Miaka 60 ya Uhuru:Miundombinu ya kisasa ni kipaumbele cha Serikali ya Awamu ya Sita


NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan tarehe 5 Desemba, 2021 amefungua rasmi Barabara ya New Bagamoyo sehemu ya Morocco hadi Mwenge yenye urefu wa Kilomita 4.3 kwa ufadhili wa Serikali ya Japan kupitia Shirika lake la Maendeleo la Japan (JICA).
Sherehe za ufunguzi wa barabara hiyo zilizofanyika Kijitonyama ni sehemu ya Wiki ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru ambapo Mhe. Rais Samia anakagua, kuweka Mawe ya Msingi na kufungua baadhi ya Miradi mbalimbali ya maendeleo katika Jiji la Dar es Salaam.

Mhe. Rais Samia amesema ufunguzi wa barabara hiyo ni juhudi za Serikali katika kuboresha na kujenga miundombinu ya barabara katika Jiji la Dar es Salaam, ikiwa ni sehemu ya kupunguza kero ya msongamano wa magari na ajali za barabarani katika Jiji hilo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewataka wananchi kuzingatia sheria ili kupata manufaa yaliyokusudiwa katika kujenga barabara na miundombinu kwa kuepuka kufanya vitendo vitakavyopelekea uharibifu wa miundombinu hiyo.

Pia, Mhe. Rais ameitaka Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi pamoja na Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) kuhakikisha ujenzi na ukarabati wa barabara na madaraja unafanyika kwa viwango vilivyokubaliwa kimkataba ili zidumu kwa muda uliokusudiwa.

Kuhusu Jiji la Dar es Salaam, Mhe. Rais Samia amesema kuwa sura ya Jiji imebadilika kwa kiasi kikubwa ndani ya miaka mitano iliyopita hasa katika miundombinu ya barabara kupitia Mradi wa Uendelezaji wa Jiji la Dar es Salaam (DMDP) kuwezesha mitaa mingi kuwa na barabara za lami huku akitolea mfano Magomeni na Kinondoni.

Mhe. Rais Samia amesema Serikali inaendelea na kuboresha miundombinu mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam na kwa sasa inaangalia uwezekano wa kuboresha eneo la Jangwani ambalo limekuwa kero kwa wananchi hususan kipindi cha mvua.

Vilevile, Mhe. Rais Samia amewakumbusha wananchi kuendelea kupata chanjo dhidi ya UVIKO 19 kutokana na tishio la wimbi la nne la ugonjwa huo ambalo limezikumba nchi mbalimbali duniani.

Kuhusu fedha za mkopo wa Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), Mhe. Rais Samia amesema matumizi ya fedha hizo yanahitaji ufuatiliaji makini na kupitia Wizara ya Fedha na Mipango wameanzisha kitengo cha tathmini na ufatiliaji ili kuhakikisha zinafanya kazi iliyokusudiwa.

Wakati huohuo, Mhe. Rais Samia amewatembelea Mjane wa Baba wa Taifa Mama Maria Nyerere na Mjane wa Hayati Rais Benjamin Mkapa Mama Anna Mkapa, kuwasalimia na kuwajulia hali ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Miaka 60 ya Uhuru.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news