Wilaya ya Misenyi yakamilisha ujenzi wa madarasa kabla ya muda uliowekwa Desemba 15 na ule wa nyongeza Desemba 31

NA DOREEN ALOYCE

HALMASHAURI ya Wilaya ya Misenyi mkoani Kagera imefanikisha kusimamia kwa ufanisi fedha za miradi ya maendeleo ya UVIKO-19 zilizotolewa na Serikali Kuu,ambapo imeweza kutekeleza asilimia 95 ya miradi 53 ya vyumba vya madarasa ya sekondari kabla ya muda uliowekwa ifikapo Desemba 15,mwaka huu.

Aidha, mafanikio hayo yanakuja ikiwa leo Desemba 10,2021 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa y Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Ummy Mwalimu ameziongezea halmashauri siku 15 ili kukabidhi miradi hiyo ifikapo Desemba 31,2021.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmshauri ya Misenyi,Waziri Kombo ameyasema hayo baada ya ziara yake na wataalamu wa halmshauri hiyo kukagua miradi ambayo inatekelezwa.
Kombo amesema kuwa, halmashauri yake ilipewa Shilingi Bilioni Moja na Milioni 60 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi hiyo ikiwemo ujenzi wa madarasa 53 ya wanafunzi wa kidato cha kwanza watakaoanza kidato cha kwanza mwakani na madarasa 10 ya shule shikizi za msingi.

Amesema, mafanikio hayo ni kutokana na ufuatiliaji wa karibu na wa mara kwa mara ulioenda sambamba na ushirikiano kati ya viongozi wote kuanzia walimu ambao walipewa jukumu la kusimamia mafundi,viongozi wa wilaya,chama mpaka mkoa jambo ambalo limeleta tija kubwa.
Amesema kuwa, uwepo wa madarasa hayo umewapunguzia mzigo wakurugenzi kwani ni jambo ambalo lilikuwa linawatesa kwamba watayajengaje ila kupitia fedha za Serikali itasaidia kuondoa changamoto hiyo na kuwasaidia wanafunzi kusoma bila shida.

‘’Tunamshukuru Rais wetu Samia Suluhu Hassan kwa kutupatia fedha kwa ajili ya miradi hii kwenye halmashauri yetu,tulikuwa hatulali tulifuatilia kwa karibu na kuna wakati tulitumia ukali kwa wasimamizi, lakini lengo lilikuwa ni kutimiza maagizo tuliyopewa na hatimaye leo tumemaliza kabla ya wakati na kwa viwango vya juu,’’amesema Kombo.
Kwa upande wao wataalamu ngazi ya Halmashauri hiyo akiwemo Katibu Kamati ya Ufuatiliaji Miradi ya UVIKO-19,Gozberth Bernard na Mhandisi Lucy Nshoma wamesema kuwa, mradi huo ulikuwa na usimamizi mzuri na wenye viwango bora vilivyotolewa na serikali.
Wakizungumza kwa nyakati fofauti wananchi wa Wilaya ya Misenyi wamesema kuwa, wanaishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa jinsi ilivyoleta maendeleo kwenye jamii hususani madarasa ambayo yatasaidia watoto wao kupata elimu bora.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news