Safari ya kuifungua mikoa mbalimbali kiuchumi yashika kasi Zanzibar, Rais Dkt.Mwinyi abisha hodi Mkoa wa Kaskazini Unguja

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Alhaj Dkt. Hussein Ali Mwinyi amesema ujenzi wa Gati ya Mkokotoni, unalenga kuimarisha utoaji wa huduma ili ziweze kuwa bora na endelevu, sambamba na kuufungua kiuchumi Mkoa Kaskazini Unguja.

Dkt. Mwinyi amesema hayo katika hafla ya Ufunguzi wa Gati ya Mkokotoni, Mkoa Kaskazini Unguja, ikiwa ni shamrashamra za kutimia miaka 58 ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiwa na Mkewe Mama Mariam Mwinyi wakipata maelezo ya michoro ya Gati ya Mkokotoni kutoka kwa Mhandisi wa Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA), Mansour Mohammed,kabla ya kuifungua Gati Mpya ya Bandari ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu).

Amesema, ujenzi wa Gati ya Mkokotoni una dhamira ya kuimarisha utoaji wa huduma ili ziweze kuwa bora na endelevu kwa abiria wanaotumia Bandari hiyo pamoja na mizigo mchanganyiko.
 
Rais amesema,mradi huo unalenga kuufungua mkoa huo kiuchumi, wakati ambapo malengo ya Serikali ni kuiboresha zaidi bandari hiyo ili kuziwezesha meli kubwa kutumia Bandari hiyo, ikizingatia Mji wa Mkokotoni unaendelea kukua kwa kasi kubwa na hivyo kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii.

Dkt. Mwinyi amesema, mradi wa Gati unaolenga kuimarisha shughuli za Bandari utachangia kwa kiasi kikubwa ukusanyaji wa mapato ya Serikali, sambamba na kurahisisha usafiri wa abiri na mizigo inayoingia na kutoka hapa Zanzibar.Alisema kukamilika kwa ujenzi wa Bandari ya Mkokotoni kutainua Uchumi wa Zanzibar na kurahisha shughuili za wananchi kiuchumi na kijamii.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akiondoa kitamba kuweka Jiwe la Msingi la Uzinduzi wa Gati ya Bandari ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja,ikiwa ni Shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar (kushoto kwa Rais) Mkewe Mama Mariam Mwinyi na (kulia kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kaskazini Unguja, Ndg.Iddi Ame Haji na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mhe.Zuberi Ali Maulid.(Picha na Ikulu).

Aliwaomba wananchi wanaotumia Gati hiyo kuitunza ili iweze kudumu kwa muda mrefu na akazitaka taasisi zote zitakazofanyakazi katika Bandari hiyo kufanyakazi kwa weledi, uadilifu, uaminifu na kujiepusha na vitendo vya rushwa na ubadhirifu wa mali ya umma, hususan katika suala la ukusanyaji wa mapato.

Dkt. Mwinyi amewataka Manahodha wa vyombo vya baharini kufuata sheria na mingozo inazotolewa na mamlaka zinazohusika ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.

Alisema pia Serikali inajikita katika ujenzi wa Bandari ya Mangapwani itakayohusisha Gati mbali mbali ili kuifungua Zanzibar kiuchumi.Alisema kukamilika kwa ujenzi wa Gati hiyo ni hatua itakayowaletea faraja na kuleta mageuzi makubwa ya kimendeleo kwa wananchi wanaoishi maeneo hayo.Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akitembelea Gati Mpya ya Bandari ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya kuifungua rasmi leo Januari 4,2022, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, akipata maelezo kutoka kwa Mhandisi wa Wakala wa Majengo Zanzibar (ZBA), Mhandisi Mansour Mohammed (kushoto kwa Rais) na Waziri wa Afya Ustawi wa Jamii Wazee Jinsia na Watoto Zanzibar, Mhe.Nossor Amhed Mazrui na kulia kwa Rais ni Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi na Kaimu Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi,Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale,Mhe.Lela Mohammed Mussa.(Picha na Ikulu).

Alieleza kuwa, mradi huo umetekelezwa na Serikali kwa asilimia mia moja na kunasibisha hali hiyo kwa kusema pale patakapokuwepo mipango thabiti, Serikali itaweza kutekeleza miradi mbalimbali (isiyo mikubwa) kwa kutumia fedha zake za ndani bila kutegemea wafadhili.

Aliushukuru Uongozi wa Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kwa kuimarisha Bandari ya Mkokotoni na kukamilisha ujenzi wa Gati hiyo ambayo ni muhimu sana kwa maendeleo ya wananchi, akibainisha kazi nzuri iliyofanyika na inayofaa kuigwa na Wizara nyengine.

Alisema, wakati Zanzibar ikiadhimishia miaka 58 ya Mapinduzi, imeshuhudia kuwepo maaendeleeo makubwa ya miundombinu, akibainisha hali hiyo ni kielelezo cha Serikali katika kuwaletea maendeleo wananchi na kuondokana na chanagmoto mbali mbali zinazowakabili.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk.Hussein Ali Mwinyi akikata utepe kuashiria kuifungua Gati Mpya ya Bandari ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja, ikiwa ni shamrashamra za kusherehekea Miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar na (kushoto kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Mariam Mwinyi, Kaimu Waziri wa Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Mhe.Lela Mohammed Mussa na (kulia kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, Mhe.Ayoub Mohammed Mahmoud.(Picha na Ikulu).

Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi alisema Serikali iinakusudia kuwaletea maendeleo wananchi wake katika nyanja zote za kijamii na kiuchumi, huku akibainisha azma ya Serikali ya kuziimarisha Bandari za Malindi, Mkoani na Wete Pemba pamoja na kuanza matayarisho ya ujenzi wa Bandari za Kizimkazi na Shumba Mjini ili kurahisisha shughuli za ukuaji wa kiuchumi na kijamii.

Nae, Kaimu Waziri, Wizara ya ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi, Leila Mohammed Mussa alisema kuna umuhimu wa Zanzibar kuwa na Gati za kisasa ili iweze kupata maendeleo, hususan katika utekelezaji wa dhana ya Uchumi wa Buluu.

Alisema kukamilika kwa mradi huo ni kielelezo tosha cha kuyaenzi Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, akibainisha Gati hiyo itarahisisha shughuli za ushushaji na upakiaji wa mizigo, sambamba na kuwahakikisha usalama wananhi wanaosafiri kati ya Mkokotoni na Visiwa vya Tumbatu.

Aidha, Waziri wa Nchi 0fisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira, Suleiman Jaffo alisema kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, atasimamia kikamilifu kuhakikisha changamoto mbali mbali zinazohusiana na masuala yaliomo ya Muungano yanapatiwa ufumbuzi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt.Hussein Ali Mwinyi alipokuwa akitoa hotuba yake katika sherehe za ufunguzi wa Gati ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja,hafla iliyofanyika leo ikiwa ni shamrashamra za kutimiza miaka 58 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.(Picha na Ikulu). 

Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa wa Kaskazini Unguja Ayoub Mohamed Mahamoud alisema ufunguzi wa Gati hiyo, utawaondolea kero ya usafiri wnanachi wa Visiwa vya Tumbatu, kuchochea harakati za kiuchumi, kuokoa muda wa safari za baharini kati ya Zanzibar na maeneo mengine ya Tanzania, na hivyo akatumia fursa hiyo kuiomba Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi kuharakisha ufunguzi wa shuguli za Gati hiyo ili wananchi kupata tija.

Vile vile Mwakilishi wa Jimbo la Tumbatu kupitia tiketi ya CCM, Haji Omar Kheir alieleza kuwa ufunguzi wa Gati ya Mkokotoni ni utekelezaji wa Ilani ya chama hicho ya 2020 - 2025.

Alisisitiza, umuhimu wa Serikali kusimamia matakwa ya mkataba wa mradi huo kwa kuhakikisha vyombo vyote vinaweza kufunga nanga na kufanya shughuli zake nyakati zote, iwe wakati maji yamekupwa au yamejaa.
Muonekano wa Gati Mpya ya Bandari ya Mkokotoni Mkoa wa Kaskazini Unguja baada ya kufunguliwa rasmi leo Januari 4,2022, na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi.(Picha na Ikulu).

Mwakilishi huyo alitumia fursa hiyo kuiomba Serikali kuhakikisha Boti iliyonunuliwa kwa shughuli za usafirishaji wa wananchi kati ya Mkokotoni na Tumbatu inafanya shughuli zake kikamilifu kwa kuzingatia kuwepo kwa upepo mwingi unaovuma katika kipindi hiki cha Kaskazi, hali inayotishia usalama wa wasafiri.

Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Amour Hamil Bakar, alitoa taarifa ya kitaalamu kuhusiana na mradi huo na kusema ujenzi wa Gati ya Mkokotoni umefanywa na Kampuni ya Ms Edge Engineering Co Ltd chini ya usimamizi wa Wakala wa Majengo (ZBA) na kugharimu kiasi cha shilingi Bilioni 6.4.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news