Wito wa Makamu wa Rais Dkt.Mpango kwa Mahakama

NA MWANDISHI MAALUM

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, Novemba 4,2021amefungua Mjadala wa Tano wa Umoja wa Afrika unaohusu Mahakama. 

Ufunguzi uliofanyika katika Ukumbi wa Kimataifa wa mikutano wa Julius Nyerere Dar es Salaam. 

Mjadala huo umebeba dhima ya kujenga imani ya wananchi kwa mhimili wa Mahakama Barani Afrika.
Akizungumza katika ufunguzi huo, Makamu wa Rais amesema ni muhimu kwa Mahakama za Afrika kufahamu sababu zinazopelekea wananchi kupoteza imani na mahakama hizo ili kuzifanyia kazi na kuziondoa sababu hizo. 

Amesema, wananchi wamekuwa wakikutana na changamoto mbalimbali wakati wa kutafuta haki zao katika mahakama ikiwemo ucheleweshaji wa hukumu, kutumika kwa lugha za kigeni katika utoaji hukumu, kuchelewa kwa utekelezaji wa hukumu halali za Mahakama pamoja na kukosa haki zao kutokana na uelewa mdogo wa sheria.

Makamu wa Rais amesema, katika kuongeza Imani kwa wananchi mahakama zinapaswa kuweka mkazo katika kudhibiti rushwa ili kutoa usawa kwa wananchi wote kupata haki zao, kuongeza matumizi ya Tehama katika shughuli za mahakama zitakazoongeza uwazi na urahisi wa Mahakama kufikika pamoja na kusimamia uhuru wa mahakama hizo ikiwemo kuondoa upendeleo katika utoaji haki. 

Amesema, ni muhimu mjadala unaofanyika ukatafuta suluhu ya hayo yote pamoja na kutoa mapendekezo sahihi na uelekeo wa Mahakama.Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango akikabidhiwa zawadi na Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud mara baada ya ufunguzi wa Mjadala wa Tano wa Umoja wa Afrika unaohusu Mahakama, Novemba 4,2021.

Makamu wa Rais ameongeza kwamba, Tanzania haijajitoa katika Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu bali imejiondoa katika tamko lililofanywa chini ya ibara ya 34 (6) ya itifaki ya uanzishwaji wa Mahakama hiyo inayoruhusu mashirika yasio ya kiserikali pamoja na watu binafsi kuishitaki serikali katika mahakama hiyo. Amesema Tanzania itaendelea kushirikiana vema na mahakama za Afrika kwa kutambua kwamba Afrika inahitaji vyombo vyake vya utoaji haki katika kutatua changamoto za waafrika.

Kwa upande wake Rais wa Mahakama ya Afrika ya Haki za Binadamu na Watu, Jaji Imani Aboud amesema kuongezwa kwa ufanisi katika utaoaji haki katika mahakama za ndani kwa nchi wanachama wa mahakama ya Afrika kutapunguza mrundikano wa kesi katika mahakama hiyo na kuongeza kwamba mjadala huo wa siku mbili unaofanyika hapa nchini utakua na maana zaidi kama utaongeza ufanisi wa utaoaji haki pamoja na kulinda haki za binadamu katika mahakama za ndani ya nchi.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Philip Isdor Mpango akiwasili katika ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere Jijini Dar es salaam katika ufunguzi wa Mjadala wa Tano wa Umoja wa Afrika unaohusu Mahakama. Novemba 4,2021.

Akizungumza kwa niaba ya Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji wa mahakama kuu ya Tanzania Dkt. Deo Nangela, amesema katika nchi yeyote Imani kwa mahakama inaongeza Amani na utulivu katika nchi ambavyo upelekea maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Amesema uchaguzi wa dhima katika Mjadala wa Tano wa Umoja wa Afrika unaohusu Mahakama unaonesha nia ya dhati ya mahakama ya Afrika katika kuboresha Maisha ya waafrika na uchumi wao.

Amesema, Tanzania imeendelea kuboresha mifumo ya Tehama katika utoaji haki na kuongeza kwamba umuhimu wa matumizi ya Tehama katika shughuli za mahakama unazidi kuonekana hasa wakati huu wa mlipuko wa Uviko 19 ambapo wananchi wanahitaji kuendelea kupata haki zao katika mahakama hizo licha ya uwepo wa ugonjwa huo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news