Fedha za UVIKO-19,tozo zafanya makubwa nchini, Rais Samia asisitiza lazima nchi ikope kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya wananchi, orodha ya wateule wapya kutoka karibuni

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema lazima nchi ikope kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo nchini.
Ameyasema hayo leo Januari 4,2022  Ikulu jijini Dar es Salaam wakati wa kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19.

Mheshimiwa Rais Samia amesema, kuna mahitaji ya madarasa mengi katika sekta ya elimu, ambayo kwa kutegemea fedha za tozo itachukua muda mrefu kukamilisha mahitaji hayo.

"Lakini ndugu zangu tulichopata hapa leo zaidi ya fedha hizi za UVIKO-19, kuna fedha ya tozo ambayo na yenyewe ilipoanza ilipigiwa kelele, tukasema ngoja tupunguze, tukapunguza, baada ya kupunguza kelele zimeshuka,wapigaji kelele hao wa sasa hivi waliuliza kuna fedha ya tozo? Kwa nini tunakwenda kukopa,”amesema Rais Samia.

Pia amesema mpaka sasa fedha zilizopatikana kwenye tozo zimejenga madarasa 5,000 lakini uhitaji wake ni zaidi ya madarasa 10,000 kwa shule za msingi pekee.

"Takwimu zilizotolewa na mawaziri hapa zinatosheleza kwamba pamoja na kwamba tuna fedha za tozo mahitaji ya madarasa shule za msingi ni 10,000 mpaka sasa hivi, tumeweza madarasa 5,000 kwa fedha za tozo, tunafika lini? Amehoji Rais Samia na kusisitiza lazima tukope tuweke miundombinu bora na imara.

Rais Samia  amesema,kuna uhitaji mkubwa wa madarasa kwa siku zijazo ambapo mwaka huu kuna watoto 900,000 na mwakani itakuwa zaidi ya milioni moja, hivyo kutegemea fedha ya tozo itachelewesha kufikia malengo kwa wakati

"Kwa hiyo inashangaza kuona mtu mwenye uelewa anasema kuna fedha ya tozo, lakini kaenda kukopa ya nini au kwa nini tunaendelea kutoza tozo wakati fedha ya mkopo ipo,” amesema Rais Samia.

Wakati huo huo, Rais Samia ameeleza kushangazwa na kauli za Spika wa Bunge,Job Ndugai kusimama hadharani na kukosoa mkopo wa shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wenye lengo la kuchochea mapambano dhidi ya UVIKO -19 wakati taarifa mbalimbali zinapitia kwenye Bunge lake.

Amesema, kinachosumbua sasa ni homa ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.

"Tuna Serikali ya kukopa kopa tangu uhuru,tumekopa kopa na maendeleo tuliyopata yanatokana na kukopa kopa...kukopa siyo kioja. Tutakopa mikopo isiyo na riba ili tupate maendeleo.

"Mtu na akili yake anasimama na anahoji kuhusu mikopo na tozo, sio lolote ni homa ya 2025, kwa mtu ambaye nilimtegemea kushirikiana naye kwenye maendeleo, sikutegemea kama angesimama na kusema maneno hayo. Huwezi kufikiria mtu mliyemuamini, mshika mhimili, aende akasimame aseme yale. Ni stress ya 2025.
"Kinachotokea sasa ni 2025 fever, wasameheni,haya ninayofanya sasa sifanyi kwa ajili ya mwaka 2025, nafanya kwa ajili ya maendeleo ya nchi.Tunachotazama sasa ni maendeleo kwa watanzania... kelele za wanaopiga kelele hazinisumbui mimi sivunjiki moyo, mimi nina moyo wangu, moyo wangu siyo wa glasi,ni wa nyama ulioumbwa na Mungu, hivyo sivunjiki moyo,nishikeni mkono twende sote.

"Nilipopewa mamlaka haya kuna mtu alikuja na kunipa pole na hongera akasema mtu atakayekusumbua kwenye kazi hii ni mtu mwenye shati la kijani mwenzako siyo wa upinzani na hili wanalotazama sasa ni la 2025 na ndicho ninachokiona.

"Wakati mmenikabidhi huu mzigo, nilianza kusikia lugha zinasema Serikali ya mpito, serikali ya mpito bungeni huko kwa kina Kassim. Nikarudi kwenye Katiba kuangalia serikali ya mpito imeandikwa wapi...sikuona. Nikasema ...anhaa., twendeni,"amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Mabadiliko

Pia amesema  hivi karibuni atafanya mabadiliko ya viongozi mbalimbali wakiwemo mawaziri, makatibu wakuu na wakuu wa mikoa.

"Wakuu wa mikoa nimekuwekeni nikiamini kule nilikowakasimia madaraka mtakwenda kusimamia kazi na wengine wote wakiwemo makatibu wakuu na mawaziri.

"Nataka niwaambie nitatoa lists (orodha) mpya ya mawaziri hivi karibuni, wale wanaotaka kwenda na mimi nitaenda nao ila wale wanaotumika nitawapa nafasi wakatumike huko nje wanapopataka. Wale ninaohisi wanaweza kwenda na mimi…nitakwenda nao. 

"Lakini wale wote ninaohisi ndoto zao ni kule, na wanafanya kazi kwa ajili ya kule, nitawapa nafasi waende wakajitayarishe vizuri huko nje,"amesema Rais Samia.

Waziri Ummy

Naye Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema kuwa,wanamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwani ndani ya kipindi kifupi ameacha alama kubwa katika maisha ya watanzania hususani watanzania wa vijijini wazee, vijana na akina mama.

"Nikishukuru Chama Cha Mapinduzi, Katibu Mkuu na wenyeviti wa mikoa chini ya usimamizi wa Mwenyekiti wa Chama Taifa Rais Samia tumeona ndani ya miezi hii miwili wamekuwa wakikagua miradi hii ya madarasa na kufanya usimamizi mzuri.Pamoja na fedha nyingi unazotupatia tutasimamia kikamilifu mapato ya halmashauri zetu na tumeelekeza fedha zinazokusanywa zielekezwe kwenye kutatua kero za wananchi,"amefafanua Waziri Ummy.

Waziri Ummy amefafanua kuwa, Rais Samia ameandika historia hapa nchini kwani watoto wote wataanza shule siku moja jambo ambalo haijawahi kutokea. 

"Mikoa iliyoongoza kwa kupokea fedha nyingi ni Mwanza, Dar es Salaam, Kagera, Morogoro. Shule Shikizi,mikoa iliyopata fedha nyingi ni Singida, Tabora, Tanga, Katavi na Dodoma. Hii ni hatua kubwa,"amesema.

Waziri Ummy amemuomba, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kutokata tamaa kwenye kutafuta fedha za kutatua matatizo ya watanzania maana mahitaji bado ni makubwa.

Kwa upande wa tozo, Waziri Ummy amesema, shilingi bilioni 7 wamezielekeza katika Elimu Msingi.

"Tumejenga madarasa 560 ili kuwaunga mkono wananchi maeneo mbalimbali waliojitoa kujenga madarasa haya.

"Pia tunajenga vituo vya afya 233 katika halmashauri zetu zote Tanzania Bara, tarafa 207 hazikuwa na vituo vya afya, kupitia tozo za makusanyo ya ndani ujenzi wa hivi vituo unaendelea vizuri na upo katika hatua ya ukamilishaji.

"Magari kwa halmashauri zote 184 kwa ajili ya kusimamia huduma za afya na huduma mbalimbali kwenye hospitali zetu.Kwa mara ya kwanza tunakwenda kuweka nyumba za watumishi kwa mpigo halmashauri 150 na huduma za makazi kwa watumishi 450,"amesema.

Waziri Ummy amesema,kwa upande wa Sekta ya Elimu Msingi wamepokea fedha kujenga mabweni 50 kwenye shule za Mahitaji Maalumu.

"Watoto wengi wenye ulemavu walikuwa wanakaa nyumbani, mabweni haya yanaenda kusaidia watoto wetu hawa kusoma kwenye mazingira mazuri.

"Shilingi bilioni 60 ujenzi wa madarasa ya shule shikizi za shule za msingi na shilingi bilioni 4 ni kwa ajili ya ujenzi wa mabweni 50 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalumu,"amesema Waziri Ummy.

Wakati huo huo, Waziri Ummy amesema,hakuna jimbo ambalo limekosa fedha chini ya shilingi bilioni mbilie kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo, majimbo yote 214 yamenufaika.

"Ofisi ya Rais-TAMISEMI ilipokea jumla ya shilingi bilioni 512 ambapo shilingi bilioni 240 ni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 12,000 ya shule za sekondari.Mpaka Disemba 31, 2021 kwa upande wa Sekta ya Elimu msingi, tumepokea shilingi bilioni 304 zote zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa madarasa ya sekondari na shule shikizi pamoja na mabweni.

"Kwa upande wa huduma za afya msingi, TAMISEMI imetengewa shilingi bilioni 203.1 na tuna shilingi bilioni 5 kwa ajili ya kuboresha na kuimarisha mazingira ya kufanyia biashara kwa wafanyabiashara wadogo.Nitumie fursa hii kukutaarifu kwamba ujenzi wa madarasa 15,000 umekamilka kwa asilimia 95 katika mikoa yote Tanzania Bara,"amesema.

Amesema,utekelezaji wa kazi za ujenzi na matengenezo unaendelea vyema ambapo ujenzi na matengenezo ya kawaida ya barabara yaliyofanyika katika kipindi hiki ni makubwa.

"Ujenzi wa barabara kwa kiwango cha changarawe kilomita 2,951.25, ujenzi wa lami kilomita 58.12 pamoja na ujenzi wa madaraja 35 na makalvati 799.

"Pia jumla ya shilingi bilioni 58.25 zimetolewa kwa ajili ya ujenzi wa vituo 233 vya afya katika tarafa 207 ambazo hazina vituo vya afya zenye uwezo wa kutoa huduma za upasuaji na vituo vya Afya 26 katika kata za kimkakati,"amefafanua Waziri Ummy.

Waziri wa Fedha

Kwa upande wake,Waziri wa Fedha na Mipango,Dkt. Mwigulu Nchemba amesema deni la Taifa ni himilivu.

Amesema, kutokana na tathimini iliyofanyika mwezi Novemba mwaka 2021 inaonyesha kuwa deni hilo ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

“Tathimini ya uhimilivu wa deni uliofanyika Novemba kama ulivyoelekeza Rais, unaonyesha deni letu ni himilivu kwa kipindi cha muda mfupi, wa kati na mrefu.

“Katika tathimini hiyo viashiria vinaunyesha kwamaba, deni la Serikali kwa uwiano wa Pato la Taifa ni asilimia 31 ambapo ukomo wa kidunia ni asilimia 55,” amesema Waziri Dkt.Mwigulu.

Amesema, kwa sasa bado nchi ipo kwenye nafasi nzuri kufikia kwenye kikomo cha deni kidunia.

Wachumi

Awali Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema kuwa,mikopo mingi inayochukuliwa na Serikali ni ile yenye umuhimu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi.

"Hakuna uamuzi wa kuchukua mkopo ambao haufuati taratibu za sheria ya mikopo,dhamana na misaada ambayo ni Sura ya 134 ya Sheria ya nchi,mikopo mingi inayochukuliwa na Serikali ni ile yenye umuhimu katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi,"amebainisha.

Prof.Luoga ameyasema hayo Januari 2,2022 kupitia mjadala wa Kitaifa juu ya umuhimu na usimamizi mzuri wa mikopo katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi.

Mjadala huo uliandaliwa kwa njia ya Zoom na kuratibiwa na Watch Tanzania kwa ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Kilimo Tanzania (TADB) huku wabobezi wa uchumi na wachambuzi kutoka ndani na nje ya Tanzania wakiwasilisha hoja nzito.

"Tunaposema deni la taifa ni himilivu ni uwezo wa nchi kurejesha deni lote lililokopwa ndani ya miaka 20 bila kuathiri ukuaji wa uchumi na uwezo wa serikali kugharamia shughuli za kijamii,"amesema Gavana Prof.Luoga.
 
Profesa Luoga amesema kuwa, nchi kama Tanzania inaonekana ulimwengu mzima na taasisi mbalimbali za Dunia zinaifanyia tathimini mara kwa mara.🔴 LIVE: Watch Tanzania inakuunganisha katika mjadala wa Kitaifa juu ya Umuhimu na usimamizi mzuri wa mikopo katika utekelezaji wa miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi 

"Hivyo inaonesha mwenendo wake ni mzuri na ni rahisi kukopeshwa na kurudisha kwa wakati na ukopaji wote sharti upitishwe na Bunge wakati wa kujadili mapendekezo ya bajeti ya Serikali kila mwaka,"amesema Profesa Luoga. 

Kwa upande wake, Mhadhiri na Mtafiti wa Masuala ya Uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Semboja H.Hatibu amesema kuwa,maana ya neno kukopa isiwe inatumika kupotosha kwa kuwa mikopo ina tija kubwa katika miradi ya kimkakati na maendeleo ya wananchi.

""Neno kukopa halina tafsiri kwamba unachukua kitu ambacho huna uhakika kwamba kesho utarudisha hapana, kuchukua fedha kwenye jamii nyingine na kuwekeza kwako sio tatizo ndio maana nchi kubwa sana kama Marekani, China na Japan zinachukua fedha kwenye taasisi kubwa kama World Bank (Benki ya Dunia) kwa ajili ya maendeleo ya nchi zao,"amefafanua.

Semboja ametumia mjadala huo kueleza kuwa, Tanzania inakopesheka kwa sababu ina rasilimali nyingi ambazo tutazifanyia kazi, "hivyo matokeo yake tunaweza kulipa madeni yote tunayodaiwa kwa wakati,"ameongeza Mhadhiri na Mtafiti huyo.

Naye mchambuzi wa masuala ya fedha, masoko na mitaji nchini Marekani, John Mashaka anasema kuwa,moja ya nchi ambayo ina uchumi wa kipekee ni Singapore na Tanzania inaweza kufikia hatua hiyo.

"Singapore ni moja ya nchi ambayo ni economic miracle, hii imetokana na sera bora za uchumi walizonazo, miaka ya 1967 ilikuwa ni nchi masikini sana kutokana na kutokuwa na rasilimali, lakini leo hii kipato cha wastani kwa mtu anayefanya kazi ni shilingi milioni 152,"amesema huku akiashiria kuwa, kwa mazingira yaliyopo hapa Tanzania uwezekano wa kufikia huko upo wazi.

Pia amesema, Tanzania ni kati ya nchi chache duniani ambazo zimejaliwa kuwa na rasilimali na maeneo mengi ya uwekezaji ambayo yanampa faraja mtu yeyote ambaye anataka kuwekeza mtaji wake.

"Mfano, Ethiopia sasa hivi ukiwa unafanya biashara ni ngumu sana kurudisha fedha zako nje, lakini Tanzania ni rahisi sana kuwekeza nchini na kurudisha fedha nje, hii imetokakana na mazingira mazuri ya uwekezaji yaliyopo nchini Tanzania, hivyo hilo ni jambo la kujivunia na kusonga mbele,"amesema.

Wakati huo huo,Afisa Mkuu wa Fedha katika Serikali ya Jimbo la Connectcut nchini Marekani ambaye ni Diaspora, Lunda P.Asmani amesema,mataifa mengi duniani huwa yanakopa fedha kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.

Asmani amesema, hata Marekani ambalo ni Taifa kubwa duniani na lenye nguvu kiuchumi pia huwa inakopa ingawa wao tofauti ipo kwenye matumizi.

"Nchi kama Marekani haina tofauti na nchi zingine kama Tanzania katika ukopaji, utofauti upo katika matumizi ya mkopo huo.

"Kwa nchi zinazoendelea (kama Tanzania) huwa zinakopa kwa ajili ya miradi endelevu au ile ya kimkakati, lakini nchi kama Marekani huwa inakopa kwa ajili ya usawa wa vizazi,"amesema Asmani.

Dkt.Joseph L.Masawe ambaye ni mtumishi wa zamani wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na Shirika la Fedha Duniani (IMF) amesema, Serikali iliamua kujiunga na mashirika ya Kimataifa na taasisi mbalimbali za kifedha kwa kuwa, inatambua umuhimu wake katika kuiwezesha kufikia malengo yake hususani miradi mikubwa ya maendeleo.

"Tanzania tulijiunga na vyombo hivi vya World Bank (Benki ya Dunia), IMF (Shirika la Fedha la Kimataifa) na African Development Bank (Benki ya Maendeleo Afrika) mnamo Septemba 10, mwaka 1962 na tulifanya hivyo kwa sababu tulielewa maana yake,"amesema.

Naye Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Dkt.Abdula H.Makame amesema,kukopa si jambo la ajabu kabisa, kwani nchi yeyote kabla haijakopa lazima ifanye mipango yake ni kwa namna gani inakopa na kurejesha.

"Katika nchi za Afrika Mashariki nchi zote zinakopa na kulipa kwa wakati, hivyo tupuuzie maneno mitandaoni yanayosemwa kuhusu masharti na mikopo hii haina ukweli wa aina yoyote,Tanzania iliweza kuridhia Itifaki ya Umoja wa Fedha na miongoni mambo tuliyokubaliana ni kuwa na vigezo vya uwiano wa uchumi mpana,Tanzania mapaka sasa kwa jinsi Benki ya Dunia inavyosimamia uchumi wetu, sisi ndio vinara wa kukidhi vigezo,"amesema Mbunge huyo.

Wakati huo huo, Waziri wa katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi amesema kuwa,Tanzania tunakopesheka kwa sababu tuna uwezo wa kukopa na uchumi wetu umekuwa ni imara ndio maana tumeingia kwenye uchumi wa kati na kuzidi nchi nyingi Afrika.

"Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ina jukumu kubwa sana la kuhakikisha inapitia upya na kufanya kitu kinaitwa vetting na kutoa legal opinion, hivyo mkataba wowote hauwezi kusainiwa bila kupitiwa na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.Kwenye masharti ya dhamana ni lazima masharti yawe hayagusi au kuweka rehani rasilimali yeyote muhimu ya nchi hii, ikiwa ni pamoja na madini,"amefafanua Profesa Kabudi.
 
 
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), Moremi A.Marwa amesema kuwa,ukubwa wa soko kwenye upande wa hisa umeongezeka karibu asilimia 4.5 kutoka karibu trilioni 15.4 mpaka 15.8.

Afisa Mtendaji Mkuu huyo amesema kuwa, hilo ni ongezeko la karibu shilingi bilioni 500 katika kipindi cha miezi tisa, jambo ambalo linadhirisha kuwa mambo yapo vizuri.

Post a Comment

0 Comments