Mkoa wa Singida wapokea mbegu 20,000 za Mkonge

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

MKOA wa Singida umepokea mbegu za mkonge miche 20,000 itakayogawiwa kwa wakulima wa wilaya ya Singida Vijijini ikiwa ni mpango wa kuongeza chanzo cha mapato kwa mkoa huo na wananchi kwa ujumla.
Akipokea mbegu hizo leo Desemba 3,2021 kutoka Bodi ya Mkonge Tanzania,Mkuu wa Mkoa  Dkt. Binilith Mahenge amesema, zao la mkonge ni utajiri mwingine ambao umeingia mkoani Singida na wataalamu wamekiri ardhi ya mkoa huo kustawisha mkonge ambao ni mrefu na haushambuliwi na magonjwa.

Amewataka wakulima mkoani hapo kulima mazao yanayovumilia ukame kama alizeti, mtama, mkonge na dengu kwa kuwa kuna uwezekano mkubwa mvua kunyesha chini ya kiwango kwa mwaka huu.
Awali akifungua kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa (RCC), Dkt. Mahenge ametumia muda huo kuwaasa wananchi wote wa Singida kulima mazao yanayovumilia ukame na ya muda mfupi ili kukabiliana na hali ya hewa ya sasa.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Singida Mjini, Mhanddisi Pasikas Muragili amebainisha kwamba uzalishaji wa mkonge unafanyika katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida na unafanyika katika mapalio (mipaka ya mashamba) iliyopandwa mkonge na kuuchakata.

Amesema, wakulima wilayani humo wameanzisha AMCOS inayofahamika kwa jina la Mpipiti katika kijiji cha Mpipiti ambao wana mashine 16 za kuchakata mkonge na kati ya hizo mashine 10 ni za wanachama na sita ni za watu binafsi.

Aidha,  wilaya imeandaa mashamba yenye ukubwa wa ekari 100 ambapo ekari 50 ni kwa ajili ya waanzilishi wa zao hilo na 50 kwa ajili ya wakulima wengine wa wilaya hiyo.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu Bodi ya Mkonge, Saad Kambona wakati akikabidhi mbegu hizo amesema, kuanzia sasa Singida inaingia kwenye mikoa mitatu ya uzalishaji wa mkonge ambayo ni Tanga, Morogoro na Singida.
Amesema, zao la mkonge halina msimu maalum muda wote linastawi hivyo kuwaomba wakulima wa mkoa huo kutumia fursa hiyo hasa wakati huu ambapo mbegu zinagawiwa bure na serikali.

Kambona amesema, matumizi ya zao hilo yamekuwa yakiongezeka kila mwaka ambapo kwa sasa unatumika kutengeneza mbao kwa ajili ya kutengeneza thamani, sukari, nyuzi, kamba na kwenye magari.

Hata hivyo, ameahidi kuleta mbegu 165,000 za mkonge ambazo zitatosheleza katika mashamba yenye ukubwa wa ekari 100 zilizitengwa wilayani singida vijijini.

Post a Comment

0 Comments