Wizara yatoa maagizo kwa wamiliki wa ardhi nchini

NA MUNIR SHEMWETA-WANMM

NAIBU Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula amewataka wamiliki wa ardhi nchini kuhuisha miliki zao zilizoisha muda wake ili kuepuka kufutiwa ardhi wanayomiliki kwa mujibu wa sheria.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza na Mkuu wa mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge (Kushoto) na Katibu Tawala wa mkoa huo, Profesa Faustine Kamuzora wakati wa ziara yake ya kikazi ya siku mbili mkoani Kagera Novemba 22, 2021. (Picha zote na Munir Shemweta-WANMM).

Sheria ya Ardhi Na 4 ya mwaka 1999 inamtaka mmiliki wa ardhi kuhuisha miliki yake baada ya muda wa awali aliopewa kuisha. Mmiliki huyo anatakiwa kuomba kuongezewa muda wa kumiliki ardhi na mamlaka husika inawajibu wa kumuongezea ama kutomuongezea kulingana na masharti ya umiliki ambayo ni pamoja na kufanya maendelezo katika eneo analomiliki.

Akizungumza na watendaji wa sekta ya ardhi pamoja wananchi waliowakabidhi hati za ardhi Novemba 22, 2021 kwenye ukumbi wa Manispaa ya Bukoba, Naibu Waziri Mabula alisema, watendaji wa sekta ya ardhi wanatakiwa kuangalia namna ya bora ya kuwafikia wale wote ambao hati zao za umiliki ardhi zimeisha muda wake.

Akitolea mfano wa Manispaa ya Bukoba, Dkt.Mabula alisema, kuna milIki takribanI 22 katika manispaa hiyo zimeisha muda na wamiliki wake bado hawajajitokeza kuhuisha na kuwataka watendaji wa sekta ya ardhi kwenda eneo hilo kuwakumbusha ili waweze kuhuisha milki zao.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akishiriki uzinduzi wa Anuani za Makazi mkoani Kagera, Novemba 22, 2021. Kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge.

Aidha, Naibu Waziri wa Ardhi Dkt.Mabula aliwataka watendaji wa sekta ya ardhi kuhakikisha wanatoa elimu kwa wamiliki wa ardhi kuhusiana na umuhimu wa kuhuisha milki zao zilizokwisha muda na kufafanua kuwa kutofanya hivyo kutasababisha mmiliki hizo kufutwa.

”Kama umepewa hati ya miaka 33 au 69 halafu muda wake umeimeisha na wengi wenye hati za aina hiyo muda wake ‘umeexpire’ unatakiwa kuihuisha hati na wasipofanya hivyo ardhi unayomiliki anaweza kupatiwa mmiliki mwingine na hatua hiyo inaweza kuleta manung’uniko wakati uamuzi umefanyika kisheria,"amesema Dkt. Mabula.

Hata hivyo, Naibu Waziri Mabula amewataka watendaji wa sekta ya ardhi kutotumia fursa ya kuisha muda wa umiliki kuwanyang’anya wamiliki maeneo yao na badala yake wahakikishe wanatoa elimu ya kuhuisha sambamba na kufuata sheria wakati wa kutekeleza sheria.
Naibu Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Dkt.Angeline Mabula akizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali Charles Mbuge alipowasili mkoani humo kwa ziara ya kikazi ya siku mbili Novemba 22, 2021.

Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Bukoba mkoani Kagera wametaka kuwepo utaratibu wa kuwakumbusha wamiliki ardhi kuhuisha hati zao pale muda wake unapokuwa umeisha ili kuepuka milki hizo kufutwa bila wao kujua.

Diwani wa Kata ya Katerero mkoani Kagera, Bw.Nuru Kabendera mbali na kushukuru ofisi ya Kamishna wa Ardhi Msaidizi mkoa wa Kagera kuwapatia hati katika kipindi kifupi lakini amesema wengi wa wamiliki bado hawajui muda wa kuisha kwa hati na kutaka elimu ya uhuishaji kutolewa hadi yale maeneo ya vijijni ili wamiliki waweze kufahamu.

Naye Mkazi wa Kata ya Bakoba Mtaa wa Nyakanyasi Manispaa ya Bukoba, Bi. Grace Kokuledi amewaasa wamiliki wa ardhi kuwashirikisha watoto wao katika suala zima la umiliki ardhi ili iwe rahisi kwao kuhuisha miliki pale itakapotokea Mungu amewachukua kwa kuwa hati hizo umiliki wake unafikia hadi miaka 99.

Post a Comment

0 Comments