Makachero wamdaka mwizi anayetumia vilevi kupitia biscuits, pipi kuwaibia abiria kwenye mabasi

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

JESHI la Polisi mkoani Mara linamshikilia mkazi wa Kijiji cha Rugasha Bukoba Vijijini, Marco Saidi (68) kwa tuhuma za kuwalewesha abiria kwenye mabasi.
Ni mabasi yanayofanya safari zake kati ya Jiji la Mwanza kwenda Musoma mkoani Mara.

Longinus Tibushubwamu ambaye ni Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara amesema kuwa, mtuhumiwa huyo amekamatwa katika kituo cha mabasi wilayani Bunda mkoani hapa baada ya kumywesha abiria mmoja kilevi.

Kamanda Tibishubwamu ameyasema hayo Desemba 7,2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Amesema kuwa, mtu huyo anadaiwa kuwalisha na kuwanywesha abiria dawa za kienyeji zinazojulikana kwa jina la Khabharagata kutoka nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kwa lengo la kuwalewesha abiria na kuwaibia mali zao.

Amesema, mtu huyo akishirikiana na watu wengine watano (bado hawajakamtwa) wamekuwa wakiwanywesha abiria dawa hizo kwa kuziweka kwenye maji au soda na kupaka kwenye biskuti au pipi kisha kuwapa abiria ambao baada ya kunywa ujikuta wamelewa na kupoteza fahamu.

"Walikuwa wanaweka kwenye kinywaji au anapaka kwenye shati lake eneo la mkononi kisha anasubiri abiria akishakaa yeye anapitisha mkono kama anafungua au kufunga dirisha wakati huo mkono wake anauelekeza kwenye pua ya abiria,hivyo abiria anajikuta amevuta hewa baada ya hapo mtu analewa na kupoteza fahamu au anakupa pipi ama biskuti ukila unalewa kisha anaiba na kushuka kabla hajagundulika," amesema Kamanda huyo.

Pia Kamanda huyo amesema kuwa, matukio ya watu kuleweshwa wakiwa kwenye mabasi yalianza kutokea mwishoni mwa mwezi Oktoba,mwaka huu. Huku watu kadhaa wakijikuta wameibiwa na kwamba baadhi yao walilazimika kukimbizwa hospitalini baada ya kukutwa wakiwa kwenye hali mbaya.

Kamanda huyo amesema kuwa, katika maelezo ya awali mtuhumiwa huyo amekiri kufanya vitendo hivyo katika mikoa kadhaa ikiwemo Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma na Dar es salaam huku akisema kuwa kwa sasa makazi yake alihamishia jijini Nairobi huku akija nchini kwa ajili ya kufanya uhalifu huo na kisha kuondoka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news