Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA) yatoa onyo kali kwa taasisi zinazoanzisha mifumo ya TEHAMA bila idhini yao

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MENEJA wa Huduma za Sheria Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), ACP Raphael Rutahiwa amezitaka taasisi za umma zinazoanzisha mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) bila idhini ya mamlaka hiyo kuacha mara moja, kwani kufanya hivyo ni kinyume na taratibu zilizoanzishwa na mamlaka.
Kwa nini mamlaka hii?

e-GA inalenga kuboresha uratibu na uwianishaji wa utekelezaji wa jitihada za Serikali mtandao ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa umma kwa kufanya yafuatayo:

>Uimarishaji wa ufuatiliaji na tathmini ya utekelezaji wa jitihada za Serikali Mtandao kwa umma.

>Utoaji wa Viwango na Miongozo mara kwa mara.

>Kujenga uwezo wa taasisi za umma kutumia viwango na miongozo katika hatua za kupanga, kuanzisha na kutekeleza jitihada za serikali mtandao.
ACP Rutahiwa ameyasema hayo Novemba 26,2021 wakati akizungumza na waandishi aa habari jijini Dodoma.

Kiongozi huyo amesema,  taasisi zote za umma zinapotaka kuanzisha mifumo lazima ziwasililiane na mamlaka hiyo mapema.

“Mamlaka inaelekeza taasisi yoyote ya umma isijenge au kuendeleza mradi wa wowote wa TEHAMA bila kupata idhini ya mamlaka,pia inasisitiza kutoa taarifa mara kwa mara kwa mamlaka katika utekelezaji pia sheria inasisitiza kujenga mifumo kwa kutumia wataalam wa ndani,”amesema ACP Rutahiwa.

Pia amesisitiza kutumia wataalam wa ndani katika kuokoa gharama pamoja na kulinda usalama zaidi wa kimfumo.

ACP Rutahiwa ametoa wito kwa taasisi zote za kiserikali kuzingatia Sheria Na.10 ya mwaka 2019 ya Mamlaka ya Serikali Mtandao ambayo inasisitiza kuwa na utayari wa kuweka miundombinu ya TEHAMA pindi zinapoanzisha majengo ili kuepusha gharama zinazoweza kujitokeza baadae.

“Sheria inaelekeza kwamba tunapoelekea TEHAMA inaenda kutumika kila sehemu, hivyo panapokuwa na mpango wa ujenzi wa miundombinu lazima pawepo utayari wa mifumo ya TEHAMA ,kwa kufanya hivyo tunashirikiana na taasisi husika,isiwe kesho kutwa ukitaka kujenga mfumo wa TEHAMA,"amesema ACP Rutahiwa.

e-GA ni taasisi ya umma iliyoanzishwa kwa Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019.

Hii ni taasisi yenye mamlaka ya kuratibu, kusimamia na kukuza jitihada za Serikali Mtandao pamoja na kuhimiza utekelezaji wa Sera, Sheria, Kanuni, Viwango na Miongozo ya Serikali Mtandao kwa taasisi za umma.

Aidha,kuanzishwa kwa mamlaka hii mwaka 2019 kunaendeleza afua za Wakala ya Serikali Mtandao (eGA) na kuchukua sehemu ya mipango yake kwa sababu majukumu ya taasisi hizi yanafanana ingawa yanatofautiana katika mamlaka ya utendaji.

Mamlaka ya Serikali Mtandao ni taasisi iliyoirithi Wakala ya Serikali Mtandao iliyoundwa Aprili 2012 kwa Sheria ya Wakala za Serikali Na. 30 Sura ya 245 ya mwaka 1997 yenye jukumu na Mamlaka ya Kuratibu, Kusimamia na Kukuza Jitihada za Serikali Mtandao nchini Tanzania.

Kabla ya kuanzishwa Wakala ya Serikali Mtandao, matumizi ya TEHAMA Serikalini yalikuwa yanaratibiwa na kusimamiwa na Idara ya Usimamizi wa Mifumo (DMIS) iliyopo Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma ambayo kwa sasa ni Idara ya Huduma za TEHAMA Serikalini (DICTS).

Sheria ya Serikali Mtandao Na. 10 ya mwaka 2019 imeainisha majukumu na mamlaka yanayoiongoza Mamlaka ya Serikali Mtandao katika utekelezaji wa Serikali Mtandao nchini.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news