la joto katika maeneo mengi hapa nchini, kutokana na kusogea kwa jua la utosi ambapo ongezeko hilo linakwenda sambamba na upungufu wa mvua katika maeneo mengi ya nchi yetu kama ilivyotabiriwa awali.
Meneja wa Kituo Kikuu cha Utabiri TMA, Samwel Mbuya amesema kuwa, hapa nchini, vipindi vya jua la utosi hufikia kilele mwishoni mwa mwezi Novemba wakati jua la utosi likiwa linaelekea Kusini (Tropiki ya Kaprikoni).

“Na hali hiyo hujirudia tena Februari wakati jua la utosi likiwa linaelekea Kaskazini (Tropiki ya Kansa),jua la utosi huambatana na hali ya joto kali kwa sababu uso wa dunia katika eneo tajwa huwa karibu zaidi na jua kuliko maeneo mengine”amesema.

Mbuya amesema kuwa hali ya joto kali hujitokeza zaidi kunapokuwa na upungufu wa mvua kama ilivyo katika kipindi hiki.

“Katika kipindi hiki viwango vya joto vilivyoripotiwa katika maeneo mbalimbali ni vikubwa ambapo Mkoa wa Kilimanjaro uliripoti kiwango cha juu cha joto kilichofikia nyuzi joto 36.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.6 ukilinganisha na wastani wa muda mrefu kwa Novemba,”amesema.

Ameongeza kuwa, kiwango cha juu cha joto katika Mkoa wa Dar es salaam kimefikia nyuzi joto 33.8 sawa na ongezeko la nyuzi joto 2.2 wakati katika Mkoa wa Ruvuma kimefikia nyuzi joto 34.4 sawa na ongezeko la nyuzi joto 4.3.

“Hali kama hii imejitokeza pia katika mikoa yote nchini ambapo kiwango cha joto kimekuwa kikubwa kuliko wastani wa muda mrefu,”amesema.

Mbuya amesema, vipindi vya joto kali vinatarajiwa kuendelea kujitokeza Novemba, 2021 na kupungua kidogo ifikapo Disemba, 2021 ambapo mtawanyiko wa mvua unatarajiwa kuongezeka sambamba na mionzi ya jua la utosi kuwa imeondoka katika maeneo ya nchi.

“Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania inaendelea kutoa wito kwa wananchi kufuatilia taarifa za mwenendo wa hali ya hewa zinazotolewa pamoja na kutafuta, kupata na kutumia ushauri wa wataalamu wa kisekta ili kujiepusha na madhara yanayoweza kusababishwa na hali mbaya ya hewa ikiwemo joto kali,”amesema Mbuya.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news