Yanga SC yashindwa kuonyesha makali yake kwa Namungo FC

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

YANGA SC wamepunguzwa kasi katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara baada ya kutoa sare ya 1-1 na wenyeji, Namungo FC.
Ni katika mtanange uliopigwa leo jioni ya Novemba 20,2021 katika dimba la Ilulu mjini Lindi.

Awali Namungo FC walitangulia kwa bao la mshambuliaji Mzambia, Obrey Chirwa akiifunga timu yake ya zamani dakika ya 53, kabla ya kiungo Saido Ntibanzokiza kumfunga Mrundi mwenzake, kipa Jonathan Nahimana kwa penalti dakika ya 82.

Yanga inafikisha alama 16 na kuendelea kuongoza Ligi Kuu kwa alama mbili zaidi ya mabingwa watetezi, Simba SC baada ya timu zote kucheza mechi sita.

Wakati huo huo Geita Gold wamewachapa wenyeji, Kagera Sugar 2-1 katika dimba la Kaitaba mjini Bukoba.

Mabao ya Geita Gold yamefungwa na George Mpole yote dakika ya kwanza na 35, wakati la Kagera limefungwa na Mbaraka Yussuf dakika ya 11.

Kwa matokeo hayo, Geita Gold inafikisha alama tano na kujiinua kidogo kutoka nafasi ya 15 hadi ya 13 kwenye Ligi ya timu 16, wakati Kagera Sugar inabaki na alama zake nane katika nafasi ya sita baada ya wote kucheza mechi sita.

Kwa upande wa Mbeya City imeshinda 3-1 dhidi ya Mtibwa Sugar katika dimba la Sokoine jijini Mbeya.

Mabao ya Mbeya City yamefungwa na Juma Luizio dakika ya 45, Juma Shemvuni dakika ya 60 na Suleiman Ibrahim dakika ya 85, wakati la Mtibwa limefungwa na Salum Kihimbwa dakika ya 82 kwa penalti.

Aidha, kwa ushindi huo, Mbeya City inafikisha alama 10 na kupanda nafasi ya tatu ikiizidi wastani wa mabao tu Polisi Tanzania baada ya wote kucheza mechi sita, wakati Mtibwa inabaki na pointi zake mbili za mechi sita sasa katika nafasi ya 14 kwenye Ligi ya timu 16.

Hata hivyo, Mtibwa inazizidi wastani wa mabao Geita Gold na KMC FC zilizo chini yake mkiani kwenye eneo la kushuka moja kwa moja.

Aidha, ikumbukwe timu zitakazomaliza nafasi ya 13 na 14 zitakwenda kumenyana na timu za Championship kuwania kubaki Ligi Kuu Tanzania Bara.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news