RC PWANI AWAPIGA MARUFUKU WALIMU WENYE TABIA YA KUZUIA WANAFUNZI WASIINGIE DARASANI KWA KIGEZO CHA KUKOSA MICHANGO,ASEMA MWALIMU ATAKAYEBAINIKA ATAKIONA CHA MOTO

NA ROTARY HAULE

MKUU wa Mkoa wa Pwani, Abubakar Kunenge amewapiga marufuku walimu wa Shule za Msingi na Sekondari kuacha tabia ya kuwazuia wanafunzi kuingia darasani kwa kisingizio cha kukosa michango.

Kunenge ametoa kauli hiyo leo Januari 19, 2022 wakati alipokuwa akizungumza na walimu pamoja na wanafunzi wa Shule ya Msingi Maendeleo na Shule ya Sekondari Bundikani zilizopo Kata ya Mailimoja Kibaha Mjini.
Katika ziara hiyo Kunenge amesema kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amefanyakazi kubwa ya kutafuta fedha na hatimaye kufanikiwa kujenga madarasa na kwamba hakuna ruhusa kwa walimu kuzuia wanafunzi kwasababu ya michango.

"Nataka kuona wanafunzi wote wanaingia darasani kusoma na hii tabia ya kuwazuia wanafunzi wasiingie darasani kwasababu ya kukosa michango isiwepo na sipendi kusikia katika Shule yoyote ndani ya Mkoa wangu,"amesema Kunenge.

Kunenge amesema kuwa, ikitokea shule mwanafunzi amefukuzwa kwa sababu ya michango ni wazi kuwa mwalimu Mkuu au Mkuu wa Shule ( HeadMaster) atachukuliwa hatua kali kwakuwa atakuwa ni moja kati ya watu wanaomhujumu Rais Samia.
Amesema kuwa,wanafunzi wamepata fursa ya kusoma bila malipo na itashangaza kuona wanazuiwa jambo ambalo halitachekewa kwa namna moja au nyingine huku akisema madarasa hayo lazima yazae matunda.

Kunenge,ameongeza kuwa Serikali kupitia Rais Samia bado inaendelea kuweka mazingira mazuri kwa wanafunzi na kwamba matarajio ya Rais ni kuona watoto wakitanzania wananufaika na madarasa hayo kwa kupata elimu bora.
Aidha, Kunenge amewataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii na kamwe wasidanganywe na jambo lolote kwakuwa Rais atapata faraja akiona juhudi zake za kujenga madarasa hayo yanatumika kwa malengo.

"Nimekuja hapa kuwatembelea watoto wangu ili nione jinsi mnavyotumia madarasa yenu ,lakini pia nilitaka kujua kama ninyi wanafunzi mmeripoti lakini baada ya kuona nimejiridhisha na nawaomba someni kwa bidii bila kudanganywa na mtu wala kitu chochote,"amesema Kunenge.
Aidha, Kunenge amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha, Mshamu Munde pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Kibaha, Sara Msafiri kwa usimamizi mzuri wa ujenzi wa madarasa hayo.

Kwa mujibu wa Kunenge,mpaka kufikia Junuari 18, 2022 tayari wanafunzi wa darasa la awali wameripoti shuleni kwa asilimia 44.68 ambapo maoteo yalikuwa 30,479 huku walioripoti Shuleni ni 13,618.

Kwa upande wa wanafunzi wa darasa la Kwanza mwaka huu matoteo yalikuwa 52,709 lakini jumla ya walioandikishwa ni 29,724 sawa na asilimia 56.39.

Mkuu wa Shule ya Sekondari Bundikani Bernda Muyenjwa ,amesema kuwa anamshukuru Rais Samia kwa kupeleka fedha Shuleni kwani walipokea jumla ya Sh.milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa.Muyenjwa, amesema kuwa Shule yake imekuwa ikifanya vizuri mwaka hadi mwaka na kwa upande wa Shule za Kata zilizopo Kibaha Mjini inashika nafasi ya pili.

Hata hivyo,Muyenjwa,alimuomba Mkuu wa Mkoa kuangalia namna ya kuifanya Shule hiyo hiwe na kidato cha Tano na Sita kwakuwa eneo la ujenzi wa madarasa mengine lipo na walimu wake wapo vizuri katika ufundishaji.

Diwani wa Kata ya Mailimoja Ramadhani Lutambi, amemshukuru Rais Samia juu ya fedha hizo kwakuwa watoto wote wameingia darasani muda mmoja wa asubuhi na wanakaa kwenye viti tofauti na zamani walipokuwa wanakaa chini.

"Tunaendelea kumshukuru Rais kwa zawadi nzuri aliyotupatia na sisi hatuna cha kumlipa ila tunachoahidi ni zawadi pekee ya kutoa matokeo mazuri ya kidato cha nne yasiyokuwa na ziro,"amesema.

Hata hivyo, akizungumza kwa niaba ya wanafunzi wenzake mwanafunzi wa kidato cha Kwanza katika Shule ya Sekondari Bundikani Abdul Hamad ,amesema wanamshukuru Rais Samia kwa kuwajengea madarasa kwakuwa wanasoma katika mazingira mazuri.

Abdul,amesema hakuna cha kumlipa lakini wanaahidi kusoma kwa bidii na kumpa matokeo mazuri ya kidato cha nne na hata katika mitihani yao ya kila mwaka.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news