Ajali ya Kidia One yajeruhi, polisi wathibitisha dereva kutimua mbio

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

DEREVA wa basi la abiria aina ya Zhong Tong namba T.355 DTC mali ya Kidia One Express, Evod Lyimo amedaiwa kutimua mbio baada ya basi hilo kupata ajali maeneo ya Kikatiti nje kidogo ya Jiji la Arusha.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, ACP Mary Kipesha amesema, ajali hiyo imetokea leo Januari 31, 2022 majira ya saa 12:40 katika maeneo hayo.

Amesema, ajali hiyo imesababishwa na uzembe wa dereva aliyekuwa akilipita gari lingine bila tahadhari na kulazimika kushika breki za ghafla.

ACP Kipesha amesema, breki alizoshika dereva huyo, Evod Lyimo zilisababisha gari hilo kuserereka katika eneo hilo lenye utelezi na kuanguka.

Amesema, basi hilo ambalo lilikuwa linafanya safari kutoka Arusha kwenda jijini Dar es Salaam baada ya kupinduka lilisababisha majeruhi kwa watu wawili.
"Baada ya ajali hiyo dereva alikimbia na hata hivyo Jeshi la Polisi linaendelea kumtafuta ili aweze kufikishwa mahakamani kwa kosa la kuendesha gari kwa uzembe na kusababisha ajali. Waliojeruhiwa katika ajali hiyo ni Lyidia Clara mwenye umri wa miaka 64 mkazi wa Dar es Salaam na Doreen Kawiche aliyekuwa kondakta mwenye umri wa miaka 27 mkazi wa Arusha.

"Majeruhi hao wamelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Meru kwa ajili ya matibabu na wanaendelea vizuri,"amesema ACP Kipesha.

Aidha, ametoa wito kwa madereva kuchukua tahadhari kubwa pindi wanapotumia vyombo vya moto na kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu za usalama barabarani ili kuepusha madhara ambayo yanaweza kutokea kwa binadamu ikiwa ni pamoja na uharibifu wa vyombo vya moto.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news