MO Dewji ndiyo kwaheri Simba SC? Kule Jangwani wana akiba ya alama 10

NA GODFREY NNKO

MWAKA 2022 licha ya Klabu ya Simba yenye maskani yake jijini Dar es Salaam kutwaa Kombe la Mapinduzi hivi karibuni, mwenendo wake katika michuano ya Ligi Kuu ya NBC umekuwa mbaya hali ambayo inaonesha uwezekano wa kulisalimisha taji hilo.
Wekundu wa Msimbazi ni watetezi wa taji hilo kwa msimu uliopita na huenda matokeo hayo yakamfanya mwekezaji pekee kwa umiliki wa asilimia 49 ya hisa zenye thamani ya shilingi Bilioni 20, Bilionea Mohamed Dewji akakasirika tena na kufanya uamuzi mgumu.

Tujikumbushe

Mwaka jana, Mo Dewji alitangaza kujiuzulu Uenyekiti wa Bodi ya Simba SC na kubaki mwekezaji pekee kwa umiliki wa asilimia 49 ya hisa zenye thamani ya shilingi Bilioni 20.

Akitangaza uamuzi wake huo, Dewji alisema kwamba nafasi yake itashikiliwa na aliyekuwa Makamu wake, Salum Abdallah Muhene (Try Again).

"Muda umefika mimi kama Mohamed, tumefanya mkutano tarehe 21 mwezi wa tisa, 2021 na tumekubaliana kwamba mimi nitajiuzulu kuwa Mwenyekiti wa Simba Sports Club. 

"Naomba sana wana Simba msifikirie mimi nimeondoka kwenye Simba, bali bado ni mwekezaji kwenye Simba ni mwana hisa kwenye Simba, naipenda Simba na nitaendelea kuipenda Simba mpaka siku yangu ya mwisho," alisema Dewji jijini Dares Salaam.

Hatua hiyo ilikuja siku moja tu baada ya timu kulazimishwa sare ya 0-0 na wenyeji, Biashara United katika mchezo wake wa ufunguzi wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara katika dimba la Karume mjini Musoma Mkoa wa Mara huku Nahodha, John Bocco akikosa penalti dakika ya 90. 

Aidha, Januari 13, 2020 Mo Dewji pia alitangaza kujiuzulu Uenyekiti wa Bodi ya klabu hiyo na kubaki kama mwekezaji mara tu baada ya baada ya mchezo wa fainali ya Kombe la Mapinduzi uliomalizika kwa Simba SC kufungwa 1-0 na Mtibwa Sugar Uwanja wa Amaan, Zanzibar.

Kama ilivyokuwa mwaka juzi, Mo Dewji alijiuzulu baada ya Simba SC kufungwa kwenye fainali ya Kombe la Kombe la Mapinduzi na safari iliyofuata akang'atuka.

Simba SC Vs Kagera Sugar

Hamisi Kiiza (Diego) ambaye ni mshambuliaji mkongwe wa Kimataifa wa Uganda leo ametokea benchi kuifungia bao pekee Kagera Sugar na kuibuka na ushindi wa 1-0 dhidi ya mabingwa watetezi, Simba SC.

Kiiza amewasababishia Simba SC kilio hicho leo Januari 26, 2022 katika mchezo wa Ligi Kuu ya NBC katika dimba la Kaitaba lililopo Bukoba Mkoa wa Kagera.

Mshambuliaji huyo aliingia dakika 56 kuchukua nafasi ya Ally Ramadhani na akafunga bao hilo dakika ya 70 akimalizia pasi nzuri ya Ally Nassor kabla ya Mganda huyo kutolewa kwa kadi nyekundu dakika ya 90 kufuatia kuonyeshwa kadi ya pili ya njano.

Watani zao wanachekelea kwa sauti baada ya Simba SC kucheza mechi 13 na kuambulia alama 25 huku Yanga SC ambao nao ni wenyeji wa Jiji la Dar es Salaam wakicheza mechi 13 ambazo zimewatengenezea alama 35. 

Kwa matokeo hayo, Simba imezidiwa alama 10 ambazo kwa mtazamo wa haraka ni nyingi katika Ligi Kuu ya NBC ambayo inaushindani mkubwa mwaka huu na hakuna kiporo kwa sasa.

Leo huu ni mchezo wa pili kwa Simba SC kupoteza baada ya ule wa kwanza kuwa mbele ya Mbeya City na bao walilofungwa ni moja.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news