Miaka 60 ya Uhuru:Singida na Vijana, Vijana na Singida, Vijana na Taifa ndiyo nguvu ya maendeleo

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

VIJANA wametakiwa kuenzi miaka 60 ya Uhuru wa Tanzania Bara na miaka 57 ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kuangalia mabadiliko katika nyanja za uchumi,utamaduni na namna ya upatikanaji wa viongozi unavyofanyika hapa nchini.
Akiongea katika kongamano la vijana lililofanyika katika ukumbi wa Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni, Mkuu wa Wilaya ya Iramba, Suleiman Mwenda amesema hali ya uchumi wa taifa umebadilika kwa kiasi kikubwa kabla na baada ya uhuru, hivyo vijana wanatakiwa kujifunza kutokana na mabadiliko hayo.

DC Suleiman akabainisha kwamba katika kipindi cha baada ya uhuru kulikuwa na chuo Kikuu kimoja cha Dar es Salaam ambacho kilichukua wanafunzi wachache hivyo kusababisha waliowengi kukosa fursa ya kupata elimu ya juu, ikilinganishwa na kipindi hiki ambapo vyuo ni vingi.
Amesema, ukizungumzia uhuru wa Tanzania Bara unazungumzia uhuru wa nchi nyingi za kiafrika kwa kuwa Tanzania ilishiriki katika kutafuta ukombozi wa mataifa mengi ya kiafrika yakiwemo Msumbiji, Afrika ya Kusini jambo ambalo vijana wanatakiwa kufahamu hali ya ukarimu ambao umekuwa ni sehemu ya utamaduni wetu.

Aidha, siasa za Tanzania hasa namna ambavyo viongozi wamekuwa wakibadilishwa kwa njia ya chaguzi ambapo mataifa mengi yamekuwa yakishikwa na butwaa hasa kwa kuangalia nchi za jirani na Tanzania ambazo zimekuwa zikiingia kwenye migongano mara kwa mara.
Awali DC huyo alitoa shukrani za dhati kwa wandaaji wa kongamano hilo ambalo linawafungua vijana na kuwafanya kuwa wazalendo na kuwaonesha fursa mbalimbali zinazowazunguka.

DC Mwenda akabainisha umuhimu wa kufanyika kongamano hilo wilayani Manyoni kwa kuwa ilikuwa ni sehemu ya kuwafundisha vijana umuhimu wa Mashujaa waliotokea Manyoni katika mapambano ya kudai uhuru.
Kwa upande wake Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Fredrick Ndahani akaishukuru Serikali kwa kufufua na kuendeleza shirika la ndege nchini na ambapo awali lilikuwa na ndege moja lakini baada ya miaka 60 ya uhuru shirika lina ndege 11.

Ndahani alisema shirika hilo linatoa fursa kwa vijana kufanya biashara ndani na nje ya nchi kwa kwa kuwa miundombinu ya barabara na anga vimeendelezwa kwa kiasi kizuri.
Bwana Ndahani akafafanua kwamba ni jukumu la vijana kulinda miundombinu ya barabara na reli kwa kuwa ndio vitu ambavyo vitawakomboa vijina katika mpango wa usafirishaji wa bidhaa kutoka sehemu moja na kwenda nyingine.

Afisa Vijana huyo akamalizia kwa kusema kwamba mkoa wa Singida unajivunia kuwa na shule nyingi za Sekondari na Msingi ambapo hakuna kijana ambaye ataweza kufaulu akakosa shule alifafanua Ndahani.
Kongamano hilo lilihusisha vijana wajasiriamali, wanafunzi wa shule mbalimbali za wilayani hapo, Maafisa wa Serikali pamoja na umoja wa vijana wa chama cha Mapindizi CCM.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news