TAEC yatoa mafunzo kwa watumiaji wa vyanzo vya mionzi nchini

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

TUME ya Nguvu za Atomiki Tanzania (TAEC) imeendesha mafunzo ya wiki moja kwa taasisi tatu tofauti wakiwemo wafanyakazi katika migodi, viwanja vya ndege na Baraza la Wawakilishi Zanzibar ikiwa ni utekelezaji wa takwa la kisheria, ambayo inaitaka tume hiyo kutoa mafunzo kwa watumiaji wa vyanzo vya mionzi.

TAEC imeundwa kwa Sheria ya Nguvu za Atomu Na. 7 ya Mwaka 2003 (Atomic Energy Act No.7 of 2003) ni baada ya Sheria ya Bunge Na. 7(2003) kufuta Sheria Na.5 ya mwaka 1983 (The Protection from Radiation, No. 5 of 1983) iliyoanzisha Tume ya Taifa ya Mionzi (National Radiation Commission).
Dkt.Remijius Ambross Kawala, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi na Teknolojia wa TAEC ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania akizungumza kabla ya kuyafunga mafunzo ya wiki moja yaliyofanyika makao makuu ya TAEC jijini Arusha. Washiriki wa mafunzo hayo wamejengewa uelewa juu ya usalama wa mionzi kutoka kwa wataalam wa tume hiyo. 

Sheria hii imeipa TAEC mamlaka ya kudhibiti matumizi salama ya mionzi nchini ikiwemo kuhamasisha matumizi salama ya teknolojia ya nyuklia nchini.

Dkt.Remijius Ambross Kawala, Mkurugenzi wa Huduma za Ufundi na Teknolojia wa TAEC ambaye alimuwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania katika hafla ya kuyafunga mafunzo hayo yaliyofanyika makao makuu ya tume jijini Arusha, amewataka washiriki hao kutambua kuwa, elimu waliyoipata juu ya usalama wa mionzi itawasaidia kuwa watendaji bora na kuwajali wengine huku ikiwasaidia kuishi maisha marefu,pamoja na kuisaidia jamii yao kuepukana na madhara yatokanayo na mionzi
Pia amewataka washiriki hao kuzichangamkia fursa zilizopo TAEC kwa ajili ya kujali afya zao wawapo kazini,kutambua mazingira yao yenye viasili vya juu vya mionzi pamoja na kuhakikisha usalama na kuwalinda wengine bila kuvunja sheria ya nchi.

Dkt.Kawala amewasihi wale wote waliopata mafunzo kutoka sehemu za Mafia,Baraza la Wawakilishi Zanzibar, machimbo ya madini Bulyanhulu,waweze kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kuwashirikisha wenzao ambao hawajapata mafunzo,sambamba na kuwatia moyo ili na wao waweze kupata mafunzo hayo.
Dkt. Kawala kutoka TAEC akimkabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo juu ya usalama wa mionzi mmoja wa washiriki kama inavyoonekana katika picha.

"Mazoezi yako yoyote unayoyafanya sasa hivi lazima yajikite na kujali mazingira yaliyopo na haki ya mwenzako,kazi unayoifanya hakikisha haimuumizi mwenzako. Hatusemi kwamba teknolojia ya mionzi ina madhara kiasi hicho la hasha,ila kitu chochote kina madhara kama utakiuka taratibu ya kukitumia,mfano ndege ni nzuri sana, lakini ikitokea hitilafu ni hatari,kila kitu chenye matumizi mazuri ukikiuka kinakuwa na matumizi mabaya,"amesema Dkt.Kawala kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa TAEC. 

Naye Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Mafunzo TAEC, Dkt.Shovi Sawe amesema kuwa, lengo la mafunzo hayo kwanza kabisa wanatekeleza matakwa ya kisheria ya nguvu za Atomiki Tanzania anmbayo inaitaka Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania kutoa mafunzo kwa watumiaji wa vyanzo vya mionzi

Aidha, amesema kuwa TAEC inataka kuwajengea uwezo waelewe namna salama ya kufanya kazi maeneo ya mionzi wao pamoja na wote wanaofanya kazi katika maeneo hayo ili waweze kuwa salama pamoja na mazingira na kuwaelekeza namna nzuri vyanzo vya mionzi vikishatumika au kuisha muda wake jambo gani wafanye ili waweze kuwa salama zaidi.

"Na kwa utararibu tu ni kwamba watatakiwa vyanzo hivyo wavirudishe TAEC kwa ajili ya uhifadhi katika stoo ya kutaifa au kurudisha kwenye nchi waliyotoa kwa ajili ya kuhifadhiwa huko,"amesema.
Akisisitiza utii wa sheria katika mionzi, Dkt.Sawe ameisema, mionzi ni moja vitu ambavyo vina manufaa makubwa kwa jamii na maendeleo ya kiuchumi, lakini isipotumika vizuri ni mbaya sana,hivyo ndiyo sababau TAEC imekuwa ikikumbusha mara kwa mara hatua zichukuliwe ili kuhakikisha kuna usalama wa wafanyakazi,raia pamoja na usalama wa mazingira.

Akifafanua mionzi kwa lugha rahisi, Dkt.Shovi Sawe amesema, nishati ambayo inatiririka kutoka vyanzo vya asili kama vile madini ya uranium,lakini pia inaweza ikawa ni nishati inayotiririka kutoka kwenye vifaa vilivyotengenezwa na binadamu kama mashine za x-ray,ambapo binadamu ameweza kuona faida ya kuvitumia.

Kwa upande wake mshiriki kutoka Ofisi ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Mohamed Bilal amesema hapo awali kabla ya kupata mafunzo walikuwa wanatumia mashine za kuskani, lakini walikuwa hawafahamu usalama wao upo wapi ila kwa sasa baada ya mafunzo anajiona akiwa salama zaidi,ameahidi kwenda kuyatendea kazi kwa weledi yale yote aliyojifunza kwa faida ya wengine pia.

Amesema, jamii inatakiwa kujifunza zidi kwani ipo tabia ya kuchukua vitu ambavyo vimeshatumika ambavyo havifahamiki usalama wake zaidi,hivyo ameishauri jamii kutokupenda kutumia vitu ambavyo vimeshapitwa na wakati, kwani ni hatari kwa afya zao,badala yake wachukue vitu vipya ili waweze kuwa salama zaidi.

Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya walioshiriki mafunzo mwenyekiti wa muda amewashukuru TAEC kwa mafunzo hayo,kwani wameongeza vitu vingi ambavyo hapo awali walikuwa hawavitambui na ameahidi kwenda kuwa mabalozi wazuri na kuaahidi kuzingatia na kuyapa kipaumbele huku wakifuata taratibu zote za kiusalama kwani mionzi ni mizuri.
Dkt. Kawala kutoka TAEC akimkabidhi cheti cha ushiriki wa mafunzo juu ya usalama wa mionzi mmoja wa washiriki kama inavyoonekana katika picha.

Kwa mujibu wa Dkt.Sawe, washiriki 19 kati yao watano wametoka Baraza la Wawakilishi Zanzibar,mmoja kutoka Uwanja wa Ndege Mafya na 12 kutoka mgodi wa Bulyanhulu Kahama ambapo hadi sasa tangu kuanza kwa robo mbili zilizopita wameshiriki 303 kati ya Julai hadi Desemba 2021.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news