Rais Samia asema ukweli kuhusu 27,000/- ya kuunganisha umeme

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema, kuna maeneo nchini gharama za kuunganishwa umeme haitakuwa shilingi 27,000.
Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo Januari 4,2022 baada ya kupokea taarifa ya utekelezaji wa Mpango wa Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya UVIKO-19 Ikulu jijini Dar es Salaam.

"Tuliharibiwa kwa kusema mwananchi ataungiwa umeme kwa 27,000,gharama za umeme haziko hivyo,kuna maeneo tutafanya hivyo kuwabeba wananchi,kuna maeneo lazima gharama ya umeme irudi pale pale,Waziri umeogopa kusema,nakusaidia nenda katekeleze.

"Kuna maeneo lazima gharama ya umeme ibebe uhalisia unapompangia TANESCO aende akaunge umeme kwa elfu 27 kwa kila mtu yeye anatoa wapi hizo fedha? Hana pa kuzitoa lazima aunge umeme kwa gharama inayopaswa kwa kila pahala, Waziri nenda kasimamie hilo.
"Juzi nilikuwa naona watu wanalalamika kwenye TV wameshalipa miezi kadhaa umeme hawaungiwi ukiuliza TANESCO wanasema hatuna nguzo, hatuna vifaa elfu 27 tunafanyaje?Kwa hiyo waziri nenda usimamie watu walipe fedha inayotakiwa.

"Kila anayetaka umeme alipe gharama stahiki msiende juu, lakini nendeni kwenye gharama ambayo mwanachi atamudu kulipa na wale wa hali ya chini kabisa tuwabebe kama sera yetu inavyosema.

Hata hivyo,awali bei ya kuunganisha umeme wa njia moja iwe kijijini au mjini ilikuwa ni shilingi 27,000 kutoka sh. 177,000 iliyokuwepo awali, na wenye kuhitaji kuunganishiwa umeme wa njia tatu, gharama yake ni shilingi 139,000 kutoka shilingi 912,000 iliyokuwa ikitozwa awali.

Gharama hizo zimechangia kwa kiasi kikubwa TANESCO kushindwa kukidhi mahitaji ya watu wanaohitaji kufungiwa umeme kwa wakati kutokana na changamoto ya vifaa ambavyo pia upatikanaji wake na kuvifikisha baadhi ya maeneo nchini kwa ajili ya kuunganisha umeme ni gharama kubwa, hivyo kutekeleza majukumu yake kadri wanavyopata fedha.

Maagizo ya Mheshimiwa Rais Samia kwa waziri yakitekelezwa kwa ufanisi, kasi ya uunganishaji umeme itaendelea kuwa kubwa, kwa kuwa wananchi wakilipia gharama elekezi tofauti na 2,7000 ya sasa itawezesha upatikanaji wa vifaa kwa haraka, hivyo litabaki jukumu la TANESCO kuweka ratiba, kusambaza vifaa na kuunganisha umeme kwa kila mtu aliyeomba kuunganishiwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news