Rais Samia ataja kazi mpya ya Mheshimiwa Lukuvi,Kabudi akemea kejeli

NA GODFREY NNKO

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amesema aliyekuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na aliyekuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi amewapangia kazi maalumu.
Mheshimiwa Rais Samia ameyasema hayo leo Januari 10,2022 katika hafla ya kuwaapisha viongozi mbalimbali aliowateua mwishoni mwa wiki, uapisho huo umefanyika katika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.Walioapishwa ni pamoja na mawaziri,manaibu mawaziri,makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu.

“Nina kaka zangu wawili, William Lukuvi na Palamagamba Kabudi ukiwatazama hao umri wao ni kama wangu na niliowateua hamfanani kabisa, kwa hiyo kaka zangu hawa nimewavuta waje kwangu ili waje wanisimamie kuwasimamia nyie, kwa hiyo kuwaacha kwangu kwenye ile orodha hapo wote ni wadogo na mnahitaji kusimamiwa vizuri.

“Kaka yangu Kabudi amefanya kazi nzuri sana kusimamia mazungumzo ya Serikali na mashirika na ndiyo kazi ninayotaka nimkabidhi sasa kindakindaki aendelee na kazi hiyo ila kazi yake kwa sababu haipo kwenye muundo haitangazwi, mashirika yote kazi zote zitakazoingia ubia na Seriikali yeye ataongoza hiyo timu, kwa hiyo yeye ni baba mikataba,”amesema Mheshimiwa Rais Samia.

Pia ametumia nafasi hiyo kuwataka baadhi ya viongozi na Watanzania kwa ujumla kuacha kumchafua aliyekua Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi akisema kuwa waziri huyo ameitumikia nchi kwa uadilifu mkubwa, hivyo anastahili heshima zote.
Wakati huo huo, Mheshimiwa Rais Samia amesema kuwa, Mheshimiwa Lukuvi hatagombea Uspika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania badala yake amemsogeza Ikulu ili amsaidie kazi zake Ikulu.

"Kaka yangu Lukuvi, yeye ana kazi na mimi, mtaisikia baadaye. Lakini namvuta Ikulu, kazi yetu ni kuwasimamia nyinyi.Hatagombea Uspika. Kwa sababu nikiwatamazama hapo wote wanakaribia kustaafu bado miaka miwili wengine mna safari ndefu mimi na wale tulishastaafu, kwa hiyo kazi yetu sasa ni kushika kiboko kuwasimamia nyie na makatibu wakuu.

“Nimeona meseji nyingi wengine wanasema afadhali Lukuvi katoka, hajatoka yupo, wengine wameanza kumletea meseji za ajabu wakijua atagombania uspika, hatagombania ana kazi na mimi msianze kumchafua ametumikia taifa hili kwa uadilifu kwa muda mrefu muacheni aende na mimi tumalie kazi atakayopangiwa,”amesema Mheshimiwa Rais Rais.

Kwa upande wake, Naibu Spika wa Bunge, Mheshimiwa Dkt. Tulia Ackson amesema kuwa bunge lipo tayari kushirikina na kuyafanyia kazi mambo yote yatakayoletwa na mkuu huyo wa nchi. 

“Natoa ushauri kwenu kuwa Mheshimiwa Rais Samia amewaamini kumsaidia, hizo kazi ni kazi zake hivyo ninyi mnapoenda kuzifanya kazi hizo fanyeni kama wasaidizi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si vinginevyo. 

“Kila mmoja ambaye ameteuliwa katika nafasi yoyote aliyoipata, Mhe. Rais Samia alishafanya kazi katika maeneo hayo kwa kupeleka fedha nyingi kwa ajili ya miradi mbalimbali, ninawapongeza kwa sababu mnayo sehemu ya kuanzia katika kuelezea mazuri ya Serikali hii,”amesema Dkt. Tulia.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Mahakama Kuu ya Tanzania itaendelea kushirikiana na wizara zote hasa wizara inayohusiana na teknolojia iweze kwenda kwa kasi, isiwe na vizuizi wala masharti mengi ili kuweza kukuza uchumi kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).

Post a Comment

0 Comments