TANZIA:Mwanahabari mkogwe nchini Tanzania, Rashid Zahoro afariki

NA MWANDISHI MAALUM

MWANAHABARI mkogwe nchini Tanzania, Rashid Zahoro amefariki akiwa huko Chanika jijini Dar es Salaam leo Desemba 3,2021.

Zahoro wakati wa uhai wake alikuwa ni mmoja wa wahariri wa magazeti ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya Uhuru na Mzalendo mpaka umauti ulipomkuta siku ya leo Ijumaa.
Mzee Zahoro alizaliwa mwaka 1966 na amefariki dunia nyumbani kwa Dada yake Chanika jijini Dar es Salaam.

Dada wa marehemu, Asha Zahor, alisema kaka yake amefariki dunia saa tatu asubuhi baada ya kusumbuliwa na maradhi mbalimbali.

Alisema,kabla ya umauti, marehemu Zahoro alikuwa akisumbuliwa na maradhi ya kisukari na shinikizo la damu kwa muda mrefu.

“Amefariki akiwa anaendelea na matibabu,  tulitoka hospitali baada ya  kusumbuliwa kwa maradhi muda mrefu, tukarudi nyumbani ilipofika saa tatu asubuhi alifariki,” alisema kwa majonzi.

Dada huyo wa marehemu alieleza kuwa, msiba  upo Chanika nyumbani  na maziko yatafanyika katika Makaburi ya Kisutu jijini Dar es Salaam saa 10.00 alasiri.

Alieleza kuwa, Zahoro alikuwa ni mtoto wa pili na baada ya mtoto wa kwanza kufariki ndio alikuwa mkubwa wa familia yao yenye watoto tisa kwa Baba na mama mmoja.

Aliongeza kuwa baba wa Zahoro  alishafariki dunia na walibaki na mama mzazi, hivyo Zahoror amefariki akiwa amemwacha mama yake mzazi na nduguze saba.

Zahoro alianza kwa kuandika hadithi katika magazeti ya Uhuru, akiwa mwandishi wa kujitegemea mnamo mwaka   1995 aliajiriwa rasmi na kuanza kuitumikia taasisi hiyo.

Uongozi wa DIRAMAKINI BLOG unawapa pole familia, ndugu, jamaa na marafiki kwa kuondokewa na mpendwa wao. Mwenyenzi Mungu ailaze mahali pema roho ya marehemu. Amen

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news