Dar yang'ara ukusanyaji mapato, Waziri Bashungwa ataja walioshika nafasi za juu hadi mwisho

NA GODFREY NNKO

HALMASHAURI ya Jiji la Dar es Salaam imeibuka kinara katika ukusanyaji wa mapato mengi zaidi kuliko halmashauri zote nchini kwa kukusanya shilingi Bilioni 36.2.
Hayo yamesemwa leo Januari 28,2022 jijini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Innocent Bashungwa wakati akiwasilisha taarifa ya nusu mwaka ya mapato ya ndani ya halmashauri kwa kipindi cha Julai hadi Desemba, 2021.

"Katika kuzipima halmashauri zote kwa kigezo cha wingi wa mapato (pato ghafi), Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, limekusanya mapato mengi zaidi kuliko halmashauri zote kwa kukusanya Shilingi Bilioni 36.2, ikifuatiwa na Jiji la Dodoma Bilioni 26.8 na Manispaa ya Kinondoni Bilioni 24.8, Halmashauri 13 kati ya 184 zimekusanya kuanzia Shilingi Bilioni 5 na zaidi,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Pia amesema kuwa, Ofisi ya Rais –TAMISEMI, inao utaratibu wa kutoa taarifa za mapato na matumizi ya mapato ya ndani, kila robo mwaka ili kuongeza uwazi na uwajibikaji, katika ukusanyaji wa mapato ya ndani ya halmashauri nchini. 

"Taarifa hii inaainisha ufanisi wa kila halmashauri, katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, kwa kulinganisha makisio yaliyoidhinishwa, na hali halisi ya utekelezaji. Uchambuzi wa matokeo umeandaliwa kwa kulinganisha aina za halmashauri katika makundi, na kimkoa. 

"Kadhalika, taarifa hii inaonesha mwenendo wa matumizi ya mapato ya ndani, kwa kuainisha matumizi ya halmashauri kwenye miradi ya maendeleo, kwa kuzingatia asilimia 40 au 60, na asilimia kumi 10 ya mapato ya ndani, kwa ajili ya mikopo ya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu,"amesema Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Ufanisi

Mheshimiwa Waziri Bashungwa akizungumzia ufanisi katika Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani kwa Mwaka 2020/21 na Mwaka 2021/22 amesema, kwa mwaka wa fedha 2021/22, halmashauri zimepanga kukusanya Shilingi Bilioni 863.9, kutoka kwenye vyanzo vyake vya ndani. 

Amesema, katika kipindi cha mwezi Julai hadi Disemba 2021, halmashauri zimekusanya jumla ya Shilingi Bilioni 460.2, ambayo ni asilimia 53 ya makisio ya mwaka, sawa na asilimia 107 ya lengo la nusu mwaka. 

"Itakumbukwa kwamba bajeti ya makusanyo ya mapato ya ndani, ya Mamlaka za Serikali za Mitaa iliongezeka kutoka Shilingi Bilioni 814.96 katika mwaka wa fedha 2020/21, hadi Shilingi Bilioni 863.9 katika mwaka wa fedha 2021/22.

"Uchambuzi wa taarifa za mapato ya ndani ya Halmashauri, katika kipindi cha Julai - Disemba 2021, umeonesha kuwepo kwa ongezeko la mapato yaliyokusanywa, kwa kiasi cha Shilingi bilioni 78.9, ikilinganishwa na kiasi kilichokusanywa katika kipindi kama hicho cha Julai - Disemba 2020, sawa na ongezeko la asilimia 21,"amesema Waziri Bashungwa.

Amesema, katika kipindi hiki, halmashauri za Wilaya za Kishapu na Longido, zimeongeza jitihada katika ukusanyaji, ukilinganisha na kipindi kama hiki cha mwaka wa fedha 2020/21, ambapo zilikuwa ni halmashauri za mwisho kwa asilimia ya makusanyo. 

Pia amesema, zipo baadhi ya halmashauri ambazo katika kipindi cha Julai hadi Disemba 2021, ufanisi wa kukusanya umeshuka, ukilinganisha na kipindi kama hiki cha Julai hadi Disemba 2020. 

"Moja ya halmashauri hizo ni Halmashauri ya Wilaya ya Masasi, ambayo iliongoza kwa asilimia 88 na sasa imeshuka kwa asilimia 20 tu,"amesema Waziri Bashungwa.

Mwenendo

Waziri Bashungwa akizungumzia juu ya mwenendo wa Ukusanyaji wa Mapato ya Ndani kwa Kipindi cha Julai hadi Disemba, 2021 amesema, uchambuzi wa taarifa kuhusu ufanisi wa halmashauri, katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, unaonesha kuwa halmashauri 113 zimekusanya kwa asilimia 50 au zaidi ya lengo la mwaka na halmashauri 71 zimekusanya chini ya asilimia 50. 

"Ulinganisho wa ufanisi wa ukusanyaji wa mapato ya ndani, unaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang' imeongoza katika halmashauri zote 184, kwa kukusanya asilimia 102 ya makisio yake ya mwaka inafuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Kaliua, Shinyanga, na Mlele ambazo zimekusanya kwa asilimia 91 ya lengo la mwaka. 

"Hata hivyo, kuna uwezekano wa halmashauri hizi kuwa na makisio yasiyoakisi uhalisia wa uwezo wake, wa ukusanyaji mapato ya ndani hivyo kuhitaji kufanya mapitio ya bajeti, ili kuongeza bajeti ya makusanyo, na kuweza kuendelea kufanya matumizi ya fedha kutoka kwenye makusanyo hayo,"amebainisha Waziri Bashungwa. 

Mheshimiwa Bashungwa amesema kuwa,Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli na Kilindi, zimekuwa za mwisho kwa kukusanya asilimia 27 na zinafuatiwa na Halmashauri Wilaya ya Bunda ambayo imekusanya asilimia 28.

Manyara juu 

Wakati huo huo, Mheshimiwa Bashungwa amesema kuwa, Mkoa wa Manyara umeongoza kwa kukusanya asilimia 69 ya lengo la mwaka, ikifuatiwa na Mkoa wa Songwe asilimia 68, Mkoa wa Njombe asilimia 64 na Ruvuma asilimia 61. 

Amesema, Mkoa wa Kilimanjaro umekuwa wa mwisho kwa kukusanya asilimia 43, ukifuatiwa na Mkoa wa Kigoma asilimia 44, na Mkoa wa Mara asilimia 45. 

Mapato ya ndani

Akizungumzia kuhusiana na Mapato ya Ndani ya Halmashauri kwa Kuzingatia aina (kundi) ya Halmashauri ambapo ameanzia na halmashauri za majiji Mheshimiwa Waziri Bashungwa amesema kuwa,kundi hilo linajumuisha halmashauri sita. 


"Kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22, Halmashauri ya Jiji la Tanga, limeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 56 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Arusha asilimia 55, na Halmashauri ya Jiji la Mwanza asilimia 54. 

"Aidha, Halmashauri ya Jiji la Mbeya limekuwa la mwisho, katika kundi hili ambapo limekusanya asilimia 45 ya makisio yake ya mwaka ikifuatiwa na Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam asilimia 52, na Jiji la Dodoma asilimia 53,"amesema Mheshimiwa Bashungwa.

Halmashauri za Manispaa 

Mheshimiwa Waziri Bashungwa akizungumzia, kundi hili ambalo linajumuisha halmashauri 20 amesema kuwa, kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22, Halmashauri ya Manispaa ya Kahama, imeongoza kwa kukusanya mapato kwa asilimia 67 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma asilimia 65, na Manispaa ya Ilemela asilimia 55.

Amesema, katika kundi hili Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, imekuwa ya mwisho ambapo imekusanya asilimia 37 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Manispaa ya Kigoma asilimia 38 na Ubungo asilimia 40.

Halmashauri za Miji 

Amesema, kundi hili linajumuisha halmashauri 21 ambapo kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22, Halmashauri ya Mji wa Mbulu imeongoza kwa kukusanya asilimia 83 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Miji ya Tunduma asilimia 79, na Njombe asilimia 73. 

Pia amesema,Halmashauri ya Mji wa Korogwe imekuwa ya mwisho kwa kukusanya asilimia 39 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Mji ya Nzega asilimia 42, na Halmashauri ya Mji Masasi asilimia 42.

Halmashauri za Wilaya

Wakati huo huo, Mheshimiwa Bashungwa akizungumzia kundi hili ambalo linajumuisha halmashauri 137 amesema kuwa, kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22 Halmashauri ya Wilaya ya Hanang, imeongoza kwa kukusanya asilimia 102 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri za Wilaya ya Kaliua, Shinyanga, na Mlele ambazo zimekusanya kwa asilimia 91. 

Aidha, Halmashauri za Wilaya ya Bumbuli na Kilindi zimekuwa za mwisho katika kundi hili kwa kukusanya asilimia 27 ya makisio yake ya mwaka, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Bunda ambayo imekusanya kwa asilimia 28 ya makisio yake ya mwaka.

Matumizi 

Akizungumzia kuhusu matumizi ya mapato ya ndani katika miradi ya maendeleo, Mheshimiwa Bashungwa amesema kuwa,uchambuzi wa taarifa za matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa kipindi cha kuanzia Julai hadi Disemba 2021, ikiwa ni nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22, unaonesha kuwa halmashauri zimetumia Shilingi Bilioni 129.1.

Matumii ambayo ni sawa na asilimia 76 ya fedha zilizopaswa kutumika kwenye miradi ya maendeleo kwa kipindi cha nusu mwaka. 

Aidha, amesema kwa kipindi hiki kiasi kilichopaswa kutumika ni Shilingi Bilioni 170.4 ambazo ni asilimia 40 au 60 ya mapato yasiyolindwa yaliyokusanywa ambayo ni Shilingi Bilioni 356.7. 

"Halmashauri 31 zimetumia asilimia 100 au zaidi ya kiasi kilichopaswa kutumika kwenye Miradi ya Maendeleo, Halmashauri 128 zimetumia kati ya asilimia 50 na 99 ya kiasi kilichopaswa kutumika kwenye Miradi ya Maendeleo, Halmashauri 25 zimetumia chini ya asilimia 50 ya kiasi kilichopaswa kutumika kwenye Miradi ya Maendeleo. 

"Aidha, taarifa zinaonesha kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji imeongoza kwa kuchangia asilimia 148 kwenye Miradi ya Maendeleo ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro kwa asilimia 146, na Halmashauri ya Wilaya ya Hanang kwa asilimia 142. 

"Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma imekuwa ya mwisho kwa kuchangia asilimia 18, kwenye Miradi ya Maendeleo ikifuatiwa na Halmashauri ya Bumbuli kwa asilimia 20, na Halmashauri ya Mji ya Mafinga kwa asilimia 26,"amefafanua Mheshimiwa Waziri Bashungwa.

Mikopo

Katika hatua nyingine, Waziri Bashungwa amezungumzia kuhusu mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu amesema kuwa,uchambuzi wa taarifa za matumizi ya fedha za mapato ya ndani kwa kipindi cha kuanzia mwezi Julai hadi Disemba 2021, ikiwa ni nusu mwaka kwa mwaka wa fedha 2021/22, unaonesha kuwa halmashauri zimechangia kiasi cha Shilingi Bilioni 27.6, kwenda kwenye vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. 

"Hii ni asilimia 77 ya kiasi kilichopaswa kuchangiwa kwa kipindi cha nusu mwaka, kwa mwaka wa fedha 2021/22 ambacho ni Shilingi Bilioni 35.7. Fedha hizi zinatokana na asilimia 10 ya mapato halisi ya vyanzo visivyolindwa, yaliyokusanywa katika kipindi hiki, ambayo ni Shilingi Bilioni 356.7. 

"Aidha, halmashauri 28 zimechangia asilimia 100 au zaidi, halmashauri 137 zimechangia kati ya asilimia 50 na 99, na halmashauri 19 zimechangia chini ya asilimia 50, kwenye mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu. 

"Aidha, Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga haikuchangia kiasi chochote kwenye mfuko huu, kwa kipindi hiki ambapo sababu waliyoitoa ni kwamba wamenunua pikipiki na bajaji zenye thamani ya shilingi 94,217,000, ambapo mchakato wake ulianza mwezi Desemba 2021, na umekamilika Januari 2022,"amesema Waziri Bashungwa. 

Pia amesema kuwa, taarifa zinaonesha kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Singida, imeongoza kwa kuchangia fedha za vikundi kwa asilimia 142, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti asilimia 139, na Halmashauri ya Mji wa Masasi asilimia 122. 

Mheshimiwa Bashungwa amesema kuwa,Halmashauri ya Manispaa ya Sumbawanga imekuwa ya mwisho, kwa sababu haijachangia kiasi chochote, ikifuatiwa na Halmashauri ya Wilaya ya Namtumbo, ambayo imechangia asilimia 7, ikifuatiwa na Jiji la Mbeya asilimia 24. 

Maelekezo

Katika hatua nyingine, Waziri Bashunwa ametoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa kwa ajili ya halmashauri za majiji, manispaa, miji, na halmashauri za wilaya ambapo amewataka wahakikishe kuwa halmashauri zote ambazo zimekusanya chini ya asilimia 50 ya lengo la mwaka la makusanyo ya ndani, zinawasilisha maelezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI.

"Ni kuhusu sababu za kushindwa kufikia lengo la makusanyo ndani siku 14, baada ya kusomwa kwa taarifa hii. Maelezo hayo pia yabainishe mikakati ya jinsi ya kuboresha mapato ya ndani, katika kipindi cha nusu mwaka kilichosalia (Januari hadi Juni 2022) ili kuweza kufikia malengo ya makusanyo.

"Wakuu wa mikoa wahakikishe kuwa, halmashauri ambazo zimetumia chini ya asilimia 100, ya asilimia 40/60 ya kiasi kilichokusanywa kutoka katika mapato yasiyolindwa, kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka 2021/22, kwa ajili ya miradi ya maendeleo, zinawasilisha maelezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI.

"Ni kuhusu sababu za kushindwa kupeleka asilimia 100 ya fedha hizo za maendeleo. Maelezo hayo yaonyeshe pia mikakati ya jinsi ya kutimiza malengo ya kuchangia miradi ya maendeleo kwa asilimia 100. Aidha, maelezo haya yawasilishwe ndani ya siku 14 baada ya kusomwa kwa taarifa hii.

"Wakuu wa mikoa wahakikishe kuwa Halmashauri ambazo zimetumia chini ya asilimia 100 ya kiasi kilichokusanywa kutoka katika mapato yasiyolindwa, kwa kipindi cha nusu mwaka kwa mwaka 2021/22, kwa ajili ya asilimia 10 ya mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, zinawasilisha maelezo kwa Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, kuhusu sababu za kushindwa kupeleka asilimia 100 ya fedha hizo. 

"Maelezo hayo yaonyeshe pia mikakati ya jinsi ya kutimiza malengo ya kuchangia kwa asilimia 100 fedha za mikopo. Aidha, maelezo haya yawasilishwe ndani ya siku 14 baada ya kusomwa kwa taarifa hii.

"Wakuu wa mikoa wasimamie na kufanya uchambuzi wa mahitaji halisi ya mashine za kukusanyia mapato (POS), ili kufahamu upungufu uliopo na kuchukua hatua ili kuziba upungufu huo. 

"Wakuu wa Mikoa wazisimamie Halmashauri, ili kuandaa makisio ya mapato ya Ndani yenye uhalisia kulingana na fursa zilizopo, kwenye Halmashauri zao ikiwa ni pamoja na kuibua vyanzo vipya vya Mapato, ili kuongeza mapato na hatimaye kuboresha utoaji wa huduma.

Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa utaratibu uliotumika kwenye usimamizi na ufuatiliaji wa miradi ya Fedha za mkopo nafuu wa IMF (TCRP), unatumika kwenye kusimamia miradi inayotekelezwa kwa kutumia asilimia 40/60 ya fedha za mapato ya ndani, ili kupata thamani ya fedha zinazotumika.

Wakuu wa Mikoa wahakikishe kuwa, Halmashauri zinatenga fedha kwa ajili ya miradi ya fedha za ndani (40/60%) kama ilivyoidhinishwa kwenye bajeti. Vilevile wahakikishe fedha zinazotengwa haziendi kutekeleza miradi midogo midogo, ambayo katika kutekelezwa kwake haileti matokeo yaliyokusudiwa.

Wakuu wa Mikoa wahakikishe wakati wa kufanya ukaguzi wa Miradi ya Maendeleo wakague na Miradi ya inayotokana na fedha za asilimia kumi (10) inayotolewa kwa makundi ya Wanawake, Vijana na Watu wenye ulemavu. 

Wakuu wa Mikoa wasimamie na kuhakikisha hoja zote za ukaguzi zilizotolewa na Mkaguzi wa nje (CAG) zinajibiwa, zihakikiwe na wakaguzi ili ziweze kufungwa na kupunguza mzigo wa hoja kwa halmashauri. Aidha, hatua stahiki zichukuliwe kwa wote waliosababisha hoja zinazosababisha ubadhirifu wa fedha za umma,"ameagiza Waziri Bashungwa.

Kwa Katibu Mkuu

Waziri Bashungwa amemuelekeza, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais-TAMISEMI ahakikishe Mfumo wa Kielektroniki wa usimamizi wa mikopo ya Wanawake, Vijana na watu wenye ulemavu unakamilishwa na uanze kutumia si zaidi ya Julai 1, 2022.

"Maboresho ya mfumo wa mapato wa LGRCIS (TAUSI) yakamilishwe na mfumo mpya uanze kutumika si zaidi ya tarehe 1 Julai, 2022.Mfumo wa GIS uunganishwe na mifumo yetu ya mapato na ya utoaji wa huduma mbalimbali ili kurahisisha ukusanyaji wa mapato na utoaji wa huduma kwa wananchi,"ameelekeza Waziri Mheshimiwa Bashungwa.

Diramakini

DIRAMAKINI is Tanzanian news media house established to play role in shaping the global agenda through telling true stories by delivering quick and in-depth.Our readers trust our coverage of the issues that matter most to them. Our agenda-setting journalism attracts. Contact us on diramakini@gmail.com OR +255 719 254 464.

Post a Comment

Previous Post Next Post

International news