CATA MINING yaunga mkono maono ya UWT Mara

NA FRESHA KINASA

JUMUIYA ya Umoja wa Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi Tanzania (UWT) Mkoa wa Mara umepokea msaada wa vyakula ikiwemo mchele kilo 100, maharage kilo 100, pamoja na fedha kiasi cha shilingi 500,000 kutoka kwa Mgodi wa CATA MINING uliopo eneo la Kataryo Wilaya ya Butiama Mkoa wa Mara.
Viongozi wa UWT Mkoa wa Mara wamepokea msaada huo kutoka kwa uongozi wa mgodi huo leo Januari 28, 2022 katika Ofisi za CCM Mkoa wa Mara zilizopo Manispaa ya Musoma. 

Ambapo msaada huo utakabidhiwa Februari 3, 2022 na UWT katika Kituo cha Nyumba Salama kinachotoa hifadhi kwa wasichana waliokimbia ukeketaji na aina nyingine za ukatili wa kijinsia kilichopo Kiabakari Wilaya ya Butiama kinachomilikiwa na Shirika la Hope for Girls and Women in Tanzania katika kuadhimisha miaka 45 tangu kuzaliwa kwa Chama Cha Mapinduzi.
Mwenyekiti wa UWT Mkoa wa Mara, Wegesa Hassan ameupongeza uongozi wa mgodi huo kwa kutoa msaada huo kufuatia ombi walilolitoa kuomba kusaidiwa na mgodi huo ili kuyagusa makundi yenye uhitaji ndani ya jamii katika kuadhimisha miaka 45 tangu kuzaliwa kwa chama hicho. 

Ambapo maadhimisho hayo kitaifa yatafanyikia katika Manispaa ya Musoma Mkoa wa Mara chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa ambaye pia ni Rais wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan.

"Niushukuru Mgodi wa CATA MINING tuliandika barua ya kuomba kusaidiwa ili na sisi tuwasaidie Watoto wenye uhitaji na wao bila kusita wametoa msaada huu. Kama jumuiya ya tutapeleka msaada huu kwa watoto wenye uhitaji, waliokimbia ukatili wa kijinsia katika Kituo cha Nyumba Salama Kiabakari Butiama katika kuadhimisha miaka 45 ya kuzaliwa kwa chama chetu cha mapinduzi,"amesema Hassan.
Naye Mjumbe wa Baraza Kuu la UWT Taifa Mkoa wa Mara, Rhobi Samwelly amesema kuwa jamii inawajibu wa kuendelea kuwajali watoto wenye uhitaji katika jamii pamoja na makundi mengine kwa kuonesha upendo wa hali na mali ili kuzidi kujenga ustawi bora katika jamii.
Rhobi ameongeza kuwa, wadau mbalimbali wanawajibu wa kuunga mkono juhudi za Serikali na Chama Cha Mapinduzi kusukuma mbele gurudumu la maendeleo bila kurudi nyuma hasa kuyawezesha makundi maalum na watu wasiojiweza kupata mahitaji ya msingi sambamba na kushirikiana nao kwa karibu.

Kwa upande wake Afisa Uhusiano wa CATA MINING, John John amesema kuwa, kwa kutambua umuhimu wa makundi yenye uhitaji katika jamii hawakusita kutoa msaada huo baada ya kupokea barua ya kuombwa kusaidia na UWT Mkoa wa Mara kwani ni njia mojawapo wa kuimarisha ustawi bora na uhusiano katika jamii. 
Aidha, amesema kuwa mgodi huo utaendelea kushirikiana vyema na Jumuiya ya UWT Mkoa wa Mara katika nyanja mbalimbali za kimaendeleo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news