Vijana wenye fani ya ufundi watakiwa kuchangamkia fursa Dodoma

NA DOREEN ALOYCE

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka amesema Serikali katika kutambua umuhimu wa mafundi,amewataka vijana wenye fani ya ufundi kuchangamkia fursa ya kujenga vyumba vya madarasa jijini hapa vyenye thamani ya shilingi bilioni 14.
Mheshimiwa Mtaka amesema kuwa, fedha hizo zilizotolewa na Serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kupitia Mpango wa Matumizi ya fedha za Mapambano dhidi ya UVIKO-19 kutoka Shirika la Fedha Duniani (IMF).

Kauli hiyo ameitoa Jijini hapa wakati alipokuwa Mgeni Rasmi kwenye Mahafali ya 36 ya Chuo cha Ufundi stadi Donbosco kilichopo nje kidogo na Jiji la Dodoma ambapo aliwatunuku vyeti wahitimu 150 ngazi ya cheti na stashahada (Diploma) fani mbalimbali.
 
Mtaka amesema kuwa, Serikali inatoa kipaumbele kwa vijana wenye ujuzi mbalimbali ikiwemo ufundi ili waweze kunufaika na fedha hizo kama Serikali inavyoelekeza hivyo na kuutaka uongozi wa chuo hicho kuwasilisha majina ya wahitimu ofisini kwake ili waweze kutafutiwa fursa hizo.

"Kwenye mpango wa Serikali ni kuhakikisha inajali vijana na hii, nchi ina changamoto ya mafundi japo ajira zipo, lakini tatizo linakuja kwa vijana wenyewe hawajitambui wanapopelekwa kwenye soko la ajira wanaanza kuiba vifaa,na kuonyesha tabia mbaya mpaka kupelekea kufukuzwa, sasa hivi tunajenga vyumba vya madarasa hapa Dodoma vyenye thamani ya shilingi bilioni 14 niwatake mkachangamkie fursa,"amesema Mtaka.
Katika hatua nyingine ameutaka uongozi wa chuo hicho kuwa wabunifu,kuwa na ushindani katika soko la ajira ambapo wanapaswa kuanzisha kampuni tanzu ya kufanya shughuli nyingi kutokana na fani walizonazo ili chuo hicho kiwe kitovu cha kuzalisha malighafi mbalimbali badala ya kuagiza nje ya mkoa.

"Tunataka Donbosco shindani ambayo itakuwa na kampuni tanzu ya kufanya shughuli nyingi unakuta mafundi wazuri wanatoka Dar es Salaam, tunataka vijana wakitoka hapa chuoni wawe chachu kwenye jamii wakienda kwenye kampuni wanaaminika na kwenda kufanya kazi kwenye majengo makubwa,"amesema.
 
"Lazima muwe na uso wa kazi, mfungue kampuni zinahusiana na fani zenu mnazofundisha mtapata masoko,tenda nyingi na kuongeza kipato cha chuo na Taifa kwa ujumla huku tukiangalia namna ya kusapoti vijana wenye ujuzi, lakini hawana uwezo," amesema Mtaka.
Kwa upande wake mkuu wa Chuo cha Ufundi Stadi Donbosco, Padri Boniphace Chami amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa chuo hicho mwaka 1982 kililenga zaidi vijana wasiokuwa na uwezo wa kuendelea na vyuo ambapo walianza na fani nne lakini mpaka sasa imefikia fani 12 ikiwemo fani ya kilimo.

Aidha amesema kuwa chuo kimekuwa kikiwasaidia vijana kitaaluma kwa kuwatafutia ajira,kukuza karama za michezo,mziki kuwakuza kimalezi na kiimani huku wakipata elimu ya ziada ili waweze kujieleza.

"Tumejenga mahusiano (uhusiano mzuri) mazuri kati ya vyuo vya ufundi stadi VETA,kwa kuwaunganisha wanachuo kupitia soko la ajira, kuzalisha umeme wa sola ambapo tuna kilowatt 34 na kusaidia chuo kupunguza gharama za umeme,na tumeanzisha fani ya kilimo ili kuwasaidia vijana wasiwe legelege na kukuza kiwango cha kujitegemea katika kilimo,"amesema Padri Boniphace.

Padri Boniphace amesema kuwa licha ya mafanikio hayo bado kuna changamoto ya mila na desturi mbovu kwa jamii juu ya mtoto wa kike kusomea fani za ufundi kwa madai kuwa ni kazi ya wanaume na kupelekea wazazi kutowajibika ipasavyo.
Hata hivyo amesema chuo kina mkakati wa kujenga mabweni ya wasichana ambao watalala hapo ili wapate muda mwingi wa kujisomea jambo ambalo litasaidia kuondoa dhana potofu kwamba mtoto wa kike hawezi kusomea ufundi.

Kwa upande wao wahitimu wameieleza DIRAMAKINI BLOG kuwa, elimu waliyoipata inaenda kuleta matokeo chanya kwa jamii kwa kutatua changamoto mbalimbali.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news