Serikali yasitisha uzalishaji wa pombe ya Banana mkoani Kilimanjaro

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

SERIKALI imesitisha uzalishaji wa pombe aina ya Banana inayozalishwa na kiwanda cha Tanbasi Investment kilichoko Wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro baada ya kubainika kushindwa kukidhi viwango vya ubora.

Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Stephen Kagaigai ametangaza kufungwa kwa kiwanda hicho kutokana na ripoti ya Shirika la Viwango Tanzania (TBS).

Kagaigai amefikia uamuzi huo baada ya kupokea taarifa kutoka kwa wataalamu wa TBS.

“Ripoti ya TBS inaonyesha kuwa sampuli za pombe hiyo zilizopelekwa huko hazifai kwa matumizi ya binadamu kutokana na kuongezwa kiwango kikubwa cha kemikali ya Asetic Acid.

“Nilivyokuja Kilimanjaro, niliambiwa na viongozi wa dini kwamba Rombo kuna viwanda vingi vya kutengeneza pombe, ambazo hazina ubora na zinaleta madhara kwa binadamu.

“Nikaelezwa zipo zilizosababisha baadhi yao kupoteza maisha ndio maana nikafanya ziara maalum huko ya kutembelea viwanda hivyo na nilipochukua sampuli katika moja ya viwanda, hayo ndio majibu yake,"amesema.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa, mara nyingi imekuwa vigumu kubaini pombe ambazo hazifai kwa matumizi ya binadamu kutokana na udanganyifu unaotumiwa na baadhi ya watendaji wasio waaminifu.
Amesema, wilaya hiyo imekuwa na matumizi makubwa ya pombe zisizo rasmi ambazo zinachangia kupoteza nguvu kazi ya taifa, ongezeko la matukio ya kihalifu na migogoro ya ndoa.

Akizungumzia zaidi madhara ya pombe hiyo, Meneja wa TBS Kanda ya Kaskazini, Happy Kanyeka, amesema sampuli waliyopokea kutoka kwenye kiwanda hicho imeonyesha pombe hiyo haikidhi kiwango cha ubora.

“Pombe hiyo aina ya Banana inayozalisha kiwandani hapo haitauzwa mpaka pale TBS itakapofanya uchunguzi wa kina, tutaangalia mchakato mzima wa uzalishaji, tutachukua sampuli nyingine tena na kiwanda hicho kitakuja kufunguliwa baada ya kujiridhisha na ubora wake.

“Pia tumekubaliana tutapitia viwanda vyote vinavyozalisha pombe aina hiyo katika mkoa wa Kilimanjaro na mikoa jirani kuangalia kama vinakidhi viwango.

"Ingawa tulifanya ukaguzi Septemba mwaka huu, tutarudia hasa kwenye viwanda vya Banana, tutafanya utafiti kuona madhara yanayowakumba watu wa wilaya ya Rombo yanatokana na nini kinachowekwa kwenye pombe hiyo,"amefafanua.

Amesema, katika sampuli iliyochukuliwa awali imeonyesha uwapo wa asidi (asetic acid) nyingi hali inayopelekea kushindwa kukaa kwa muda uliokusudiwa.

Post a Comment

0 Comments