Tumaini Letu wamshukuru Diwani wa Magomeni kwa kuwaunga mkono

NA ANNETH KAGENDA

KIKUNDI cha Tumaini Letu cha Watu wenye Ulemavu wa viungo mbalimbali kimetoa pongezi za dhati kwa Diwani wa Kata ya Magomeni, Noordin Butembo kwa kuwaunga mkono pamoja na kuwatafutia misaada mbalimbali kwa kushirikiana na Manispaa ya Kinondoni.
Kadhalika, kikundi hicho kimewaomba wadau, makampuni pamoja na taasisi zingine mbalimbali kuendelea kujitokeza kukisaidia kwa madai kuwa kinayo malengo makubwa ya kufanya vitu vya maendeleo kwa ajili ya watu wenye ulemavu.

Wakizungumza na DIRAMAKINI Blog kwa nyakati tofauti jijini Dar es Salaam jana, viongozi wa kikundi cha Tumaini Letu mmoja wapo akiwa ni Mjumbe Msabila Kanyenye akiwa nyumbani kwao Magomeni Makuti 'B' amesema, wanampongeza Diwani Butembo kwa kuwathamini na kwamba awali kikundi chake kilipata mkopo kutoka Manispaa.

"Mkopo huu ulitusaidia kununua bajaji mbili lakini kumbuka sisi ni kikundi cha watu watano hivyo bajaji mbili hazitutosha kwani kila mtu anatakiwa awe na ya kwake ili kwa pamoja tuweze kukusanya fedha na kulipa mkopo tuliopewa, lakini pia hata matumizi yetu tunayaangalia hapo hapo," amesema Kanyenye.

Amesema kutokana na hali hiyo japokuwa wanaenda vizuri lakini si kwa kasi inayohitajika kutokana na kwamba ela inayohitajika kurejeshwa ni nyingi wanaomba hata wadau wengine kujitokeza kuwashika mkono ili waweze kusonga mbele na kufanya miradi mingine midogo ya kuwaingizia kipato.
Mhazini wa Kikundi hicho Hamad Suleiman Feruz, amesema kikundi chake kinajitahidi kukusanya fedha ili kianze kulipa rejesho japokuwa rejesho ni kubwa ambapo mkopo waliopewa ni sh. Milioni 16 ambazo walifanikiwa kununua bajaji mbili na kwamba rejesho la kila mwezi ni milioni 1.3.

"Kwanza tunashukuru uongozi wa Diwani pamoja na Manispaa lakini nipende kusema kuwa, kwa vitendea kazi tulivyonavyo bado ni vidogo kwa ukusanyaji wa fedha japo tunajitahidi hivyo tungeomba kama ingewezekana tukaongezewa mda hata kulipa kwa mwaka mmoja na nusu ingekuwa imetusaidia zaidi," alisema Feruz.

Mwenyekiti wa Kikundi cha Tumaini Letu, Ajuaye Abdallah Kondo, alisema kuwa kikundi chake kilipata usajili tangu mwaka jana na kuanza harakati za kutafuta ufadhiri ili kiweze kufanya shughuli za kujiingizia kipato na kwamba bahati mzuri Diwani Butembo akakisaidia na kuweza kupata mkopo.

"Tunamshukuru Diwani wetu kwenye hili kwakweli alitusaidia kwa kushirikiana na Manispaa yetu ila tunaomba wafadhiri wajitokeze ili wasaidiane naye ili tuweze kuongeza vitendea kazi vingine zaidi lakini pia tunamipango mingine ya kufanya shughuli za kujiingizia kipato ndio maana tunaomba wadau watushike mkono," amesema Mwenyekiti Kondo.

Hata hivyo, alisema kikundi chake kinalenga kuhakikisha kinalipa mkopo huo kwa haraka ili kiweze kumaliza kwa wakati na kuchukua mkopo mwingine ambao kikundi hicho kinaweza kuongeza vitendea kazi vingi zaidi pamoja na kufungua mradi wa sabuni.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news