International Holding Company (IHC) yaahidi kuleta wawekezaji Zanzibar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi amekutana na uongozi wa Kampuni ya International Holding Company (IHC) yenye makao yake Abudhabi.

Kampuni hiyo ni kubwa katika Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na ya pili kwa nchi za Magharibi ambapo katika mkutano huo Abudhabi imeahidi kuleta wawekezaji wa kigeni hapa Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akizungumza na Uongozi wa Kampuni ya International Holding Company (IHC) ya Abu Dhabi ukingozwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni hiyo Bw.Syed Basar Shueb, kuzungumzia masuala ya Uwekezaji Zanzibar, mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa Kampuni hiyo Abu Dhabi Januari 18,2022, na kushoto kwa Rais ni Balozi wa Tanzania (UAE), Mhe. Balozi Mohammed Abdalla Mtonga.

Mkutano huo ulifanyika katika ukumbi wa Kampuni ya International Holding Company (IHC) uliopo Mjini Abudhabi.

Rais Dkt. Mwinyi katika mazungumzo hayo aliwaeleza kwa undani wawekezaji hao wa Kampuni ya IHC fursa zilizomo katika Uchumi wa Buluu na kuwaalika kuja Zanzibar.

Alisema kuwa, Zanzibar kwa sasa inahitaji wawekezaji makini huku akieleza kwamba moja ya fursa zilizomo katika Uchumi wa Buluu ni uwekezaji katika visiwa vidogo vidogo vinavyofikia 53 katika bahari ya Zanzibar.

Fursa nyingine zinazoambatana na uwekezaji wa Uchumi wa Buluu alizozieleza Rais Dkt. Mwinyi ni pamoja na uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, uvuvi mkubwa katika bahari kuu, ujenzi na kuzifanyia matengenezo meli za uvuvi, ujenzi wa bandari kubwa zitazoweza kuhimili meli kubwa za mizigo.

Aidha, Rais Dkt. Mwinyi amesisitiza kwamba yote hayo yatafanikiwa iwapo kutakuwa na miundo mbinu mizuri katika huduma za kijamii na kuwaeleza wawekezaji hao umuhimu wa kusaidia huduma za kijamii za elimu na afya na kuanzisha mikakati maalum ya kiuchumi.

Nae Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), Shariff Ali Shariff akitoa muelekeo wa fursa za uwekezaji kwa waekezaji hao aligusia hali ya watalii ilivyo Zanzibar ambapo licha ya ugonjwa wa UVIKO- 19, Zanzibar iliendelea kupokea watalii 39,512 kati ya mwezi Januari hadi Disemba mwaka jana.

Alieleza kuwepo kwa fursa za kuwekeza katika kuchakata bidhaa za baharini, ujenzi wa boti za uvuvi pamoja na kuzifanyia matengenezo, ujenzi wa mji mwengine utakaoitwa Zanzibar Marina City na kusaidia kilimo cha mwani.

Pia, alieleza haja kwa wawekezaji hao kuisaidia Zanzibar kuwa na kituo cha kukuza vipaji kwa michezo mbalimbali hali itakayoipaisha Zanzibar katika sekta ya michezo.

Mkurugenzi huyo wa ZIPA alibainisha kuwepo kwa hekta 6000 za ardhi inayohitaji kuendelezwa katika eneo la Makurunge, ardhi ambayo ni mali ya Zanzibar na inafaa kwa ajili ya kilimo.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alikutana na Waziri wa Nchi anayeshughulikia Mambo ya Nje Sheikh Shajkboot Nahyan Al Nahyan ambapo walizungumza uhusiano baina ya Tanzania na Umoja wa Falme za Kiarabu ambapo pamoja na mambo mengine alizungumzia ufunguzi wa Ubalozi Mdogo wa UAE Zanzibar pamoja na kurejesha huduma za ndege za (UAE) na kufanya safari zake Zanzibar.

Ziara ya Rais Dkt. Mwinyi ilimalizika Jumatano Januari, 19, 2022.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news