Mtanzania Yusuph Kileo aongoza jopo la wataalamu duniani kujadili wimbi kubwa la wahalifu mtandaoni

NA GODFREY NNKO

MTANZANIA ambaye ni mbobezi na Mtaalaamu wa Masuala ya Usalama katika Mitandao na Uchunguzi wa Makosa ya Kidigitali, Bw. Yusuph Kileo ameongoza mjadala maalumu uliojadili changamoto na namna bora ya kukabiliana na wimbi kubwa la wahalifu mtandao duniani.

Ni kupitia Mkutano Mkuu wa Wataalamu wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) barani Afrika wa AfICTA uliokamilika jana.

Katika mjadala huo uliongozwa na Bw.Kileo pamoja na mambo mengine, washiriki wamehimiza zaidi ushirikiano, elimu ya uelewa wa matumizi sahihi ya mitandao, kutumia watu sahihi kukabiliana na wahalifu mtandao na kujikita kwenye kuzuia matatizo ya kihalifu mtandao kabla hayajawa na athari katika jamii na mifumo yetu ya TEHAMA.

Wazungumzaji katika mjadala huo ulioongozwa na Bw. Kileo alikuwa ni Rais wa Chama cha Usajili wa Mtandao nchini Nigeria (NiRA), Muhammed Rudman, Mbunifu Mkuu wa Teknolojia kutoka iPNX, Oluwaseun Oluboyo.TAZAMA MJADALA CHINI
Wengine ni Afisa Mtendaji Mkuu wa WHOGOHOST Ltd, Toba Obaniyi na Deepak Kumar (D3) ambaye ni Mtaalaam wa Masuala ya Usalama katika Mitandao na Uchunguzi wa Makosa ya Kidigitali kutoka nchini India

Imebainika kuwa, uhalifu wa mtandao unaathari kubwa duniani hususani katika Bara la Afrika ambalo katika GDP yake mwaka 2021 iliguswa kwa dola za Marekani bilioni 4.12.

Wataalamu hao wamebainisha kuwa, juhudi za kushughulikia matumizi mabaya na wimbi kubwa la wahalifu mtandao  zimebanwa na rasilimali na ukosefu wa uratibu mzuri ili kuweza kuukabili kwa matokeo bora. Hivyo, wakuu na viongozi wa nchi wanapaswa kuangalia namna bora ya kuwekeza rasilimali za kutosha katika upande huu ili kuweza kuokoa fedha nyingi na maumivu yanayosababishwa na wahalifu mtandaoni.

Uhalifu mtandaoni ni nini?

Wataalam wa masuala ya mtandao wanasema kuwa, ni shughuli yoyote ya uhalifu inayohusisha kompyuta, kifaa cha mtandao au mtandao wenyewe.

Ingawa uhalifu mwingi wa mtandao unafanywa ili kuzalisha faida kwa wahalifu wa mtandao, baadhi ya uhalifu wa mtandaoni ufanya dhidi ya kompyuta au vifaa moja kwa moja ili kuharibu au kuzima mitandao kwa maslahi yao.

Wengine hutumia kompyuta au mitandao kueneza programu hasidi, maelezo haramu, picha au nyenzo nyinginezo ambazo zinatoa taswira mbaya katika jamii.

Baadhi ya uhalifu wa mtandaoni hufanya mambo yote mawili, hulenga kompyuta ili kuambukiza virusi vya kompyuta, ambavyo huenezwa kwa mashine nyingine na wakati mwingine mitandao kwa ujumla.

Tafiti zinaonesha kuwa, athari kuu ya uhalifu wa mtandaoni ni upande wa kifedha. Kwani uhalifu wa mtandaoni unaweza kujumuisha aina nyingi tofauti za shughuli za uhalifu zinazoendeshwa kwa faida, ikiwa ni pamoja na mashambulizi ya 'rasomware', ulaghai wa barua pepe na mtandao, na ulaghai wa utambulisho, pamoja na majaribio ya kuiba akaunti ya fedha, kadi ya mkopo au maelezo mengine ya kadi za malipo.

Wahalifu wa mtandao wanaweza kulenga taarifa za kibinafsi za mtu binafsi au taarifa za shirika kwa wizi na kuziuza kwa gharama kubwa ili kujinufaisha.
Mtaalaamu wa Masuala ya Usalama katika Mitandao na Uchunguzi wa Makosa ya Kidigitali, Bw. Yusuph Kileo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news