Waziri Mkuu:Rais Samia ana nia ya kuwaletea maendeleo

NA MWANDISHI MAALUM

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ana nia thabiti ya kuwatumikia Watanzania na kuendelea kuleta maendeleo nchini kote hususani maeneo ya vijijini.

Amesema kuwa Serikali inapeleka miradi mbalimbali ya maendeleo kwa ajili ya kuwanufaisha wananchi wote bila ya ubaguzi wa aina yoyote ikiwemo ya ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji, elimu na afya.

Ameyasema hayo Novemba 23, 2021 wakati akizungumza kwa nyakati tofauti na wananchi wa vijiji vya Lipande, Narungombe, Machang’anja na Namgurugayi akiwa katika ziara ya kikazi wilayani Ruangwa.

Akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa daraja la Mto Mbwemkuru linalounganisha wilaya ya Ruangwa na Liwale wenye thamani ya shilingi bilioni nne amesema mradi huo utapunguza adha ya usafiri katika maeneo hayo.

“Awali wananchi wa maeneo hayo walikuwa wanapata adha kubwa hasa kipindi cha masika ambapo walitumia mitumbwi na madumu kuvuka kutoka upande mmoja kwenda mwingine.”
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipata maelezo kutoka kwa Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (TARURA) wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, Mhandisi Mashaka Nalupi kuhusu ujenzi wa daraja la mto Mbwemkuru litakalounganisha wilaya za Ruangwa na Liwale mkoani Lindi, Novemba 23, 2021. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Naye, Meneja wa TARURA wilaya ya Ruangwa Mhandisi Mashaka Nalupi amesema mradi huo ulianza kujengwa Januari 31, 2020 na unatarajiwa kukamilika Desemba 31, 2021 ambapo kwa sasa umefikia asilimia 54.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezengumza na wananchi wa kata Narungombe baada ya kukagua ujenzi wa kituo cha Afya cha kata hiyo, ambapo amesema ameridhishwa na ubora wake kwani umeendana na thamani ya fedha iliyoyolewa.

“Msisitizo wa Mheshimiwa Rais Samia kwenye ujenzi wa miradi ya Serikali ni ubora, kamati zote zilizopewa mamlaka ya kusimamia miradi hii ni lazima wajiridhishe na viwango vya ubora wake ili iendane na thamani ya fedha zilizotoka”

Aidha, Waziri Mkuu amesema kuwa Mheshimiwa Rais Samia ametoa fedha nyingi kwa ajili ya sekta ya elimu hivyo wazazi kote nchini wahakikishe watoto wote wenye umri wa kuanzia miaka minne wanakwenda shule. “Mzazi usikubali mtoto wako amefika miaka minne hadi mitano halafu anakaa nyumbani, msiwatumikishe watoto kwenye biashara wapelekeni shule.”

Pia, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito kwa Watanzania kutofanya shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji. “Lindeni vyanzo vyetu vya maji, msiruhusu watu walime kwenye vyanzo kuweni walinzi wa maeneo hayo.”

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news