Makala ya Tume ya Utumishi wa Umma kuhusu Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Desemba 9,2021

NA MAGNUS MAHENGE

KATIKA kipindi hiki Serikali, na nchi yetu tupo katika sherehe za Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru wa lililokuwa taifa la Tanganyika tulioupata Desemba 9, 1961 na baadae kuzaliwa kwa taifa liitwalo Tanzania.

Kauli mbiu ya maadhimisho haya ni “Tanzania Imara, kazi iendelee”.Katika miaka 60 ya Uhuru, Tume ya Utumishi wa Umma ni miongoni mwa vyombo vilivyoanzishwa na Serikali ili kusimamia masuala ya uendeshaji wa Rasilimali watu katika Utumishi wa umma.

Tunapoadhimisha sherehe hizi, kupitia makala haya tutaangalia hatua ambazo Tume imepiga tangu nchi yetu ilipopata Uhuru, ilipo, mafanikio na inapoelekea.

Hivi karibuni, Tume ya Utumishi wa Umma kupitia Waziri mwenye dhamana na Utumishi wa Umma nchini, Mheshimiwa Mohamed O. Mchengerwa (Mb) ilitoa taarifa kuhusu mafanikio makubwa ya Serikali kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru.

Baada ya nchi yetu kupata Uhuru, iliendelea kurithi Tume mbalimbali zilizoanzishwa kushughulikia watumishi wa umma nchini, miongoni mwa Tume hizo ni Tume ya Utumishi Serikalini, Tume ya Utumishi wa Walimu na Tume ya Utumishi wa Serikali za Mitaa ambapo chimbuko lake ni Sheria iliyojulikana kama “The Native Authority Ordinance of 1926” na Sheria ya Machifu “The African Chiefs Ordinance of 1953”.

Tangu kipindi hicho, Tume hizi zilikabiliwa na changamoto mbalimbali katika kushughulikia masuala ya kiutumishi katika Utumishi wa Umma.

Miongoni mwa changamoto zilizokuwapo ni kuwepo kwa mifumo ya utawala na uongozi iliyopitwa na wakati, masuala ya ajira yaliyotofautiana, nidhamu na utaratibu wa kupima utendaji kazi wa watumishi usio na malengo yaliyo wazi ili kutambua utendaji mzuri wa kazi na kukosekana kwa mipango madhubuti ya kuwapa motisha watumishi wa Serikali.

Ili kukabiliana na changamoto hizo kupitia maboresho yaliyokuwa yanafanyika Serikalini kuhusu Utumishi wa Umma, yaliwezesha kutungwa kwa Sera ya Menejimenti na Ajira katika Utumishi wa Umma ya mwaka 1999. 

Lengo la Sera hiyo ilikuwa ni kuunganisha Tume tofauti zilizokuwepo na kuunda Tume moja ya Utumishi wa Umma ambayo madhumuni yake ni kuhakikisha kuwa Utumishi wa Umma unakuwa mmoja na watumishi wote wana taratibu za usimamizi, hadhi, haki na maslahi yanayofanana.

Kufuatia hatua hii ya Serikali, Tume zilizokuwepo zilikoma na Tume ya Utumishi wa Umma kuanza kutekeleza majukumu yake mwaka 2004.

Tume ya Utumishi wa Umma ni miongoni mwa Taasisi zilizoandaa taarifa kueleza mafanikio yaliyopatikana katika Tume kuonyesha dhahiri maendeleo yaliyopatikana ya miaka 60 ya Uhuru wa nchi yetu katika usimamizi wa masuala ya Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma.

Akizungumzia zaidi kuhusiana na suala hilo, Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M.Kirama amesema, ili kuipa nguvu ya kisheria Sera hiyo, Serikali ilitunga Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 ambayo iliainisha majukumu ya Tume.

Bwana Kirama, anafafanua kuwa masuala ya msingi yanayoshughulikiwa na Tume ni pamoja na Kushughulikia Rufaa na Malalamiko ya Watumishi; Kuelimisha Wadau jinsi ya kutekeleza Sheria, Kanuni na Taratibu zinazosimamia Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma; Kufanya ukaguzi wa Rasilimali Watu kwa Taasisi zote katika
Utumishi wa Umma; na Kuandaa Taarifa ya Utekelezaji wa Majukumu ya Tume inayowasilishwa kwa Rais na Waziri mwenye dhamana na Utumishi wa Umma na Taarifa za Utekelezaji wa Majukumu ya kila Robo kwa Taasisi za Umma ambazo huwasilishwa kwa Katibu Mkuu Kiongozi.

Mafanikio ya Tume kwa kipindi cha miaka 60 tangu Uhuru

Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Bw. Mathew M. Kirama amefafanua kuwa, tunapoadhimisha miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara, Tume ya Utumishi wa Umma inajivunia mafanikio iliyoyafikia katika kipindi hiki hususan katika maeneo yafuatayo;-

(i) Utumishi wa Umma kusimamiwa chini ya Sheria moja:

Kwa sasa Taasisi na makundi yote ya Watumishi wanashu-ghulikiwa chini Sheria ya Utumishi wa Umma, Sura ya 298 (marejeo ya Mwaka 2019) makundi hayo ya Utumishi ni pamoja na Serikali Kuu, Utumishi wa Serikali za Mitaa, Utumishi wa Afya, Utumishi wa Wakala za Serikali na Utumishi wa Taasisi na Utumishi wa Huduma za Kawaida.

(ii) Kutoa Miongozo ya Kisheria:

Tume imeweza kuandaa kitabu cha rejea na kutoa Miongozo mbalimbali ya Sheria ambayo imekuwa ikitumika kama nyenzo kuwawezesha Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuwa na tafsiri inayofanana katika utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma.

Kitabu cha rejea kinajumuisha Sera, Sheria, Kanuni, Taratibu na Nyaraka mbalimbali kuhusu masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma.

Miongozo inayowezesha Waajiri, Mamlaka za Ajira na Nidhamu kuwa na tafsiri moja ya utekelezaji wa Sheria ya Utumishi wa Umma. Miongozo hiyo ni pamoja na:-

Mwongozo kuhusu uandaaji na uwasilishaji taarifa za masuala ya Kiutumishi Tume ya Utumishi wa Umma Toleo la 1, mwaka 2005;

Mwongozo kuhusu masuala ya Ajira katika Utumishi wa Umma;Toleo la 1, mwaka 2005, Toleo la 2, mwaka 2009;

Mwongozo kuhusu mashauri ya nidhamu na rufaa kwa watumishi wa umma; Toleo na.2, mwaka 2009 (unahuishwa kwa sasa).

Mwongozo kuhusu ukaguzi wa rasilimali watu katika Utumishi wa Umma; Toleo la 1, mwaka 2009;

Mwongozo wa kushughulikia malalamiko katika Utumishi wa Umma;Maelekezo mahsusi kwa Mamlaka za Nidhamu na Kamati za Uchunguzi kuhusu namna ya kuendesha uchunguzi wa mashauri ya nidhamu; Toleo la 1, mwaka 2008.

(iii) Kufanya Ukaguzi wa Rasilimali Watu kwa Waajiri: Tume inaendelea kutekeleza jukumu hili la kufanya Ukaguzi wa Rasilimali Watu kwa Waajiri kuangalia kama wanazingatia Sheria, Kanuni na Taratibu zilizopo katika usimamizi wa Rasilimali Watu wanavyotekeleza majukumu yao. Taarifa za Ukaguzi zinasaidia Serikali kuboresha usimamizi wa Rasilimali Watu katika Utumishi wa Umma kwa kufanya marekebisho ya Sera, Sheria na Kanuni, kutokana na upungufu unaobainika katika ukaguzi.

Maeneo ambayo yanayokaguliwa na Tume ni kuhusu Masuala ya Ajira; Nidhamu; OPRAS; Likizo ya mwaka; Likizo ya ugonjwa; Upandishwaji vyeo na Mafunzo.

(iv) Kupokea na kushughulikia Rufaa na Malalamiko: Tume imeweza kutekeleza jukumu lake la kutoa haki kwa kupokea na kushughulikia rufaa na malalamiko ya Watumishi wa Umma ambao hawakuridhika na uamuzi wa Mamlaka zao za Ajira na Nidhamu Watumishi wanaoshughulikiwa ni makundi ya Utumishi katika Serikali Kuu, Utumishi wa Serikali za Mitaa, Utumishi wa Afya, Utumishi wa Wakala za Serikali na Utumishi wa Taasisi na Utumishi wa Huduma za Kawaida.

(v) Uwezeshaji Wadau katika Utumishi wa Umma: Tume imewawezesha Waajiri, Mamlaka za Ajira na Mamlaka za Nidhamu ili kuweza kutekeleza majukumu yao ipasavyo katika usimamizi wa Rasilimali Watu kupitia Semina na Mikutano ya kazi na Wadau, Ziara za Viongozi, Vipindi vya Redio, Televisheni, Machapisho, Vipeperushi na Tovuti ya Tume.

(vi) Tume ya Utumishi wa Umma imekuwa miongoni mwa Tume za mfano barani Afrika. Tume nyingine zikiwemo Zimbabwe na Afrika Kusini zimekuja Tanzania kujifunza masuala ya usimamizi na uendeshaji wa Rasilimali Watu.

Bw. Kirama anahitimisha kwa kusema kuwa,baada ya Uhuru mwaka 1961, Utumishi katika Sekta ya Umma katika Nyanja mbalimbali ulishikiliwa na wageni.

Hivi sasa, tunapoadhimisha miaka 60 baada ya Uhuru hali imebadilika sana ambapo Utumishi wa Umma sasa unaendeshwa na Watanzania wenyewe katika Nyanja zote ambapo kupitia juhudi zilizofanyika katika awamu zote za Uongozi wa Nchi hii, wataalam katika fani mbalimbali wameandaliwa wakijumuisha Wahandisi, Makandarasi, Walimu na Madaktari wenye sifa na wanaofanya kazi kwa weledi.

Kupitia programu mbalimbali za kuelimisha na kuhamasisha utendaji wenye matokeo kwa watumishi wa umma, Tume imeendelea kutoa wito kwa watumishi wa umma kuheshimu Sheria, kufanya kazi kwa Weledi, Uadilifu na Uzalendo ili kuwezesha Utumishi wa Umma kuwa daraja muhimu la uhusiano mzuri kati ya Serikali na Wananchi wake.

Kwa kufanya hivyo, Kauli Mbiu ya Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya “Kazi iendelee” itakuwa imetekelezwa kwa vitendo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news