Mambo mazuri yanaendelea kushika kasi Zanzibar

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi ameshuhudia utiaji saini mpango mkuu na kufanya utafiti na upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya ya Malindi ambayo itakuwa ya kitalii pamoja na mji wa kisasa katika eneo la Bwawani Mjini Zanzibar.

Utiaji saini huo umefanyika Ikulu jijini Zanzibar ambapo kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar saini iliwekwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi,Mawasiliano na Uchukuzi, Amour Hamil Bakari na kwa upande wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ambayo ni taasisi ya Serikali ya nchi hiyo saini iliwekwa na Sheikh Nasser Al Harthy ambapo pia Mkurugenzi wa Shirika la Bandari Nahaat Mahfoudh naye aliweka saini kwa upande wa wizara hiyo na Mohamed Al Taooq alisaini kwa niaba ya mamlaka hiyo. 
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe.Dkt.Hussein Ali Mwinyi akishuhudia utiaji wa saini wa Mpango Mkuu na kufanya utafiti na upembuzi yakinifu kwa ajili ya ujenzi wa bandari mpya ya Malindi,kwa upande wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar amesaini Katibu Mkuu Wizara ya Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Bw.Amour Hamil Bakari na kwa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman, Sheikh Nasser Al Harthy,hafla hiyo imefanyika katika ukumbi wa Ikulu jijini Zanzibar.

Akizungumza mara baada ya utiaji wa saini huo,Rais Dkt.Mwinyi alieleza kwamba katika mradi huo bandari mpya ya Malindi ambayo inatarajiwa kujengwa mara baada ya kujengwa bandari ya mpya ya Makontena huko Mangapwani itageuzwa kuwa bandari ya kitalii pamoja na kulitengeneza eneo lote kutoka Bandarini Malindi hadi Bwawani Hoteli ili eneo hilo liwe na majengo mapya ya burudani,hoteli na majengo ya kuishi.

Alisema kuwa, eneo hilo ambalo litakuwa la mji mpya wa kitalii linakisiwa kuwa na ukubwa wa hekta 30 ambazo zitapatikana baada ya kufukia Bahari katika eneo hilo ambalo litakuwa la mji mpya wa kitalii.

Alieleza kwamba amefurahishwa kutokana na hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutafuta wawekezaji katika maeneo mbalimbali, Serikali ya Oman mbali ya kutiliana saini na Serikali juu ya ujenzi wa Bandari ya Makontena imetiliana saini tena na Serikali katika ujenzi huo utakaopelekea kuwa na mji mpya wa kisasa hapo Malindi.

Rais Dkt.Mwinyi alitoa shukurani kwa kujitokeza kwa wawekezaji hao na kusema kwamba kiasi cha Dola milioni 500 zitatumika katika ujenzi wa mradi huo mkubwa wa kimkakati. 

Alitumia fursa hiyo kuwapongeza wawekezaji hao waliokuwa na nia ya kuwekeza hapa Zanzibar na kusema kwamba Zanzibar inaendelea kutafuta wawekezaji katika maeneo mbalimbali ambapo lengo na madhubuni ni kwamba mpango wa maendeleo ya Zanzibar wa miaka mitano unatakiwa kuwashirikisha sekta binafsi katika kusaidia na Serikali katika kujenga miradi ya maendeleo yenye tija na ile ya kibiashara. 

Aliongeza kuwa, Serikali itaendeleza jukumu lake la kuweka mazingira mazuri pamoja na kuwavutia wawekezaji ambapo kwa yale mambo ambayo wawekezaji hawataweza kuingia yatafanywa na Serikali kama vile ujenzi wa barabara.

Aidha, Rais Dkt.Mwinyi alieleza kwamba wawekezaji hao kutoka Serikali ya Oman wana moyo mkubwa hiyo ni kutokana na kuweka fedha nyingi katika mradi huo. 

Nae Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi,Rahma Kassim Ali alisema kuwa ujenzi wa mradi huo utasaidia kwa kiasi kikubwa katika kuiletea mendeleo endelevu Zanzibar. 

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman, Sheikh Mohamed Al Taooqi kwa upande wake alimuhakikishia Rais Dkt.Mwinyi kwamba mamlaka hiyo itahakikisha mradi huo unafanikiwa na kufikia malengo yaliyokusudiwa. 

Mapema uongozi huo wa Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman ulimuonesha Rais, Dkt.Mwinyi michoro na ramani za mradi huo ambao utakuwa wa aina yake na utaweza kuinua uchumi na maendeleo ya Zanzibar ambapo Rais kwa upande wake alitoa shukurani zake na kupongeza hatua hiyo iliyofikiwa. 

Mamlaka ya Uwekezaji ya Oman pia, ilishawahi kulitiliana saini na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mnamo Januari 18, mwaka 2021 juu ya ujenzi wa bandari ya Mangapwani ambayo itajumuisha bandari tofauti ikiwemo ya makontena na mizigo mchanganyiko kazi ambayo hivi sasa inakwenda vizuri na ipo katika hatua ya upembuzi yakinifu na hatimae itaingia katika utekelezi wa ujenzi.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news