Serikali kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo kukabiliana na maafa

NA MWANDISHI MAALUM

SERIKALI itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kukabiliana na maafa ambayo husababisha madhara makubwa kwa wananchi ikiwemo uharibifu wa miundombinu pindi yanapotokea.
Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Bw. Kaspar Mmuya akizungumza na wadau kutoka sekta na wizara mbalimbali (hawapo pichani) katika ufunguzi wa kikao kazi cha Kuthibitisha Mpango wa Dharura wa Kukabiliana na Ukame Tanzania kilichofanyika katika ukumbi wa Hazina jijini Dodoma Januari 26, 2022. (Picha na OWM).

Hayo yalisemwa na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya wakati akifungua kikao kazi na wadau mbalimbali kwa lengo la kuthibitisha Mpango wa Dharura wa Kukabiliana na Maafa kilichofanyika Januari 26, 2022 jijini Dodoma. 

Naibu Katibu Mkuu Mmuya alisema, mpango huo umeainisha shughuli zitakazofanywa na sekta mbalimbali kwa ajili ya kuzitekeleza kuweka mbinu bora za kuzuia madhara yatokanayo na ukame kupitia rasilimali zilizopo nchini kupata matokeo chanya huku akieleza kuwa katika mpango wa dharura ambao Ofisi ya Waziri Mkuu inaratibu kupitia Idara ya Menejimeti ya Maafa hadi kufikia hatua ya kupata rasimu yake ni jukumu la wote kuboresha na kuthibitisha ili uanze kutumika.

“Maafa ni kitu ambacho kinakuja bila kutegemea, hivyo serikali inajitahidi sana kutoa ushirikiano kutoka kwa mashirika na wadau mbalimbali kutatua ama kutoa huduma mbalimbali katika maeneo yaliyokumbwa na majanga. Pia Serikali inatambua mchango wenu mashirika ya kimataifa (WFP) ambaye kwa sasa ndiye mwenyekiti wa Emergence Coordination Group na pia Agricultural Working Group ambao ni wadau muhimu Sana na wadau wengine wa maendeleo,” alisema Mmuya.

Aidha, alitoa wito kwa wadau wengine wa maendeleo kujitokeza kwa wingi kushirikiana na Serikali ya Awamu hii katika nyanja mbalimbali zinazolenga kuleta maendeleo ya Taifa na kuendelea kubadilishana uzoefu wa namna ya kukabili majanga katika maeneo husika ili shughuli za kiuchumi na kijamiii kufanyika katika mazingira rafiki na salama.
Wadau kutoka Shirika la Afya Duniani wakifuatilia uwasilishwaji wa mada wakati wa kikao hicho, kushoto ni Bw. Brian Bogat ambaye ni Mwenyekiti wa Wadau wa Umoja wa Mataifa wa Shughuli za Maafa na Bw.Juvenal Kisanga (Sekretarieti). (Picha na OWM).

Sambamba na hilo aliwaasa wananchi kufuatilia na kuzingatia taarifa za utabiri wa hali ya hewa zinazotolewa na Mamlaka ya Hali ya Hewa nchini (TMA) kupata elimu na kufahamu tahadhari za kuchukua endapo kutatokea mabadiliko ya hali ya hewa ama mabadiliko ya tabia nchi. 

“Mamlaka ya hali ya hewa Tanzania kwenye utabiri wake wa Septemba 2021 na mwezi Novemba hadi Aprili umeonesha mvua za msimu zitakuwa chache kwa baadhi ya maeneo nchini hali itakayosababisha ukame, kukauka kwa mabwawa, malambo ya maji na kupungua kwa malisho ya mifugo,”alieleza.
Washiriki kutoka Vyombo vya Ulinzi na Usalama wakifuatilia taarifa kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Bw. Kaspar Mmuya (hayupo pichani) wakati wa kikao hicho.(Picha na OWM).

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa wa Ofisi hiyo, Kanali Matamwe Said alieleza kwamba mkutano huo umefanyika kwa lengo la kufanya maandalizi ya kujiandaa na athari zinazoweza kutokea kutokana na utabiri ulio tolewa na Mamlaka ya Hali Hewa.
Naibu Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Bw. Kaspar Mmuya (katikati mwenye miwani) akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu pamoja na wadau kutoka Sekta na Wizara mbalimbali baada ya ufunguzi wa kikao kazi hicho. (Picha na OWM).

“Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo yenye jukumu la kuratibu shughuli za serikali kupitia Idara ya Menejimenti ya Maafa imeamua kukutana na wadau kujadili Mpango huo endelevu ili kuanza kutumika bila kuchelewa kama tunavyofahamu maafa huwa hayatoi taarifa yanatokea wakati ambao hujayatarjia hivyo, serikali haiwezi kukaa kimya lazima ichukue hatua kukabili ili wananchi wake wafanye shughuli zao kwa utulivu,” alibainisha Mkurugenzi huyo.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news